Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Niebel azuru Afghanistan | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.04.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani Niebel azuru Afghanistan

Amshinikiza Karzai kupambana na rushwa

Waziri Dirk Niebel akishuka katika uwanja wa ndege Kabul

Waziri Dirk Niebel akishuka katika uwanja wa ndege Kabul

Waziri wa misaada ya maendeleo wa Ujerumani, Dirk Niebel, ameanza ziara ya siku tatu nchini Afghanistan hii leo. Bwana Niebel amesema licha ya ufanisi uliopatikana katika kuijenga upya Afghanistan, bado kuna mapungufu katika utawala wa nchi hiyo na katika vita dhidi ya ufisadi.

Akiwa mjini Kabul, waziri Niebel amesema Ujerumani haitatoa pesa ovyo bila mpango kwa sababu walipakodi wa Ujerumani wanafanya kazi ngumu kupata pesa za kulipia kodi. Baada ya kukutana na rais wa Afghanistan Hamid Karzai, waziri Niebel amesema amelikataa pendekezo la serikali ya Afghnistan kutaka ipewe sehemu kubwa ya fedha kutoka Ujeumani kwa matumizi yake.

Akiwa ameandamana na mwenyeji wake rais Karsai pamoja na waziri wa fedha Omar Zakhilwal, na mshauri wa rais Karsai, Dadfar Spanta, kwenye mkutano wa waandishi wa habari mjini Kabul baada ya mkutano wao, waziri Dirk Niebel, ameitaka serikali ya Afghanistan ifanye mengi zaidi kupambana na rushwa.

Mara ya mwisho waziri Niebel aliitembelea Afghanistan miaka minane iliyopita na anatambua kwamba hali ya mambo imebadilika nchini humo.

"Nilipoitembelea Afghanistan miaka minane iliyopita pamoja na waziri wetu wa mambo ya kigeni wa zamani Joschka Fischer, ulikuwa wakati wa tabasamu na kupungiwa mikono. Wanajeshi wetu waliweza kusafiri kwenye magari yaliyo wazi, na walipiga doria vijijini bila ulinzi mkubwa; ambako wakaazi waliwakaribisha kama wageni. Hayo yote yamebadilika na kitisho kimekuwa kikubwa zaidi."

Kutokana na hali mbaya ya usalama, ziara ya waziri Niebel inafanyika chini ya ulinzi mkali, huku kukiwa na hofu ya kufanyika mashambulio dhidi yake. Njia atakazopitia kiongozi huyo, hazikutangazwa na zitabakia siri hadi atakapokamilisha ziara yake. Akiwa mjini Kabul, waziri Niebel atafanya mazungumzo na wajumbe wa serikali ya Afghanistan, lakini atakutana kwanza na rais wa nchi hiyo, Hamid Karzai. Waziri Niebel amesema mazungumzo yake na rais Karzai yamekuwa ya kirafiki, lakini ujume wake uko wazi.

"Tunahitaji bila shaka ushirikiano wa serikali ya Afghanistan na lazima itimize ahadi ilizotoa katika mkutano wa London: kuwezesha utawala bora serikalini, kupambana na ufisadi na kuhakikisha mamlaka halali inatamuliwa na raia. Hilo ndilo sharti letu litakalotuwezesha katika kazi yetu ya kuimarisha jamii ya Waafghanistan na hatimaye kuwezesha kukabidhi jukumu kwa mamlaka za kiraia za Afghanistan."

Hamid Karzai

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai

Waziri Niebel amemsisitizia rais Karzai mabadiliko ya mkakati wa serikali ya Ujerumani nchini Afghanistan. Mkakati mpya wa Ujerumani nchini humo unazipa kipau mbele juhudi za kuwaimarisha raia. Fedha zinazohitajika kwa kufanikisha kazi hiyo kila mwaka zitaongezeka takriban marudufu na kufikia euro milioni 430. Euro milioni 250 zitatoka kutoka bajeti ya wizara ya misaada ya maendeleo ya Ujerumani.

Fedha hizi zinapaswa kutumiwa katika juhudi za kulijenga upya eneo la kaskazini, ambako wanajeshi wa Ujerumani wanahudumu. Waziri Niebel anatarajiwa pia kulitembelea eneo hilo kujionea miradi mbalimbali. Amepongeza ufanisi uliopatika kufikia sasa, lakini hata hivyo akasisitiza umuhimu wa kuboresha zaidi.

Waziri Niebel anataka kwa haraka kusaidia, anataka kuwafikia Waafghanistan wengi zaidi na kusambaza msaada kwa njia nzuri zaidi. Kwa mantiki hiyo, mashirika yasiyo ya kiserikali yanapaswa kushirikiana kwa karibu na jeshi la Ujerumani, Bundeswehr, katika siku za usoni, vinginevyo hayatapewa tena fedha zozote kutoka bajeti ya wizara ya misaada ya maendeleo.

Mwandishi: Josephat Charo/Kleber, Mark/ZPR

Mhariri: Abdul-Rahman

 • Tarehe 01.04.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ml2i
 • Tarehe 01.04.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Ml2i
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com