1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri Mkuu wa Israel aelekea Washington kwa ziara rasmi

25 Agosti 2021

Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennett ameelekea mjini Washington Marekani kukutana na Rais Joe Biden, ikiwa ni ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu alipoingia madarakani miezi miwili iliyopita.

https://p.dw.com/p/3zSBL
Bildkombo Naftali Bennett und Joe Biden

Ziara ya Bennett inakusudia kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kufikia mwafaka juu ya adui wa muda mrefu wa Israel-Iran. 

Waziri Mkuu wa Israel Naftali Bennette ameelekea nchini Marekani, ikiwa ni safari yake ya kwanza nje ya nchi kama Waziri Mkuu.

Soma zaidi: Morocco, Israel zasaini mikataba katika ziara ya kihistoria

Kabla ya kuabiri ndege Bennett alisema, "Sasa naelekea Washington kukutana na Rais wa Marekani Joe Biden, rafiki wa zamani na rafiki wa kweli wa Israel. Jumatano hii napanga kukutana na maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani. Kuna utawala mpya nchini Marekani na pia kuna serikali mpya Israel, napeleka ujumbe wa ushirikiano mpya, ambao umejengeka kutokana na uhusiano mzuri wa muda mrefu kati ya nchi hizi mbili"

Ziara ya Waziri Mkuu huyo nchini Marekani inatokea katikati ya msuguano kati ya Israel na Iran.

Israel pia inakabiliwa na ongezeko la kitisho cha usalama kwenye mpaka wake wa kusini na Ukanda wa Gaza, ikiwa ni chini ya miezi mitatu baada ya kutokea kwa vita na kundi la wanamgambo la Hamas vilivyodumu kwa siku 11.

Israelische Armee im Westjordanland 20.06.2014
Wanajeshi wa Israel wakati wa uvamizi kwenye kijiji cha Arura, kaskazini mwa Ramallah.Picha: picture-alliance/dpa

Bennett anatarajiwa kukutana na maafisa wakuu wa Marekani akiwemo Waziri wa mambo ya nje Anthony Blinken na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin, kabla ya kufanya mkutano mnamo siku ya Alhamisi na Rais Joe Biden wakati wa ziara yake ya siku mbili.

Soma zaidi: Israel kuichunguza kampuni yake ya ujasusi

Mkutano huo utakuwa wa kwanza kati ya viongozi hao wawili, na ziara ya kwanza ya kidiplomasia ya Bennette kuifanya kama Waziri Mkuu, katika wakati ambapo hali ya usalama ni tete katika ukanda wa Mashariki ya kati.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu huyo wa Israel imesema, kipau mbele katika mazungumzo yake na Biden ni Iran, hasa juu ya mpango wake wa nyuklia. Kati ya mambo mengine watakayojadiliana ni uimarishaji wa jeshi la Israel na janga la ugonjwa wa Covid-19.

Kisiasa, viongozi hao wawili wanajaribu kuonyesha ukomavu wao juu ya kushughulikia masuala mbalimbali ikiwemo kadhia ya nchini Afghanistan.

Wachambuzi wa kisiasa wanatumai kuwa mazungumzo hayo yataimarisha uhusiano kati ya Marekani na Waziri Mkuu huyo, anayeegemea siasa kali za mrengo wa kulia aliyemaliza utawala wa miaka 12 wa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.