1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Morocco, Israel zasaini mikataba katika ziara ya kihistoria

Bruce Amani
12 Agosti 2021

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa Morocco na Israel wameasaini mikataba mitatu, wakati wa ziara ya kwanza ya afisa wa ngazi ya juu wa taifa hilo la Kiyahudi tangu nchi hizo mbili ziliporejesha mahusuano yao mwaka jana

https://p.dw.com/p/3yrvH
Marokko | Israels Außenminister Lapid in Marokko
Picha: Mosa'ab Elshamy/AP/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Morocco Nasser Bourita na mwenzake wa Israel Yair Lapid walisaini jana makubaliano kuhusu mashauriano ya kisiasa, sekta ya anga na utamaduni.

Lapid aliwaambia waandishi wa habari kuwa mikataba hiyo italeta uvumbuzi na fursa za nchi hizo kwa manufaa ya vizazi vijavyo. "Tulifanikiwa nini kutokana na miaka hii yote ya uhasama wakati mahusuano kati ya mataifa yetu ya jadi na ya kifahari yalikatwa? Hakuna. Raia wetu walipata nini? Hakuna. Leo tunabadilisha hili kwa faida ya utalii na uchumi, kwa biashara na mabadilishano ya utamaduni, kwa urafiki na ushirikiano." Amesema Lapid.

Israel na Morocco zilifikia muafaka mwishoni mwa mwaka jana baada ya aliyekuwa Rais wa Marekani Donald Trump kuitambua haki ya uhuru unaopambaniwa vikali na Morocco wa eneo la Sahara Magharibi.

Morocco ilikuwa nchi ya nne ya Kiarabu kuweka mahusiano na Israel mwaka jana baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain na Sudan.

Wapalestina hakufurahishwa

Hatua hiyo iliwakarisisha Wapalestina, kwa sababu iliyavunja makubaliano ya nchi za Kiarabu yaliyodumu muda mrefu kuwa kusiwe na mahusiano hadi Israel iukubali mpango mpana na wa kudumu wa amani.

Bourita alisema kuwa wakat iwa mazungumzo yake na Lapid, hali nchini Israel na maeneo ya Wapalestina ilijadiliwa. "Leo, kuna haja ya kurejesha uaminifu kati ya pande zote ili kuleta amani, utulivu na mazingira yanayowiri katika kanda hii. Kujenga upya uaminifu, kuweka utulivu na kujizuia kuchochea mvutano ni muhimu ili kufungua njia ya suluhisho la kisiasa kwa mgogoro wa Wapalestina na Israel linalozingatia suluhisho la mataifa mawili." Amesema Bourita.

Mfalme wa Morocco Mohammed VI alimhakikishia Rais wa Palestina Mahmud Abbas baada ya kurejeshwa mahusiano kuwa Morocco itaendelea kuunga mkono harakati za Kipalestina.

Hii leo Lapid anazindua rasmi uwakilishi wa kidiplomasia wa Israel katika mji mkuu Rabat.

Waziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani Antony Blinken amesema ziara ya Lapid ni muhimu kwa Israel, Morocco na kanda nzima ya Mashariki ya Karti.

AFP