Washington. Benki kuu ya dunia yaidhinisha ufutaji madeni.
26 Septemba 2005Kamati ya maendeleo ya benki kuu ya dunia imeidhinisha mpango wa kufuta madeni kwa ajili ya mataifa masikini zaidi duniani.
Hii inafuatia uamuzi wa shirika la fedha la kimataifa siku ya Jumamosi kuunga mkono mpango huo ambao utafuta zaidi ya dola bilioni 55 za madeni ya nchi nyingi za Afrika.
Tamko hilo limekuja mwishoni mwa mikutano kadha na shirika la fedha la kimataifa IMF katika mji mkuu wa Marekani Washington.
Bodi za watendaji za mashirika yote mawili zinapaswa sasa kutoa idhinisho la mwisho. Mpango wa kufuta madeni ulipendekezwa hapo kabla katika mkutano wa mataifa manane yenye utajiri wa viwanda duniani G8 uliofanyika huko Gleneagles, Scotland.