Wanasiasa Ujerumani na juhudi za kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.01.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Wanasiasa Ujerumani na juhudi za kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi

Vyama vingi katika bunge la Ujerumani vinataka kuanzishwe nafasi ya kamishna wa kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi.

Hatua hiyo haiwezi kubadilisha hali mbaya inayozidi, lakini hata hivyo inatoa ishara muhimu. Hayo ni kwa mujibu wa maoni ya mwandishi wa DW Jens Thurau.

Chuki dhidi ya Wayahudi huwa zinaonekana katika aina tofauti. Ipo tangu zamani, toka enzi za mauaji ya Wayahudi wa Ulaya yaliyofanywa na utawala wa Kinazi katika miaka ya 1930 na 1940. Chuki hiyo ilikuwepo hadi baada ya vita vya Ujerumani Mashariki na Magharibi na ukweli ni kwamba ilifanywa kuwa kinyume cha sheria, ingawa imesaidia kwa kiasi kidogo.

Hivi leo nchini Ujerumani, chuki dhidi ya Wayahudi bado inatoka katika jamii ya wanaofuata siasa kali za mrengo wa kulia. Imezidi kuwa mbaya baada ya kuingia kwa wahamiaji kutoka mataifa ya Kiarabu, ambao mara nyingi wanakataa kuitambua Israel. Hisia hiyo imejitokeza ulimwenguni baada ya bendera za Israel kuchomwa moto mjini Berlin na kwenye miji mingine ya Ujerumani, kwa lengo la kupinga uamuzi wenye utata wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuitambua Jerusalem kama mji mkuu wa Israel.

Ikiwa ni zaidi ya miaka 70 baada ya kumalizika kwa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia, kuona matukio kama hayo yanayojitokeza nchini Ujerumani, ni jambo lisilokubalika. Lakini kuchoma moto bendera sio tatizo pekee. Imeripotiwa kuwa Wayahudi wa Ujerumani wanachukua tahadhari zaidi kuhusu kuweka au kubandika alama za utambulisho wao wa Kiyahudi katika umma, kama vile Nyota ya Daudi. Hatua hiyo ndiyo hasa muafaka kwa wanasiasa kupeleka ujumbe.

Thurau Jens Kommentarbild App

Mwandishi wa DW, Jens Thurau

Chama cha kihafidhina cha Christian Democratic, CDU na chama ndugu cha Christian Social Union, CSU, Chama cha Social Democratic, SPD, chama kinachowapendelea wafanyabiashara cha Free Democratic, FDP na chama kinacholinda mazingira cha Kijani, vyote vinataka kuanzishwa kwa nafasi mpya serikalini ambayo ni kamishna wa kupambana na chuki dhidi ya Wayahudi. Kamishna huyo atakuwa na majukumu ya kukusanya taarifa kuhusu matukio ya chuki dhidi ya Wayahudi, kushinikiza mipango ya elimu katika shule na kuanzisha nafasi zaidi kuhusu mada hiyo ndani ya nyanja za kisiasa.

Inaonyesha kuwa mwiko huo umevunjwa katika muda huu zinapoongezeka siasa za kizalendo na za mrengo wa kulia. Ndiyo maana kiongozi wa chama kinachofuata siasa kali za mrengo wa kulia na kinachopinga wahamiaji, AfD, Björn Höcke ameyaita makumbusho ya mauaji ya halaiki dhidi ya Wayahudi kama ''mnara wa aibu'' bila ya kujali madhara yatakayojitokeza, hata ndani ya chama chake mwenyewe.

Bila shaka mwanahistoria wa Ujerumani mwenye asili ya Israel, Michael Wolffsohn alikuwa sahihi aliposema chuki dhidi ya Wayahudi umekuwepo kwa maelfu ya miaka. Pia yuko sahihi kusema kwamba Ujerumani tayari ina sheria katika vitabu ambazo kwa uwazi zinapiga marufuku chuki dhidi ya Wayahudi na zinahitaji tu kutekelezwa.

Bado inabakia muhimu kwa Ujerumani kuona aibu na kuwajibika kwa mauaji ya kimbari ya Wayahudi wa Ulaya. Wakati chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani inaanza kuongezeka, ni wajibu wa wanasiasa kuanza kuchukua hatua. Kwa hoja hiyo ya hivi karibuni, ni jambo sahihi kulifanya.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DW http://bit.ly/2BdyBRJ,
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com