1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani

Sekione Kitojo21 Desemba 2010

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazungumzia kuhusu uchaguzi huko Belarus , ziara ya waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Seehofer nchini jamhuri ya Czech.

https://p.dw.com/p/QhIx

Wahariri  wa  magazeti  ya  hapa  Ujerumani  wamejishughulisha zaidi  hii  leo  na  hali   baada  ya  uchaguzi  huko  Belarus,  ziara  ya waziri  mkuu  wa  jimbo  la  Bavaria  nchini  Ujerumani  Horst Seehofer  huko   jamhuri  ya  Czech , na  pia  barafu  nyingi inayoanguka  katika  bara  la  Ulaya  na  kusababisha  kuvurugika kwa  safari.

Tukianza  na  hali  huko  nchini  Belarus, gazeti  la  Nordwest Zeitung la  Oldenburg  linaandika.

Iwapo Urusi  haitaacha  kuyanyooshea  kidole  mataifa  ya magharibi  kutokana  na  shutuma  zake, hali  haitabadilika. Rais  wa Belarus  Lukashenko  anaendelea  kuwa   na  uhuru  wa  kufanya atakavyo  licha  ya  miito, vitisho  na  pia  kuzuiwa   kusafiri  katika mataifa  ya  umoja  wa  Ulaya.  Ni  watu  wa  Belarus  pekee  ambao wanaweza  kubadilisha  hali  hiyo. Umoja  wa  Ulaya  unaweza  tu kutoa  msaada  wa  kiutu.  Lakini  hali  bado  inaonekana   kuwa  ni mbaya. Matamshi  ya  Lukashenko  kwamba  wapinzani watashughulikiwa  kwa  nguvu  zaidi,  hayaleti  matumaini  kabisa.

Gazeti  la  Sächsische  Zeitung  la  mjini  Dresden  likizungumzia kuhusu  mada  hiyo  linaandika.

Lukashenko  anaendelea  kufanya  kile  atakacho. Kwa  kuwakamata watu  kadha   pamoja  na   kuwashambulia  waandamanaji  ambao wanapinga  matokeo  ya   uchaguzi  wa  rais , ameendelea kusherehekea  ushindi  wa  kuchaguliwa  kwake. Hakuna  jipya  kwa hiyo  kutoka  Minsk  mji  mkuu  wa  Belarus, na  kila  mmoja angeshangaa  iwapo  kungekuwa  na  jipya.

Mhariri  wa  gazeti  la  Rhein - Neckar-Zeitung  la  mjini  Heidelberg anazungumzia  ziara  ya  waziri  mkuu  wa  jimbo  la  Bavaria  nchini Ujerumani  huko  jamhuri  ya  Czech.  Gazeti  linaandika.

Horst  Seehofer  na  mwenzake   wa  jamhuri  ya  Czech  Petr Necas wamezungumzia  pia  masuala  kadha  ya  kisiasa   katika  mkutano wao  mjini  Prag, pamoja  na   masuala  ya  kiuchumi, kitamaduni  na pamoja  na  mambo  kadha   mengine  ya  kawaida. Mzozo  kuhusu suala  la  kufukuzwa  Wajerumani  waliokuwa  wakiishi  nchini  humo hata  hivyo  halijatatuliwa. Suala  hilo  hata  hivyo  limetupwa  nje  ya mjadala.  Hali  ya  kuongeza  ushirikiano ni  njia  ambayo  inatumika hapa  kuondoa  hali  ya  kutoweza  kuzungumzia  chochote kilichotokea  katika  wakati  baada  ya  vita.

Kufukuzwa  kwa  Wajerumani  waliokuwa  wakiishi  katika  ardhi  ya jamhuri  ya  Czech   na  mauaji  ni  suala  ambalo ni  tata, na wanasiasa  wa  nchi  hiyo  wanatetea   hatua   hiyo  kuwa  ilikuwa  ni lazima  wakati  huo, lakini  hata  Seehofer  anataka  kuchukua mtazamo  mwingine  wa  ushirikiano  kama  mtaji  kati  ya  nchi  hizi mbili.

Gazeti  la  Märkische  Oderzeitung  la  mjini  Frankfurt -Oder linazungumzia  kuhusu  hali  ya  mtafaruku  iliyosababishwa  na kuanguka   kwa  theluji  nyingi  barani  Ulaya  hivi  sasa. Gazeti linaandika.

Kila  mwaka  hali  ni  ile  ile, wanasema  maafisa  na  makampuni. Tuko  tayari  kwa  majira  ya  baridi.  Huo  ni  wakati  ambao  hakuna barafu.  Mara  baada  ya   kuanza  kuanguka  barafu, hayo  huyasikii tena  wala  kuyaona. Mara  hii  tumejifunza  zaidi  kutoka  kwa kampuni  ya  treni. Nyakati  za  majira  ya  baridi  ni  wakati  ambao wasafiri  na  wale  wanaotaka  kwenda  likizo wanajitayarisha  kwa matatizo. Lakini  kama  walipa  kodi  na  wateja  wanaona  kuwa majigambo  ya  wakati  wa  majira  ya  mapukutiko  kwamba  wako tayari  kwa  majira  ya  baridi  ni maneno  matupu  ambayo yameishia  kuganda  wakati  huu  wa  baridi  kali.

Mwandishi : Sekione  Kitojo  / Inlandspresse

Mhariri:  Abdul-Rahman