Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya Rais Mubarak kupewa hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani | Magazetini | DW | 09.02.2011
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanatoa maoni juu ya Rais Mubarak kupewa hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani

Wahariri wanasema Mubaraka asipewe hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani.

default

Rais Hosni Mubarak wa Misri. Jee atapewa hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya minong'ono inayohusu rais Mubarak wa Misri kupewa hifadhi nchini Ujerumani. Wahariri hao pia wanazungumzia juu ya mchango wa mtandao wa Internet katika mapinduzi yanayotokea kaskazini mwa Afrika. Na gazeti la Frankfurter Rundschau linatoa maoni juu ya kile linachoita mfarakano nchini Sudan.

Jee Rais Hosni Mubarak atapewa hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani.? Ipo minong'ono juu ya uwezekano huo.Na wananchi wa Ujerumani wanataka kujua ukweli kama anavyosema mhariri wa gazeti la Münchner Merkur.

"Sauti za juu zinasikika kuhusu uwezekano wa Rais Hosni Mubarak wa Misri kupatiwa hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani"

Lakini gazeti hilo linasema wahusika serikalini wamegawanyika katika pande mbili. Hata hivyo mhariri anatilia maanani, kuwa Mubarak ana ahadi ya kukutana na daktari ili kuendelea na matibabu nchini Ujerumani. Na kwa sababu za kibinadamu mtu hawezi kumnyima Rais huyo haki ya kupatiwa matibabu; na ikiwa matibabu hayo yatatoa fursa kwa Mubarak kuondoka Misri kabisa, kwa staha, basi hilo litakuwa jambo zuri, litakaloendeleza mchakato wa kuleta demokrasia nchini Misri.

Lakini mhariri wa gazeti la Lübecker Nachrichten hakubaliani na hoja juu ya kumpa Mubarak hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani.Mhariri wa gazeti hilo anaeleza kuwa ni sawa kabisa kumpa Rais Mubarak haki ya kufanyiwa matibabu nchini Ujerumani. Lakini baada ya kutibiwa lazima aondoke Ujerumani. Madikteka wasipewe hifadhi asilani nchini Ujerumani. Mubarak anaweza kwenda Saudi Arabia ili kupata hifadhi,kwani huko atakutana na madikteta wenzake.

Mhariri wa gazeti la Nürnberger Nachrichten leo anazungumzia juu ya mchango wa mtandao wa internet katika harakati za upinzani. Lakini mhariri huyo anaeleza kuwa mtandao wa internet ni sawa na kisu chenye makali katika pande zote mbili.Mhariri huyo anasema watawala katika nchi kama Iran, Saudi Arabia au China wamezitambua siku nyingi athari za internet.Na wanapoona watu wao wanajiandaa kuanzisha upinzani, wanayakata mawasiliano yote ya mtandao. Kwa kuwa watawala hao wenyewe wanatumia mtandao kueneza propaganda zao, wanauhofia mtandao kwa sababu ni vigumu kuyadhibiti maudhui yanayowasilishwa.

Gazeti la Frankfurter Rundschau linasema katika maoni yake leo kwamba kuachana pia kunaweza kuwa jambo la furaha. Gazeti hilo linazungumzia juu ya uamuzi wa watu wa Sudan ya Kusini kujitenga na Sudan ya Kaskazini

Gazeti hilo linaeleza kwamba kwa muda wa nusu karne watu wa Sudan ya Kusini walikuwamo katika ndoa ya maafa. Kwa hiyo kupiga kura kwa asilimia 99 kuchagua kujitenga, maana yake ni mwisho wa jinamizi lililokuwa linawainamia watu hao.

Mwandishi/Mtullya /Deutsche Zeitungen/

Mhariri/Abdul-Rahman .....

 • Tarehe 09.02.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10E0b
 • Tarehe 09.02.2011
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/10E0b