1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wahafidhina wanaongoza katika orodha ya wagombea urais Iran

Tatu Karema
25 Mei 2021

Iran siku ya Jumanne iliwaidhinisha wagombea saba wa uchaguzi wa rais utakaofanyika mwezi ujao, orodha iliyokuwa na majina mengi ya kihafidhina huku aliyekuwa spika wa bunge Ali Larijani akikosa kuorodheshwa .

https://p.dw.com/p/3tw9l
Iran Tehran | Iranischer Präsident | Hassan Rouhani
Picha: Iranian Presidency/Anadolu Agency/picture alliance

 

Hatua hiyo huenda ikatoa fursa kubwa kwa mkuu mmoja wa mahakama Ebrahim Raisi katika uchaguzi huo wa Juni 18 unaofanyika wakati Iran inatafuta kuokoa mkataba wake wa nyuklia na mataifa yenye ushawishi duniani.

 

Raisi alipata ushindi wa asilimia 38 katika uchaguzi wa mwaka 2017 lakini akashindwa kwa kura kidogo na rais wa sasa Hassan Rouhani ambaye katiba inamzuia kuwania muhula wa tatu madarakani. Baraza la usimamizi, linalowasaili wagombea wa uchaguzi pia lilimzuia aliyekuwa rais Mahmoud Ahmadinejad kushiriki katika uchaguzi huo. Orodha hiyo iliyotangazwa na waziri wa mambo ya ndani wa taifa hilo, imeonekana kabla ya tangazo rasmi na kuzua shutuma kutoka kwa wana mageuzi na pia wahafidhina.

Ushindani ulitarajiwa kuwa vipi?

Vyombo vya habari vilikuwa vimebashiri ushindani mkali kati ya Raisi na Larijani ambaye kwa sasa ni mshauri wa kiongozi mkuu wa kidini Ayatollah Ali Khamenei. Wana mageuzi walikuwa wameweka matumaini yao kwa Eshaq Jahangiri, naibu rais wa kwanza wa rais wa sasa Hassan Rouhani, lakini pia amezuiwa kushiriki.

Iran Präsidentschaftswahlen Kandidaten
wagombea urais walioidhinishwa nchini IranPicha: ASSOCIATED PRESS/picture alliance

Mhariri mkuu wa kituo cha habari cha Tasnim kinachoegemea siasa za mrengo wa kihafidhina Kian Abdollahi, amesema kuwa hatua ya baraza hilo ya kuwazuia wagombea kadhaa muhimu sio haki kwa umma na kwamba sehemu kubwa ya wahafidhina wameipinga hatua hiyo.

Usiku wa Jumatatu, kituo cha habari cha Fars kiliripoti kuzuiwa kushirika katika uchaguzi huo kwa wanasiasa hao watatu wakuu. Kiliitaja hatua hiyo kama ''kupinga wale wanaodumisha hali ilivyo'' hii ikimaanisha kuwa waliozuiliwa wanahusika kwa matatizo makubwa ya kiuchumi na kijamii nchini Iran.

Uchaguzi huo unafanyika wakati ambapo mataifa yenye ushawishi duniani yanakutana mjini Vienna katika juhudi za kuishirikisha tena Marekani katika mkataba wa nyuklia wa Iran ambao Marekani ilijitoa mwaka 2018.

Athari za kujiondoa kwa Marekani katika mkataba wa nyuklia wa Iran

Kujiondoa kwa Marekani katika mkataba huo chini ya aliyekuwa rais Donald Trump na kuwekewa upya vikwazo kwa Iran kulilisababisha taifa hilo kuimarisha shughuli zake za nyuklia. Larijani, aliyeunga mkono mkataba huo wa mwaka 2015, siku ya Jumanne alikubali kuondolewa kwake katika uchaguzi huo, ijapokuwa ana muda wa hadi Jumanne saa sita usiku kukata rufaa.

Wanasiasa wengi wanasema kuwa hakuna tena ushindani kwa kuwa kuzuiwa kwa Larijani kunampa ushindi rahisi Raisi. Mchambuzi wa mrengo wa kihafidhina Mohammed Imani, anasema kuwa Raisi tayari alikuwa ameshinda kura zote na inaoonekana kuwa ushindi wake utakuwa na uadilifu zaidi iwapo angekuwa na upinzani zaidi.

Raisi anasema amekuwa na shughuli nyingi tangu siku ya Jumatatu akipiga simu na kufanya mashauriano ya kuwashirikisha wagombea zaidi katika uchaguzi huo.