Waasi wa Syria walitumia silaha za gesi ya Sarin yasema Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.07.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Waasi wa Syria walitumia silaha za gesi ya Sarin yasema Urusi

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa amesema wataalamu wa nchi yake wamebaini waasi wa Syria walitengeneza silaha za kemikali zilizokuwa na gesi ya Sarin na kuitumia kwenye mashambulizi ya eneo la Khan al-Assal.

A Syrian opposition fighter tries a gasmask in the northern city of Aleppo on July 25, 2012. Battles raged through the night in several districts of Syria's second largest city to which the regime had rushed reinforcement, after rebels launched an all-out assault for control of the country's commercial hub on July 20. Arabic graffiti on the police station's entrance reads Assad's Syria. AFP PHOTO / PIERRE TORRES (Photo credit should read Pierre Torres/AFP/GettyImages)

Syrien Kämper mit Gasmaske in Aleppo Chemiewaffen

Kwa mujibu wa Balozi Churkin, mashambulizi hayo yalifanywa tarehe 19 mwezi Machi kwenye eneo la Khan al-Assal nje kidogo ya mji wa Allepo unaodhibitiwa na serikali. Balozi huyo ameelekeza kidole cha lawama kwa wapiganaji wa upinzani kwa mashambulizi hayo yaliyowauwa watu 26 wakiwemo maafisa 16 wa usalama huku wengine 88 wakiwa wamejeruhiwa.

Lakini huku hayo yakiarifiwa waasi nao au wapiganaji wa upinzani wanailamu serikali kwa mashambulizi hayo.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin

Akizungumza na waandishi habari wakati alipokuwa akimkabidhi Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon ripoti ya uchunguzi huo, Churkin amesema utawala wa Assad uliiomba Urusi ambaye ni mshirika wake wa karibu kufanya uchunguzi juu ya mashambulizi hayo baada ya wataalamu wa Umoja wa Mataifa kushindwa kuingia nchini humo kufuatia kutoelewana na Syria.

Balozi Churkin amesema kwa sasa majibu ya uchunguzi huo yanaonesha kuwa silaha zilizotumika hazikutengenezwa kiwandani na zilikuwa zimejaa gesi ya Sarin. Kukosekana kwa udhibiti wa kemikali inayohitajika katika kuiweka kwa muda mrefu inaonesha kwamba imetengenezwa katika siku za hivi maajuzi kwa hivyo kulingana na Churkin hii moja kwa moja inaonesha waasi ndio waliotumia silaha hizo za kemikali katika mashambulizi ya Khan al-Assal

Ban Ki Moon ataka ushahidi zaidi

Hata hivyo Uingereza, Ufaransa na Marekani sasa zimewasilisha ripoti tofauti kwa Umoja wa Mataifa inayozungumzia mashambulizi ya silaha za kemikali nchini Syria.

Marekani inasema inaamini kwamba vikosi vya serikali ya Bashar Al Assad vimewauwa zaidi ya watu 150 kwa kutumia gesi ya Sarin. Kwa upande wake Ban Ki Moon amesema anataka ushahidi zaidi juu ya hilo na sio tu katika eneo moja la Khan al-Assal.

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon

Matumizi ya silaha za kemikali nchini Syria imevuka mpaka aliouweka Rais wa Marekani Barrack Obama wa kutojiingiza moja kwa moja katika mgogoro wa Syria unaoendelea kwa kwa zaidi ya miaka miwili sasa.

Kando na kutuma misaada ya kibinaadamu Marekani imekuwa na wazo la kutuma silaha kwa waasi wa Syria. Tangu kuanza kwa ghasia hizo takribani watu 93,000 wameshauwawa, kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa.

Mwandishi: Amina Abubakar/AP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com