1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Von der Leyen: Trump si mwaminifu

20 Januari 2026

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen ameuelezea mpango wa Rais Donald Trump wa Marekani kuziwekea ushuru nchi za Ulaya kama kosa hasa kati ya washirika wa zamani.

https://p.dw.com/p/578SN
Rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Halmshauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Fabrice Coffrini/AFP

Matamshi hayo ameyatoa wakati ambapo Rais wa UfaransaEmmanuel Macron ameitaka Ulaya isihofie kutumia sheria yake kali ya kibishara dhidi ya Marekani.

Ursula von der Leyen alikuwa akizungumza leo huko Davos nchini Uswisi kulikofunguliwa rasmi Jukwaa la Kiuchumi la Dunia, ambapo ameutilia shaka uaminifu wa Trump akisema, mwaka jana alikubali kutoziwekea ushuru zaidi nchi za Umoja wa Ulaya.

Misukosuko inastahili kuwa fursa kwa Ulaya

Von der Leyen alikuwa analijibu tangazo la Trump kwamba kuanzia Februari bidhaa kutoka nchi nane za Umoja wa Ulaya ambazo zinaiunga mkono Denmark katika azma yake ya kuizuia Marekani kutoichukua Greenland zitawekewa ushuru wa asilimia 10.

Rais wa Marekani Donald Trump
Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Suzanne Plunkett/PA Wire/picture alliance

"Misukosuko ya kikanda inastahili kuwa fursa kwa Ulaya. Kwa mtazamamo wangu, mabadiliko tunayopitia leo ni fursa, isitoshe inatoa haja ya kuunda mfumo mpya wa uhuru wa Ulaya. Ila ukweli pia ni kwamba, tutaweza kuitumia kikamilifu fursa hii, tutakapotambua kuwa mabadiliko haya ni ya kudumu. Kwa hiyo hoja yangu ni, iwapo mabadiliko haya ni ya kudumu, basi Ulaya ni sharti ibadilike kikamilifu pia," alisema Von der Leyen.

Trump amesisitiza kuwa Marekani inakihitaji kisiwa cha Greenland kwa sababu za kiusalama dhidi ya uwezekano wa kitisho kutoka kwa China na Urusi.

Wakati huo huo, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema ulimwengu unapitia kipindi ambacho sheria za kimataifa zinapuuzwa na sheria zinazoonekana kuwa zenye umuhimu ni sheria za wenye nguvu tu.

Akizungumza huko mjini Davos, Macron ameilaani hatua ya Marekani kutaka kuidhoofisha Ulaya kupitia makubaliano ya kibiashara ambayo yanakiuka maslahi yake ya uuzaji bidhaa nje na kulitaka bara hilo likubaliane kikamilifu na matakwa yake.

Heshima ya kimipaka ni muhimu

Macron vile vile amewaambia waandishi wa habari kuwa hana mpango wa kuzungumza na Donald Trump katika Jukwaa hilo la Kiuchumi la Dunia mjini Davos.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron
Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Fabrice Coffrini/AFP

Kwengineko Waziri Mkuu wa Greenland amesisitiza uwepo wa heshima ya kimipaka wakati mzozo kuhusiana na kisiwa hicho unapozidi. Jens-Frederik Nielsen amesema serikali yake inalitazama suala hili kwa umuhimu mkubwa akidai wamefanya mazungumzo na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na washirika wake.

Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen naye ametahadharisha kuwa "mabaya zaidi bado yapo njiani" kwani kwa sasa wanatishiwa na rafiki wao wa karibu zaidi. Frederiksen ameyasema haya huko mjini Copenhagen alipokuwa analihutubia bunge.

Serikali ya Denmark alipata mwaliko wa kushiriki Jukwaa la Kiuchumia Duniani huko Davos, ila msemaji wa jukwaa hilo amesema wawakilishi wa nchi hiyo hawana mpango wa kuhudhuria.

Vyanzo: AP/AFP/Reuters