Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana Rome | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.05.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wakutana Rome

Viongozi wa Umoja wa Ulaya akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wanafanya mazungumzo ya siku mbili mjini Rome yatakayojadili hatua zaidi katika mzozo wa wakimbizi barani humo.

Wakimbizi wakiwasili nchini Italia

Wakimbizi wakiwasili nchini Italia

Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk anakutana na viongozi wenzake wa Umoja huo mjini Rome, Italia akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel katika mazungumzo ya siku mbili juu ya hatua zaidi za kupambana na mzozo wa wakimbizi barani humo.

Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi ambaye ameenza kuonyesha hofu ya nchi yake kuwa kimbilio jipya la wakimbizi baada ya kufungwa kwa njia ya Balkan atafungua mkutano huo katika siku ya kwanza kabla ya Papa Francis kuendelea na mkutano huo hapo kesho.

Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi

Waziri mkuu wa Italia Matteo Renzi

Renzi kwanza atafanya mazungumzo na Kansela Merkel na kufuatiwa na mazungumzo ya pamoja na Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker, rais wa Umoja huo Tusk na kiongozi wa bunge la Ulaya Martin Schulz kabla ya kufanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Tangu Januari mosi idadi ya wahamiaji imefikia 28,500 huku Italia ikirejelea kuwa kituo kikuu cha kwanza cha kuingilia wakimbizi ni kupitia njia ya Mediterania, ikiwa ni baada ya makubaliano tata yaliyofikiwa nchini Uturuki na kufungwa kwa njia ya Balkan.

Italia inahofia kwamba, tofauti na hapo awali, sasa inaweza kuwa na mzigo mkubwa wa kuwapokea wakimbizi ikiwa Austria itaweka udhibiti mkali katika njia ya Brenner inayoiunganisha Italia na Ulaya kaskazini. Mkataba wa uhuru wa kusafiri miongoni mwa nchi za Schengen umekumbwa na vitisho vya mzozo wa wahamiaji barani Ulaya..

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Naye msemaji wa shirika la wakimbizi la Umoja wa Mataifa nchini Italia, Carlotta Sami amepongeza harakati za dharura za kuwa na muundo mzuri, utakaotoa mipango inayoashiria ushirikiano wa kuwapokea wakimbizi pale wanapowasili katika nchi hizo.

Papa Francis pia atafanya mazungumzo na Kansela Merkel hapo keshoItalia kwa sasa imekuwa ikipokea wakimbizi wanaovuka Bahari ya Mediterania na idadi hiyo imezidi kuongezeka na hivyo kuwepo na haja kwa nchi hiyo kutafuta njia za kukabiliana na wakimbizi.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi

Mhariri: Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com