1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G20 wakutana kuvijadili virusi vya Corona

Amina Mjahid
26 Machi 2020

Viongozi wa nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kwa kasi kiuchumi G20 wanakutana kwa njia ya vidio kujadili namna ya kukabiliana na virusi vya Corona pamoja na athari zake za kiuchumi.

https://p.dw.com/p/3a3fs
Coronavirus Belgien Brüssel Intensivstation im Krankenhaus
Picha: Getty Images/AFP/K. Triboillard

Mawaziri wa fedha wa G20 na magavana wa benki kuu walikubaliana wiki hii kuanzisha mpango wa dharura wa kushughulikia mripuko wa virusi hivyo vya Corona ambapo shirika la fedha la kimataifa IMF limesema mripuko huo huenda ukaathiri ukuaji wa kiuchumi duniani, lakini halikutoa habari zaidi juu ya hilo.

Katika mkutano wa leo Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni Tedros Adhanom Ghebreyesus anatarajiwa kuwahutubia viongozi hao wa G20 hii leo kuomba msaada wa kifedha na vifaa vya kujilinda na virusi vya Corona kwa wataalamu wa afya kutokana na ukosefu wa vifaa hivyo duniani.

Akizungumza mjini Geneva hapo jana Ghebreyesus aliuambia mkutano wa waandishi habari kuwa viongozi wana jukumu kubwa la kufanya la kibinaadamu na hasa kwa mataifa yaliyoendelea kiviwanda na yanayostawi kwa kasi kiuchumi G20, huku akitaka mataifa zaidi kuendelea kuchukua tahadhari za kuzuwiya maambukizi ya virusi vya Corona.

Marekani inatarajia kupitisha msuada wa msaada dola trilioni 2.2 kwa ajili ya kuuokoa uchumi wake

USA Amtsenthebungsverfahren | Abstimmung
Wabunge wa Baraza la senate nchini MarekaniPicha: picture-alliance/dpa/Senate Television

Nchini Marekani baraza la senate kwa pamoja huenda likapitisha siku ya Ijumaa msuada wa msaada wa dola trilioni 2.2 kwa ajili ya kuuokoa uchumi wake. Fedha hizo zitaelekezwa kwa makampuni makubwa ya kibiashara, wafanyakazi na mifumo ya afya. Hiki ni kitita kikubwa zaidi cha fedha kuwahi kutolewa katika kuuokoa uchumi katika historia ya Marekani.

Idadi ya waliofariki nchini Marekani pekee imepanda na kufikia watu 1,041 huku takriban watu wengine 70,000 wakiambukizwa.

Duniani kote zaidi ya watu bilioni tatu wanaishi chini ya vizuizi vilivyotangazwa na serikali zao katika kukabiliana na viruisi vya Corona. Lakini Umoja wa Mataifa umeonya leo kuwa hatua hiyo inatishia hali ya ubinaadamu. Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amesema ugonjwa wa COVID 19 unatishia ubinaadamu lakini ni lazima binaadamu wapambane katika kukabiliana nao.

Huku idadi ya vifo duniani ikifikia elfu 21 Uhispania imeungana na Italia kwa kuona idadi ya waathirika ikizidi kuongezeka na kuipiku ile ya China ambako ndio chimbuko la mripuko huo miezi mitatu iliyopita.

Huku kila serikali ikiendelea kuchukua hatua ya kuzuwia kueneo kwa virusi vya Corona Ujerumani imepanga kuwaweka karantini kwa siku 14 abiria watakaoingia kwa ndege kutoka nchi nje ya bara la Ulaya kupunguza maambukizi ya virusi hivyo nchini mwake.

Vyanzo: Reuters, afp, ap