1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa Afrika wakutana Malabo

30 Juni 2011

Hivi leo (30.06.2011), viongozi wa Afrika wameanza mkutano wao wa siku mbili mjini Malabo, Guinea ya Ikweta, mada kubwa ikiwa mgogoro wa Libya, ambapo pia wawakilishi wa waasi wamealikwa kuhudhuria.

https://p.dw.com/p/11mHa
Muammar Gadhafi mbele ya bendera za mataifa ya Afrika.
Muammar Gadhafi mbele ya bendera za mataifa ya Afrika.Picha: AP

Mkutano huo unaanza kukiwa tayari na mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wake. Baadhi ya viongozi wakuu wa nchi za Afrika wamekuwa wakimuunga mkono wazi wazi Muammar Gaddafi wa Libya kwa sababu amekuwa mfadhili mkubwa barani humo.

Ufadhili wa Gaddafi kwa mataifa ya Afrika umo kwenye masuala mbalimbali yakiwemo ya kisiasa kama vile utatuzi wa migogoro na ya kiuchumi kama vile miradi ya kimaendeleo. Gaddafi pia aliwahi kushika wadhifa wa uenyekiti wa Umoja huo miaka miwili tu iliyopita.

Hata hivyo, wapo baadhi ya viongozi wa Afrika wanaosema muda umefika kwa Gaddafu kuondoka madarakani. Mmoja ya wajumbe anayehudhuria mkutano huo, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema hakuna anayetaka kusema wazi, kwa sababu Gaddafi amewasaidia sana kifedha.

Libya yenyewe katika mkutano huo imewakilishwa na pande zote mbili zinazozozana: serikalini na waasi.

Saif al-Islam, mtoto wa Gaddafi, ambaye naye anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Saif al-Islam, mtoto wa Gaddafi, ambaye naye anatakiwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.Picha: AP

Waziri wa Libya anayeshughulikia Masuala ya Umoja wa Afrika, Jumaa Ibrahim Ameir, aliwaambia waandishi wa habari kabla ya kuanza kwa mkutano huo kwamba serikali ya Gaddafi inatarajia kuungwa mkono na Umoja wa Afrika.

Amesema msimamo wa Umoja wa Afrika uko wazi kabisa, ambapo mpango wake wa kupatikana kwa ufumbuzi wa mzozo huo kwa amani unaungwa mkono na Libya.

Amesisitizia kuwa mpango huo ni hatua muhimu katika kupatikana ufumbuzi wa amani, lakini mashambulio yanayofanywa na jeshi la Jumuia ya Kujihami ya NATO, ambayo yanalenga maeneo ya raia kama vile shule na hospitali, lazima kwanza yasitishwe.

Aidha Ameir amesema nchi yake haitambui waranti uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) wiki iliyopita, unaoidhinisha kukamatwa kwa Gaddafi, mtoto wake Saif al-Islam na Mkuu wa Usalama wa Taifa, Abdullah al-Sannoussi, kwa makosa dhidi ya uhalifu wa binadamu.

Ameishutumu Mahakama hiyo kwa kutumiwa kama chombo cha kisiasa na mataifa makubwa, hususan dhidi ya nchi za Kiafrika, akitolea mfano waranti mwingine uliotolewa na Mahakama hiyo dhidi ya Rais wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir.

Akizungumzia hatua hiyo ya ICC, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, amesema inasababisha hali kuwa ngumu zaidi.

Jubel Internationale Strafgerichtshof Gaddafi Libyen
Waasi wa Libya wakifurahia kuteka silaha za GaddafiPicha: dapd

Kwa upande wao waasi, ambao pia wametuma ujumbe wao katika mkutano huo wa Malabo, wameshasema wazi kwamba wataunga mkono tu mpango wa Umoja wa Afrika utakaowezesha Gaddafi kuondoka madarakani.

Mkutano huo umeanza hii leo baada ya jopo la viongozi lililo na jukumu la kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo wa Libya, kukutana jana usiku, huku pendekezo lao la ufumbuzi wa kisiasa katika mzozo huo wa Libya lililojikita katika mpango wao ulioandaliwa mwezi Machi, likitarajiwa kuwasilishwa, ili kuweza kuungwa mkono.

Jopo hilo linalowajumuisha marais watano, akiwemo Jacob Zuma wa Afrika ya Kusini na Mohamed Ould Abdel Aziz wa Mauritania jana pia lilijadili hali inavyoendelea nchini Libya tangu, walipokutana mara ya mwisho, wiki iliyopita.

Kamishna wa Baraza la Amani na Usalama katika umoja wa Afrika Ramtane Lamamra amesema jopo hilo ambalo pia linawahusisha rais Yoweri Musseveni wa Uganda, Denis Sassou Nguesso, wa Jamhuri ya Congo pamoja na rais wa Mali Amadou Toumani Toure, limezingatia uchaguzi kuchagua "ufumbuzi wa amani".

Kauli mbiu ya mkutano huo wa Umoja wa Afrika ni "Vijana na Maendeleo".

Mwandishi: Halima Nyanza /AFP
Mhariri: Abdu Mtullya