Urusi yaanza operesheni za anga Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 30.09.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Urusi yaanza operesheni za anga Syria

Ndege za kijeshi za Urusi zimeanza mashambulizi ndani ya Syria, katika kile ambacho rais wa Urusi Vladimir Putin amesema ni kulisaidia jeshi la Syria katika operesheni zake. Nchi za Magharibi zimeikosoa hatua hiyo.

Mojawapo ya ndege za Urusi zinazofanya mashambulizi nchini Syria

Mojawapo ya ndege za Urusi zinazofanya mashambulizi nchini Syria

Kulingana na duru za kijeshi za Marekani, Urusi imefanya mashambulizi ya kwanza ya anga nchini Syria karibu na mji wa Homs, na kuashiria kujiingiza kijeshi kwa nchi hiyo katika mzozo wa Syria ambao umedumu kwa zaidi ya miaka minne.

Afisa wa Marekani ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema mwanajeshi wa Urusi mwenye cheo cha jenerali ambaye anafanya kazi katika kitengo cha ujasusi nchini Iraq, ameutembelea ubalozi wa Marekani mjini Baghdad na kutoa taarifa ya mdomo kuhusu operesheni hiyo. Afisa huyo amesema taarifa hiyo imetolewa saa moja kabla ya mashambulizi ya Urusi kuanza.

Mapema leo rais Vladimir Putin wa Urusi amepata ridhaa ya baraza la seneti kulitumia jeshi la nchi hiyo katika operesheni nchini Syria. Rais huyo amenukuliwa na mashirika ya habari ya Urusi leo hii, akisema nchi yake haitajiingiza moja kwa moja katika mzozo wa Syria. Hata hivyo, kulingana na mashirika hayo, Putin amesema Urusi italisaidia jeshi la rais Bashar al-Assad muda wote litakapokuwa likiendelea na operesheni zake.

Aidha, rais Putin amenukuliwa akisema anatumai kwamba rais wa Syria Bashar al-Assad atakuwa tayari kuketi meza moja na upinzani, kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mgogoro wa nchi yao.

Utata kuhusu shabaha ya Urusi

Rais wa Urusi, Vladimir Putin

Rais wa Urusi, Vladimir Putin

Jioni hii maafisa wa Marekani wamesema inavyoelekea ndege za Urusi hazililengi kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS katika maeneo ya Homs, na huenda mashambulizi hayo yakapanuliwa kuhusisha sehemu nyingine.

Mchambuzi mmoja wa masuala ya kijeshi Pavel Felgenhauer, amesema kwa wakati huu kundi la IS sio kitisho kikubwa kwa utawala wa rais Assad, na kuongeza kuwa hiyo ina maana kwamba Urusi inaweza kuyalenga makundi mengine ya upinzani.

''Makabiliano kati ya jeshi la serikali na IS yako maeneo ya karibu na Palymira tu, kwingineko, kitisho dhidi ya Assad kinatokana na makundi mengine ya upinzani. Inaweza kuwa vigumu kujua iwapo mashambulizi dhidi ya makundi hayo yamefanywa na Urusi, au jeshi la Syria, na Urusi itakuwa na uwezo wa kujitenga na uharibifu utakaofanyika, ikisema, Oh, sio sisi, au hata kubakia kimya kabisa.'' Amesema Felgenhauer.

Nchi za Magharibi zalalamika

Operesheni hizo za nga za Urusi ndani ya Syria hayakupokelewa vyema na nchi za magharibi. Umoja wa Kujihami wa NATO umesema hatua hiyo haitaleta tija, kwa sababu, umesema umoja huo, rais Assad anayenufaika na operesheni hizo ni sehemu ya tatizo la Syria.

Pia waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry ameripotiwa kuwasilisha malalamiko kwa mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, akisema hatua hiyo inakwenda kinyume na makubaliano baina ya Marekani na Urusi kupunguza mvutano baina yao.

Mwandishi: Daniel Gakuba/ape/afpe/rtre

Mhariri:Josephat Charo

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com