Umoja wa Afrika wazungumzia sakata la Rais Bashir | NRS-Import | DW | 30.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

NRS-Import

Umoja wa Afrika wazungumzia sakata la Rais Bashir

Umoja huo umeelezea kusikitishwa kwake na kauli zilizotolewa na baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Viongozi wa nchi za Afrika wakiwa katika picha ya pamoja mjini Kampala, Uganda.

Viongozi wa nchi za Afrika wakiwa katika picha ya pamoja mjini Kampala, Uganda.

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika umesikitishwa na kauli zilizotolewa na baadhi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na maamuzi ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita-ICC kuliarifu Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Baraza la mataifa wanachama wa mkataba wa Roma kuhusu ziara ya Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir nchini Chad na kuwepo kwake katika sherehe za kuzinduliwa katiba mpya ya Kenya hivi majuzi ambaye anasakwa na mahakama hiyo.

Taarifa na maamuzi ya Baraza kuu zilizungumzia juu ya kilichotajwa kuwa ni wajibu wa mataifa hayo mawili ya kiafrika kushirikiana kikamilifu na mahakama hiyo ya kimataifa ili kutekeleza waranti wa kumkamata kiongozi wa Sudan, Omar Hassan al-Bashir, kuambatana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa nambari 1593 pamoja na kifungu nambari 87 cha katiba ya mahakama hiyo ambayo Chad na Kenya ni wanachama.

Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika imeeleza kusikitishwa kwake na kauli pamoja na maamuzi hayo kwa kuwa yanapuuzia na hayatoi mfano wowote kuhusiana na majukumu ya mataifa hayo mawili. Mkutano mkuu wa 13 wa viongozi na marais wa Umoja wa Afrika ulisema kuwa ombi la umoja huo halijawahi kushughulikiwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba mwanachama yoyote wa umoja huo hatoshirikiana na ICC kumkamata Rais wa Sudan Omar Hassan al-Bashir. Ombi hilo lilirudiwa kuzungumzwa katika mkutano mwingine wa 15 wa viongozi wa Umoja wa Afrika uliofanyika mwezi uliopita wa Julai mjini Kampala, Uganda.

Halmashauri hiyo imesema kuwa Chad na Kenya ambazo zote ni majirani wa Sudan, zinafanya hivyo kwa lengo la kuhakikisha usalama na amani nchini Sudan na kuimarisha amani, haki na mapatano nchini humo masuala ambayo yanaweza kupatikana kupitia serikali iliyopo madarakani kwa sasa ambayo imechaguliwa na wananchi. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa Umoja wa Afrika utaendelea kupigania kinga ya kutoshitakiwa kwa Rais Bashir kama ilivyotakiwa na maamuzi ya mikutano ya viongozi wa umoja huo. Aidha umoja huo umeyataka mataifa yote ya Afrika na marafiki wa Afrika, kukataa azimio lolote lile litakalowasilishwa katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na suala hilo la Rais Bashir.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AU)

Mhariri:Abdul-Rahman,Mohammed

 • Tarehe 30.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OzZs
 • Tarehe 30.08.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OzZs
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com