Ukraine na Mkutano wa serikali ya Ujerumani na Israel Magazetini | Magazetini | DW | 24.02.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Ukraine na Mkutano wa serikali ya Ujerumani na Israel Magazetini

Mada mbili kuu zimehodhi vichwa vya habari vya magazetini.Kilio cha Maidan kilichoung'owa madarakani utawala wa Viktor Yanukovitch nchini Ukraine na mkutano wa baraza la mawaziri la Ujerumani na Israel mjini Jerusalem.

Uwanja wa Uhuru-Maidan mjini Kiev

Uwanja wa Uhuru-Maidan mjini Kiev

Tuanzie na dalili za matumaini zilizoanza kuchomoza Ukraine.Gazeti la "Darmstädter Echo" linasifu ujasiri wa waandamanaji na kuandika:"Moyo wa ujasiri,ukakamavu na utayarifu wa waukraine kuyatolea mhanga maisha yao ili kukomesha utawala wa kiimla wa matajiri fisadi wanaomzunguka Viktor Yanukovich unastahiki sifa na uungaji mkono wa wakaazi wote wa ulaya.Hawastahiki kuwachwa peke yao wakijiinamia kwasababu ya kutojua mustakbali wa nchi yao utakuwa wa aina gani."

Gazeti la "Südwest Presse" linatahadharisha kwa kuandika:"Mwisho wa Viktor Yanukovich umeshabainika.Haimaanishi lakini kwamba Vladimir Putin au Alexander Lukaschenko wamefurahishwa na kung'oka madarakani Yanukovich.Urusi itatumia ngao ya kiuchumi kutetea masilahi yake:Ukraine ambayo Yanukovich ameiacha takriban imefilisika,inategemea biashara ya nje kuelekea Urusi pamoja pia na gesi inayotoka Urusi.Na Ulaya pua isisahau.Hata kama hivi sasa mkataba wa ushirikiano pamoja na Kiev haukabiliwi tena na vizingiti:Bila ya Urusi hakuna kinachowezekana kufanyika nchini Ukraine.Na hilo hata waliomtimua madarakani Yanukovich wanalitambua."

Uhusiano wa Ujerumani na Israel

Israel-Deutschland Symbolfoto

Bendera ya Israel (kushoto) na Ujerumani

Mada ya pili kuu magazetini hii leo inahusu mkutano wa mabaraza ya mawaziri ya Ujerumani na Israel mjini Jerusalem.Kila kitu ni cha kawaida hata hivyo ni cha aina pekee" linaandika gazeti la Kölner Stadtanzeiger linalosisitiza zaidi juu ya masilahi ya kiuchumi.Lile la Bild lakini linaandika:"Mashauriano yanayoanza leo kati ya serikali ya Ujerumani na ile ya Israel yamegeuka kuwa kitu cha kawaida.Hata hivyo ni ya aina pekee.Nchi hizi mbili zinashikamana tangu mauwaji ya halaiki ya wayahudi Holocaust hadi kufikia ushirikiano wa kipee wa kirafiki.Usalama wa Israel unatangulizwa mbele na taifa la Ujerumani,anasema kansela Angela Merkel.Kwa maneno mengine mada zifuatazo zitazingatiwa:Berlin kuanzia sasa itaiwakilisha Israel katika mataifa yote ambayo Jerusalem haina uhusiano wa kibalozi.Hii ni aina pekee ya mshikamano.Uzayuni haukubaliani hata kidogo na aina yoyote ya ususiaji ambao waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani anatishia kuutumia ili kuifanya Jerusalem iregeze kamba.Wakati huo huo wasi wasi uliosababishwa na hotuba ya spika wa bunge la Ulaya katika bunge la Israel-Knesset Martin Schulz umefifia.Mwanasiasa huyo wa Ujerumani na waziri wa Israel aliyekuwa akilalamika wameshaelezana.Ujerumani na Israel,licha ya tofauti za maoni za hapa na pale zinakubaliana:Wanataka amani."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu