Ujerumani yashinda dhidi ya Uturuki | Michezo | DW | 09.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ujerumani yashinda dhidi ya Uturuki

Ujerumani imefanikiwa kukaa kileleni mwa kundi A baada ya kuishinda Uturuki kwa mabao 3-0 katika mchezo wa kuwania nafasi katika fainali za mataifa ya Ulaya Euro 2012.

Miroslav Klose, wa Ujerumani kulia akipachika bao la kwanza kwa timu yake kwa kichwa.

Miroslav Klose, wa Ujerumani kulia akipachika bao la kwanza kwa timu yake kwa kichwa.

Mjerumani mwenye asili ya Uturuki Mesut Özil alipachika bao katika ushindi wa timu yake wa mabao 3-0 dhidi ya Uturuki jana Ijumaa katika mchezo wa kutafuta tikiti ya fainali za kombe la mataifa ya Ulaya mwaka 2012 na kuifanya timu ya kocha Joachim Loew kuwa kileleni mwa kundi A ikiwa imepata ushindi katika michezo mitatu ya kwanza.

Timu ilionyesha tangu mwanzo kwamba walihitaji ushindi na tumestahili kushinda, amesema kocha Loew. Sikutarajia kushinda kwa kiwango kikubwa kama hicho, kwasababu kila wakati huu unakuwa mchezo mgumu. Kwa Waturuki , mchezo kati yetu mara zote unakuwa suala la hadhi.

Ikiwa na point tisa, Ujerumani inashikilia usukani barabara wa kundi hilo wakati Uturuki inayopewa mafunzo na kocha Guus Hiddink iko nafasi ya pili ikiwa na point sita na ikiwa imepata kipigo chake cha kwanza katika kinyang'anyiro hiki.

Nafikiri tumefanya pale tunapoweza kuwazuwia Wajerumani , lakini tulikuwa na matatizo yetu. Tumefanya makosa kadha , hususan katika goli la tatu, alikiri Guus Hiddink. Lakini Wajerumani walicheza vizuri sana , tumekosa nafasi nzuri ya kupata goli kupitia Halil Altintop na unahitaji kutumia nafasi hizo vizuri dhidi ya timu kama Ujerumani.

Timu yangu ni changa , ya vijana wadogo bado, tuna mengi ya kujifunza , amesema kocha Hiddink.

Timu inahitaji kujifunza kuwa haipaswi kubweteka na ikipata nafasi ni lazima kuzitumia. Hiyo ndio ilikuwa tofauti kati ya timu hizo mbili, ameongeza Guus Hiddink.

Mzaliwa wa Ujerumani wazazi wake Waturuki, Mesut Özil , mwenye umri wa miaka 21, alikuwa akizomewa na mashabiki wa Uturuki ambao walikuwa karibu nusu ya mashabiki walioingia katika uwanja wa Olimpiki jana wapatao 74,244, lakini aliwanyamazisha kwa goli la dakika 79 lililoonekana kumaliza ubishi wa waturuki. Ujerumani ilipata bao lake la kuongoza wakati mshambuliaji veterani Miloslav Klose alipopachika bao muda mfupi kabla ya nusu ya kwanza ya mchezo kufika. Na nyota huyo wa Bayern Munich alipachika bao lake la pili katika dakika ya 87.

Cha ajabu ni kwamba, Klose hajafunga bao katika ligi ya Ujerumani msimu huu Bundesliga ambapo iko katika mchezo wake wa saba, lakini tayari ameweka wavuni mabao matano katika michezo mitatu ya kimataifa msimu huu katika michezo ya kutafuta tikiti ya fainali za kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2012.

Goli la pili la Klose mwenye umri wa miaka 32 lilikuja muda mfupi kabla ya firimbi ya mwisho kulia na ni goli lake la 57 katika michezo 104 na timu ya taifa , akivuka rekodi aliyoweka Franz Beckenbauer ya kucheza mara 103 na timu ya taifa ya Ujerumani na kukaribia rekodi aliyoweka Gerd Mueller ya magoli 68 kwa timu ya Ujerumani.

Wakati huo huo vigogo vya soka barani Ulaya vinaanza kujitokeza juu katika kuwania nafasi ya kucheza fainali za euro 2012 katika makundi mbali mbali wakati mabingwa wa dunia na bara la Ulaya Hispania , makamu bingwa wa dunia Uholanzi na Ureno wameshinda michezo yao jana Ijumaa.

Hispania ilisukuma kando Lithuania kwa kuifunga mabao 3-1 na kufikisha points sita kutokana na michezo miwili na kufika kileleni mwa kundi I, wakati Wadachi, Uholanzi walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Moldova na kuchukua usukani wa kundi E kwa goli la Klaas jan Huntelaar.

Ureno iliishinda Denmark kwa mabao 3-1, huku Nani akiufumania mlango wa Denmark mara mbili na Christiano Ronaldo akamalizia bao la tatu. Hata hivyo vigogo wengine katika soka la bara la Ulaya Italia imemudu tu sare ya bila kufungana na Ireland ya kaskazini. Urusi iliitungua Ireland kwa mabao 3-2.

Mwandishi : Sekione Kitojo / RTRE

Mwandishi :

 • Tarehe 09.10.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PZuT
 • Tarehe 09.10.2010
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PZuT