Ujerumani yaingia finali | Michezo | DW | 26.06.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Ujerumani yaingia finali

Ujerumani iliilaza Uturuki jana mabao 3-2 na inaisubiri jumapili hii ama Urusi au Spian kwa finali.

Philipp Lahm (kulia kabisa).

Philipp Lahm (kulia kabisa).

Ujerumani iliugeuza mkuki kifuani mwa Uturuki jana na kuwatia wao kitanzi cha mabao 3-2 dakika ya mwisho ya 90 .Ujerumani ikatoroka na tiketi ya finali ya kombe la Ulaya ijumapili hii ama na Spain au Russia, zinazocheza leo.

Waturuki walizikosha jana nyoyo za mashabiki wa dimba wa kombe la Ulaya 2008 na wameonesha Uturuki ni mojawapo ya timu kali za kabumbu ulimwenguni.

Shangwe na shamra shamra, zilienea Ujerumani nzima jana usiku,lakini hata Uturuki kwenyewe,waturuki hawakuomboleza.Walikua na kila sababu ya kujivunia timu yao iliokosha nyoyo za mashabiki wao na hata za maadui wao wa soka Ujerumani.

Kituo cha Tv cha Ujerumani ZDF kimetangaza idadi ya mashabiki walioangalia mpambano wa jana ilikua rekodi-milioni 30 na hicho ni kima cha 81%.Lakini kama mashabiki duniani kote,wajerumani nao kuna sekunde fulani hawakuweza kuuona mpira na walibidi kusikiliza sauti tu ya mtangazaji uwanjani.hii ilitokana na dharuba kali mjini Vienna,ambako matangazo yote ya TV yakitokea.

Gazeti la dimba la Ujerumani "Kicker" limejitokeza leo na kichwa hiki cha maneno: " Mabao 3-2-tumeingia finali-Philipp Lahm ameiikoa timu dhaifu."

Mkongwe wa dimba wa Ujerumani, Franz Beckenbauer amezungumzia mchezo wa timu ya Ujerumani ambao unamsangaza: mara wanacheza kwa nguvu na mara wanadorora.

Hatahivyo, takriban nchi nzima ya Ujerumani ilimiminika mitaani jana mara tu Philip Lahm kuufumania mlango wa Uturuki dakika ya mwisho ya 90 na kutia bao la ushindi.

Katika zoni ya mashabiki nje ya lango la Brandeburg mjini Berlin,ilikua "asie na mwana aeleke jiwe-shamra shamra zilitia fora.Hali ilikua vivyo hivyo, mjini Hamburg,Munich na Cologne.

Mashabiki wa Uturuki,ingawa shingo upande, walijiunga na wale wa Ujerumani kusherehekea huko Berlin.

Licha ya shangwe na sherehe hizo, kulikuwako pia visa kadhaa vya fujo na ghasia na hasa mashariki mwa Ujerumani:Mikahawa inayouza kababu, ya waturuki ilihujumiwa na wahuni mjini Dresden na polisi 6 walijeruhiwa huko Chemnitz,anakotoka nahodha wa Ujerumani, Michael Ballack.

Kwa jumla, waturuki wanaoishi Ujerumani walisherehekea na kuhuzunika kwa amani.Na sasa wanatazamiwa kuipigia debe Ujerumani jumapili hii itakapoingia uwanjani kwa finali mjini Vienna.