Ujerumani na Uturuki | Magazetini | DW | 24.06.2008
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Ujerumani na Uturuki

Kesho ni nusu-finali ya Kombe la Ulaya baina ya Ujerumani na Uturuki.Nani atatoroka na tiketi ya finali ?

Nahodha Michael Ballack

Nahodha Michael Ballack

Kesho "asie na mwana aeleke jiwe na asie na mguu atie gongo"-mkutano uwanjani Basel,Uswisi:

Mabingwa mara tatu wa ulaya na dunia-Ujerumani, wana miadi na Uturuki,inayoania tiketi yake ya kwanza kabisa ya finali ya kombe la Ulaya.

Magoli ya dakika za mwisho yamekuwa ufunguo wa ushindi wa waturuki hadi sasa katika kombe hili la Ulaya.Kwa upande mwengine,Ujerumani tangu kuzipiga kumbo Austria na Ureno nje ya kombe hili la Ulaya,imeanza kulewa sifa nyingi za ile Ujerumani ya kale ya akina Beckenbauer na Rummenigge na hivyo, yamkini ikateleza kesho katika busati la waturuki.

Ikiwa kesho nahodha Michael Ballack atapewa uhuru wa kucheza kama ule alioupata dhidi ya Ureno,ikiwa chipukizi Lukas Podolski na mwenzake Bastian Schweinsteiger watacheza kwa kasi ile ile na ari ile ile walioonesha dhidi ya Ureno na mshambulizi Miroslav Klose atazusha vishindo vyake katika eneo la adhabu la waturuki, basi Uturuki iliodhofika kwa kuumia na kufungiwa kwa baadhi ya mastadi wake, haitakua na nafasi ya kutamba mbele ya wajerumani.

Timu ya uturuki inayokumbana kesho na ujerumani katika uwanja wa st.Jakob Park,mjini Basel,itakua tofauti kabisa kutoka ile ilioilaza Croatia ijumaa iliopita katika changamoto za mikwaju ya penalty mjini Vienna.

Uturuki bila shaka,itacheza kesho bila wachezaji 6 waliotamba hadi sasa na itategemea sana vipi baadhi yao watapona haraka.

Semih Senturk,stadi wao alietia bao la dakika ya mwisho kusawsazisha mchezo dhidi ya Croatia,anadai kufufuka kwa Uturuki mara kwa mara dakika za mwisho za mchezo,ni salamu nzuri za kuwatisha wajerumani.Uturuki haifii mpaka imetiwa maiti yake kwenye jeneza.

Kipa wa uturuki Volkan Demirel alietimuliwa nje kwa kadi nyekundu na rifu ilipoitimua Jamhuri ya czech mabao 3-2 hapo juni 15, pia hatacheza kesho .Mlinzi Emre Asik na wachezaji wa kiungo wenye kuhujumu Tuncay Sanli na Adra Turan pia wamefungiwa kucheza baada ya kuonywa kwa kadi za manjano.

Tofauti na Uturuki, maandalio ya wajerumani yameongoka na hata stadi wao wa kiungo Torsten Frings ametangazwa sasa fit kurudi uwanjani.Hata kocha Joachim Loew ni ruhusa kutamba nje ya chaki ya uwanja baada ya kufungiwa mpambano 1.Na tofauti na kocha mwenzake wa Uturuki Fatih Terim, Loew ana kundi kubwa la wachezaji kuchagua.Loew mwenyewe anaijua vyema timu ya uturuki,kwani mara 2 amekuwa kocha wa klabu za Uturuki.

Chaguo la Joachim Loew ni kuendelea kucheza na timu iliompatia ushindi mara 2 zilizopita au arudi na listi ya mwanzo.Loew alichukua uamuzi mgumu wa kucheza staili ya 4-5-1 ilioingiza Simon Rolfes na thomas Hitzlsperger kama wachezaji wa kiungo huku nahodha Michael Ballack akipata uhuru wa kutamba usoni.Binafsi Loew anasema, "Daima nikiona staili ya 4-4-2 ni mfumo bora."

Kesho firimbi ikilia tutajua ameamua mfumo gani.kwa kila hali, waturuki hawatakua bonde la kuteremka mlima.