Uholanzi na Uruguay kuwania kuingia fainali ya kombe la dunia leo
6 Julai 2010Leo ni leo atakayesema kesho muongo, ndivyo wasemavyo Waswahili. Leo ni mwanzo wa michezo ya nusu fainali za kwanza katika kinyang'anyiro hiki cha kombe la dunia, huko Afrika kusini. Timu zinazoteremka uwanjani hii leo kuwania tikiti ya kucheza katika fainali ni Uruguay na Uholanzi. Sekione Kitojo anatupasha mengi zaidi kuhusu mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa kandanda duniani.
Wachezaji wa Uholanzi wameonywa kutovimba vichwa na kutokuwa na dharau wakati watakapoteremka uwanjani kupambana na Uruguay katika mchezo wa kwanza hii leo wa nusu fainali, wakati Argentina na Brazil wanaendelea kutafakari kile kilichowakuta na kuondolewa katika kinyang'anyiro cha mwaka huu cha fainali za kombe la dunia.
Wachezaji wawili wa Uholanzi Wesley Sneijder na Arjen Robben wanakutana uso kwa uso na nyota kutoka Uruguay Diego Forlan leo usiku, wakati David Villa wa Hispania na Miroslav Klose wa Ujerumani wataoneshana nani mbabe wa kuufumania nyavu hapo kesho katika nusu fainali nyingine.
Holland haijaweza kuonyesha kandanda lao safi lililozoeleka la pasi maridadi katika fainali hizi huko Afrika kusini, lakini kocha wao Bert van Marwijk amesisitiza kuwa timu yake haionyeshi ishara za majivuno ambayo huwa ni kawaida yao huko nyuma.
Siwezi kubadilisha utamaduni, lakini nimefanya kazi ngumu kuweza kuweka mazingira ya kuwafanya wachezaji watambue kuwa iwapo wanataka kupata mafanikio mashindanoni, ni lazima wautafakari mara zote mchezo ujao, amesema van Marwijk, ambaye kikosi chake kinakabiliana na Uruguay ambayo imepungua uwezo wake.
Nchini Brazil Luiz Felipe Scolari anaripotiwa kuwa anaongoza katika orodha ya makocha wanaotarajiwa kuchukua wadhifa wa kuifundisha timu hiyo baada ya kuondoka kwa Dunga. Orodha hiyo ni pamoja na Mano Menezes, Muricy Ramalho, Ricardo Gomes na kocha wa zamani wa AC Milan Leonardo.
Nchini Argentina taarifa zinasema kuwa rais wa shirikisho la kandanda nchini humo Julio Grondona, amesema kuwa Maradona anaweza kuamua mwenyewe hatima yake, kuendelea ama kuacha kuifundisha timu ya taifa ya Argentina.
Wakati huo huo serikali ya Nigeria imesema jana kuwa hatua ya marufuku ya miaka miwili , iliyowekwa dhidi ya timu ya taifa hilo baada ya kuonyesha mchezo dhaifu katika mashindano ya kombe la dunia nchini Afrika kusini imeondolewa. Rais wa nchi hiyo Goodluck Jonathan alichukua hatua hiyo wiki iliyopita baada ya kuzuka hasira katika taifa hilo la Afrika ya magharibi baada ya Super Eagles kufanikiwa kupata point moja tu kutokana na michezo mitatu katika moja kati ya makundi rahisi katika duru ya kwanza.
Shirikisho la kandanda duniani FIFA , liliitaka Nigeria kuondoa marufuku hiyo hadi Jana Jumatatu la sivyo shirikisho la kandanda la Nigeria litasimamishwa uanachama wake katika shirikisho hilo la dunia, na kuiondoa kabisa nchi hiyo kutoka katika michezo yote ya kimataifa, kikanda na barani Afrika.
Mwandishi : Sekione Kitojo / AFPE
Mhariri:Mwadzaya,Thelma