1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uhariri juu ya sakata la mtandao wa televisheni ya Ujerumani ZDF

28 Novemba 2009

Je uhuru wa vyombo vya habari unatoweka nchini Ujerumani?

https://p.dw.com/p/Kk0I
Nikolaus Brender, Mhariri mkuu wa kituo cha pili cha televisheni Ujerumani ZDFPicha: picture-alliance/ dpa

Kufuatia mjadala uliozusha utata katika mtandao wa televisheni ya taifa ya ZDF hapa nchini Ujerumani, bodi ya kituo hicho cha pili cha televisheni nchini Ujerumani siku ya Ijumaa ilikataa kuurefusha mkataba wa kazi wa mhariri mkuu wa kituo hicho Nikolaus Brender. Hatua hiyo nchini Ujerumani inaangaliwa kama ni shambulio dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari. Katika uhariri wa Deutschwelle, Garcia Ziemsen Ramon anasema Ujerumani ni nchi ambayo uhuru wa kujieleza na wa vyombo vya habari unapewa umuhimu mkubwa. Ujerumani ni nchi ambayo imejifunza kutokana na historia yake ambayo inaonekana kama ni ya kipekee duniani katika mfumo wake ulio wazi kwa vyombo vya habari na hasa ikilinganishwa katika uhusiano wake na washirika wake baada ya vita vya pili vya dunia. Ni chombo kinacholipwa ada ya kila mwezi na kupata ushawishi wa kila upande. Ni kituo cha watu kwa ajili ya watu. Haiwezekani hata mara moja kituo hicho kutumiwa kama chombo cha kuendesha propaganda,kama ilivyokuwa inatokea wakati wa usoshalisti. Hata hivyo hilo ni jambo gumu hasa ikizingatiwa kwamba chombo hicho kinaoongozwa na bodi inayowakilisha makundi mbali mbali ya kijamii wakiwemo pia wanasiasa. Ukweli ni kwamba sote tunaupenda mfumo huo wa wazi. Na sasa kutorefushwa kwa mkataba wa kazi wa mhariri mkuu wa mtandao huo wa televisheni ya pili ya taifa ZDF kutokana na kutoridhika kwa wanasiasa wa chama tawala cha CDU jambo lililosababisha bodi inayosimamia kituo hicho kupiga kura dhidi ya kurefushwa mkataba huo,ni jambo la kusikitisha.Ni kipigo kikubwa katika uhuru wa kituo cha utangazaji cha taifa.Kutengwa kwa mwanahabari huyo ambaye haegemei upande wowote wa kisiasa, kwasababu hakipendelei chama chochote ni hatua ya kuushambulia uhuru wa vyombo vya habari nchini Ujerumani. Na mshtuko huo unazidi makali kwani maswali mengi yameanza kujitokeza. Je kuna uhuru kiasi gani wa kutoa habari,na kuna ushawishi mkubwa kiasi gani wa kisiasa kutokana na kuzipa fedha Redio na Televisheni nchini?

Mwandishi/Garcia-Ziemsen,Ramon ZR/Saumu Mwasimba

Mhariri Mohammed Dahman