Ufaransa yaitisha kongamano dhidi ya Dola la Kiislamu | Matukio ya Kisiasa | DW | 15.09.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Ufaransa yaitisha kongamano dhidi ya Dola la Kiislamu

Rais Francoise Hollande na Fouad Massoum wanaongoza mkutano wa zaidi ya mataifa na mashirika 30 ya Magharibi na Arabuni unaojadili hatua za kukabiliana na wanamgambo wanaojiita Dola la Kiislamu.

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa (kulia) na mwenzake wa Iraq, Fouad Massoum, wakiwa kwenye mkutano wa kimataifa dhidi ya ugaidi.

Rais Francoise Hollande wa Ufaransa (kulia) na mwenzake wa Iraq, Fouad Massoum, wakiwa kwenye mkutano wa kimataifa dhidi ya ugaidi.

Viongozi hao wa Iraq na Ufaransa wametoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka dhidi ya wanamgambo wa Dola la Kiislamu, huku Rais Hollande akionya kwamba hakuna tena muda wa kupoteza

"Vuguvugu hili la kigaidi limesambaa kwenye eneo lote, nchini Iraq na Syria. Kundi hili la kigaidi linapuuza mipaka na lina lengo la kuunda dola. Hiki ni kitisho, ni jambo la kilimwengu. Hivyo lazima pawe na suluhisho la kilimwengu," Hollande aliuambia mkutano huo.

Rais Massoum wa Iraq aliliambia shirika la habari la AP kwamba ni lazima viongozi wanaokutana wapate suluhisho la pamoja dhidi ya magaidi wa Dola la Kiislamu.

"Ikiwa kundi hili litajikita barabara nchini Iraq, litazusha matatizo mengi kwa Iraq, kwa eneo lote la mashariki ya kati na ghuba na kwa dunia nzima. Lazima tusaidiwe na nchi nyengine ili kuwe na kampeni ya kimataifa dhidi ya kundi hili ambalo linataka kujiimarisha Iraq kisha kutokea hapo lisambae dunia nzima."

Ufaransa yatuma ndege za kijeshi

Ndege za jeshi la Uingereza na Ufaransa zikishiriki operesheni dhidi ya Dola la Kiislamu.

Ndege za jeshi la Uingereza na Ufaransa zikishiriki operesheni dhidi ya Dola la Kiislamu.

Masaa machache kabla ya mkutano huo kuanza, Ufaransa ilitangaza kuungana na Uingereza kurusha ndege za kufanyia upelelezi ikiwa ni kusaidiana na mashambulizi ya anga yanayofanywa na Marekani dhidi ya kundi hilo.

Ndege mbili aina ya Rafale zimeruka kutoka uwanja wa kijeshi wa al-Dhafra katika Umoja wa Falme za Kiarabu asubuhi hii.

Kwenye kongamano hili la Paris, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, atapigania kuwekwa sawa kwa mkakati wa kile kinachoitwa "Muungano wa Wenye Nia" ambao unaoongozwa na nchi yake.

Mkutano huu ni kama hitimisho la ziara zake za kiguu na njia kwenye eneo la Mashariki ya Kati na Ghuba, kusaka uungaji mkono wa mataifa ya huko kwenye kampeni hiyo.

Kerry amesema kila kitu kimezungumzwa kwenye ziara yake hiyo, na kwamba baadhi ya nchi zilifika umbali wa kutaka kutuma wanajeshi wa ardhini, ingawa kwa sasa uamuzi kamili haujafikiwa.

Iran yaukosoa mkutano wa Paris

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry.

Hata hivyo, Iran imeukosoa mkutano huo na kuiita kichekesho, kwani haukuishirikisha Syria ambayo nayo - kama ilivyo Iraq - inakabiliana na ugaidi wa Dola la Kiislamu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hussein Amir-Abdullahian, amemuambia mwenyekiti wa kamati ya mambo ya nje ya bunge la Ufaransa aliye ziarani mjini Tehran, Patricia Adam, kwamba hakuna namna yoyote dunia inaweza kulishinda kundi la Dola la Kiislamu bila ya ushiriki wa Syria.

Iran, kama ilivyo Syria, nayo haikualikwa kwenye mkutano huo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/dpa/AFP/AP
Mhariri: Saumu Yusuf

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com