Udondozi wa magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 20.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii wamejishughulisha na mkutano wa Mashariki ya Kati.

Mkutano wa Mashariki ya Kati uliowaleta pamoja rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas, waziri mkuu wa Israel, Ehud Olmert na waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, ulilenga kuzifufua tena juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati.

Mhariri wa gazeti la Leipziger Volkszeitung amesema mkutano wa mjini Jerusalem umeleta tu maneno matupu yasiyokuwa na maana yoyote. Cha muhimu katika mazungumuzo hayo ni kuendelea kuiheshimu mikataba ya amani iliyopo na makubaliano ya kufanya mkutano mwingine hivi karibuni.

Jibu la swali kwa nini mkutano huo unatakiwa kufanyika tena liko wazi na rahisi. Condoleezza Rice, Ehud Olmert na Mahmoud Abbas wanahitaji maono na uwezo mpya wa kisiasa. Kwa jumla ni kanuni mbaya ya kupatikana mafanikio mapya.

Gazeti la Kölnische Rundschau linakosoa. Kwa miaka mingi Marekani imeuweka kando mzozo baina ya Israel na Palestina katika ajenda yake. Hatimaye imejitokeza tena kwa nguvu mpya. Kweli serikali ya Washington inafahamu tofauti na enzi za rais wa zamani Bill Clinton, sio kama mpatanishi mwaminifu bali kama dola kuu inayoilinda Israel.

Si ajabu kwamba hakuna hatua yoyote ya kusonga mbele iliyopatikana katika juhudi za kutafuta amani. Mikutano inafanyika bila kufikia makubaliano. Hakuna matokeo yoyote yanayoonekana katika siku za usoni. Siasa ya kutaka tu kuonyesha juhudi zinafanyika ni hatari hususan ikiwa haileti matokeo yoyote. Ndio maana watu wenye siasa kali wanahimizika kujaribu kuyafikia malengo haya kutumia machafuko.

Maneno ya wazi yamesemwa na mhariri wa gazeti la Kieler Nachrichten. Mhariri amesema mkutano wa mjini Jerusalem umedhihirisha wazi athari zilizosababishwa na mamlaka ya dola kuu duniani katika kipindi cha miaka sita cha serikali ya rais George W Bush. Ni ishara ya kutoweza kwamba Condoleezza Rice tayari amekutaja kuwa ufanisi kuwakutanisha Mahmoud Abbas na Ehud Olmert.

Anayeweza kwenda chini kiasi hicho haamini tena uwezo wake katika eneo la Mashariki ya Kati. Kukosekana kwa sera ya Marekani kuelekea Mashariki ya Kati katika kipindi cha miaka sita iliyopita, hakuwezi kumalizika usiku kucha. Rais Bush amevipa kipaumbele vita dhidi ya ugaidi. Suluhu la mzozo wa Mashariki ya Kati halina umuhimu kwa Marekani kwa wakati huu.

Gazeti la Wiesbadener Kurier limesema Marekani na pande zinazohasimiana katika Mashariki ya Kati, zimezikwamisha tena kanuni za mkwamo uliopo, bila kuonyesha njia ya kuumaliza. Israel pamoja na mlinzi wake Marekani na hata pia Umoja wa Ulaya ambao pia ni miongoni mwa pande nne zinazoudhamini mpango wa amani ya Mashariki ya Kati, zinataka kuwalazimisha Waislamu katika mazungumzo yote waitambue haki ya kuwepo taifa la Israel.

Na gazeti la Tageszeitung kutoka mjini Berlin likitumalizia limekuwa na maoni haya: Ama kweli aina ya uhusiano na Israel utakuwa mtihani mgumu wa kwanza wa serikali mpya ya umoja wa taifa itakayoundwa nchini Palestina. Chama cha Hamas kinaweza kujificha nyuma ya wanachama wengine katika serikali hiyo na kutafuta njia ya kufikia muafaka.

 • Tarehe 20.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTf
 • Tarehe 20.02.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHTf
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com