1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani tarehe 6-Septemba-2004

6 Septemba 2004

Kwa upande wa mambo ya kigeni, wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo hii siku ya Jumatatu wamejihusisha zaidi na uchambuzi wa kisiasa wa pigo kubwa la kigaidi nchini Russia. Kwa upande wa mambo ya ndani, magazeti ya Ujerumani yametoa kipaumbele zaidi kwenye matokeo ya uchaguzi mdogo uliofanyika wikendi iliyopita kwenye mkoa wa Saarland, ambapo chama tawala cha SPD kimeshindwa vibaya.

https://p.dw.com/p/CHPc

Uchaguzi mdogo kwenye mkoa wa Saarland umeonyesha kwamba chama kikuu tawala cha Social Democrats – SPD, kinazidi kuanguka. Matokeo haya yana uhusiano na maandamano ya wananchi kupinga mageuzi ya mfumo wa kazi na mafao kwa watu wasio na ajira. Chama cha kihafidhina cha Christian Democrats – CDU kimejipatia kura nyingi, na vyama vingine vidogo vimejipatia kura za kutosha kuweza kuwakilishwa kwenye bunge la mkoa.
Lakini jambo linaloleta hali ya wasiwasi ni uamuzi wa baadhi ya wananchi kukipigia kura chama cha mrengu wa kulia - NPD.

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limechambua matokeo ya uchaguzi huu kwa kuandika:

"Watu wanakikimbia chama cha SPD wakielekea kila upande: wengine hawapigi kura, wengine wanahamia kwenye chama cha kijani, wengine chama cha FDP. Lakini wengine hawasiti sasa hata kukipigia kura chama cha mrengu wa kulia NPD. Hii ni ishara mbaya kwa chaguzi ndogo zinazofuata kwenye mikoa ya mashariki.

Kwa kuangalia juujuu tu, chama pekee kilichoshindwa kwenye uchaguzi huu ni SPD. Lakini hata vyama vilivyoshinda haviwezi kuwa na furaha hivyo, kwani kila kura inayokwenda kwenye chama cha msimamo mkali kinachochochea chuki, ni pigo kubwa kwa siasa za ndani. Hata kama wananchi wanafanya hivyo kwa kutokana na wasiwasi wa maisha yao au kwa nia ya kuonyesha upinzani wa kisiasa, mwelekeo huu unaleta wasiwasi."

Kuhusu mada hii gazeti la BERLINER ZEITUNG limeandika:

"Kwa mara nyingine tena chama cha SPD kimeanguka vibaya kwenye uchaguzi mdogo. Matokeo haya yalitarajiwa, lakini siyo kwa kiwango kikubwa namna hii. Mgombea wa chama chama cha SPD, HEIKO MAAS ana hali ngumu. Chini ya uongozi wake; mkoa uliokuwa unaongozwa na chama cha SPD umebadilika sasa na kuwa mkoa wa watu wanaokichukia chama hiki.

Hii inatokana na siasa za kitaifa pia, hasa kwa kuchelewa kwa chama cha kanzela Gerhard Schröder, kutambua na kuanza kufanya marekebisho mbalimbali kwenye mageuzi wanayofanya."

Hayo yameandikwa kwenye gazeti la BERLINER ZEITUNG.

Mada nyingine iliyopewa uzito wa hali ya juu kwenye magazeti ya Ujerumani leo hii ni uchambuzi wa kisiasa wa pigo la kigaidi nchini Russia.

Gazeti la NEUEN DEUTSCHLAND limeandika:
"Beslan siyo tu uthibitisho wa ugaidi unaozidi kuvuka mipaka duniani kote, bali ni uthibitisho pia kwamba, siasa za za Putin za kutumia nguvu, zimekwama.

Pamoja na vifo vya mamia ya watu, mashambulio ya kigaidi kama haya ya Beslan yataendelea kutokea, iwapo mahasimu wa pande zote hawataanza kujadiliana. Bila suluhu ya kisiasa kwa eneo hilo, bila ujenzi-upya wa kiuchumi, bila kuleta hali ya matumaini kwa wananchi wa Chechnya, Beslan nyingine nyingi zitafuatia."

Nalo gazeti la HANDELSBLATT kuhusu mada hii limeandika:

"Ni wazi kwamba ni vigumu au haiwezekani kujadiliana na wateka nyara au waislamu wenye kufuata msimamo mkali. Lakini Putin anatakiwa walau kujaribu kutafuta uungwaji mkono na uwingi mkubwa wa wakazi wa Chenchya. Mpaka hivi sasa amenshindwa hata kuwapa uhuru wa kuchagua viongozi wao. Wakazi wengi wamechoshwa na vita, lakini wanapinga kabisa kuingiliwa kisiasa na utawala wa Russia."