1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 12.12.2005

RM12 Desemba 2005

Maoni ya wahariri wa magezeti ya Ujerumani hii leo yametuwama zaidi kwenye mada mbili: · Kansela mstaafu Gerhard Schröder analaumiwa vikali kwa mpango wake wa kufanya kazi ya uongozi wa kampuni la gesi la Ujerumani na Russia. · Na kwa upande mwingine wahariri wameyakosoa maazimio ya mkutano wa kimataifa wa mazingira uliofanyika mjini Montrel Canada.

https://p.dw.com/p/CHXb

Kuhusu Kansela mstaafu Gerhard Schröder, gazeti la GENERAL-ANZEIGER limeandika:

„Gerhard Schröder yuko mbioni kuchukua kazi ya pili tangu alipoachia kazi ya ukansela. Lakini kazi anayotaka kufanya sasa, kazi ya ukurugenzi wa kampuni la Ujerumani na Russia la kujenga mabomba ya gesi, inavuka mpaka. Hususani kama madai kwamba, kampuni hili linapanga kumpa mshahara mkubwa, yatakuwa ya kweli.

Huu kwa kweli siyo mfano mzuri kwa mtu aliyekuwa kiongozi wa nchi.

Gazeti hili linamalizia kwa kuandika:

Hili ni suala la tabia – mtu anaweza kuwa na tabia nzuri au kutokuwa na tabia nzuri.

Nalo gazeti la HAMBURGER ABENDBLATT kuhusu mada hii limeandika:

“Kansela mstaafu anatuhumiwa kwa haki kutaka kujinufaisha yeye binafsi kwenye kampuni ambalo muda mfupi uliopita alilitetea kama mwanasiasa.

Wakosoaji wa Schröder watamkumbusha pia msimamo wake kuhusu siasa za kimabavu za rais wa Russia Vladmir Putin kwenye jimbo la Chechnya.

Bila shaka watataka ufafanuzi kama hii kazi sasa amepewa kama zawadi ya msimamo wake wa kufumbia macho makosa ya Russia.”

Gazeti la ABENDZEITUNG nalo linamtuhumu Schröder, kwa kile linachodai, mpango wa kujitajirisha:

“Kanuni za utawala bora hazimruhusu mwanasiasa kupokea malipo kutoka kwenye kampuni ambalo alikuwa analitetea kisiasa.

Tena kwa Schröder, kampuni hili linamilikiwa na serikali ya Russia ambayo daima alikuwa anakwepa kuikosoa wazi.

Iwapo kansela mstaafu hataona utata huu yeye mwenyewe, basi Ujerumani inahitaji kuwa na kanuni maalumu kwa wanasisa, kanuni zitakazoweka bayana jambo hili.”

Huu ndiyo msimamo pia wa gazeti la WESTDEUTSCHE ZEITUNG.

“Kama viongozi watashindwa kujiheshimu wenyewe, basi Ujerumani lazima ijiwekee masharti ya kufuata.

Kwa mfano, kifungu kitakachomzuia mwanasiasa kufanya kazi fulanifulani kwa muda wa miaka miwili, kama vile ilivyo kwa makampuni ya watu binafsi. Pia kuwe na mpango wa kupunguza mafao ya wanasiasa wanaofanya kazi nyingine.”

Tugeukie sasa mada nyingine: Wawakilishi wa nchi mbalimbali kwenye mkutano wa kimataifa wa mazingira mjini Montreal, wamekubaliana kuiendeleza na itifaki ya Kyoto.

Gazeti la FRANKFURTER RUNDSCHAU limeandika:

„Mkutano huu wa kimataifa ulionfanyikia nchini Kanada umeleta mwamko mpya wa umuhimu wa kulinda mazingira, lakini haukuwa na mafanikio ya kuvunja rekodi. Marekani bado haitashiriki kwenye makubaliano ya Kyoto wakati wa utawala wa Bush. Pia huenda miaka mingi itapita, kabla ya kuziwajibisha nchi zinazoendelea na zile zinazoibukia kiuchumi, ili nazo zishiriki kikamilifu kwenye ulinzi wa mazingira.

Hii ni kwa kuzingatia pia kwa mfano Uchina hivi sasa ni nchi ya pili kwa utoaji wa gesi ya Carbon-dioxide. Hii ni mojawapo ya gesi inayoongeza ujoto angani na hivyo kusababisha mabadiliko ya hali ya hewa yanayoshuhudiwa duniani kote.“

Kuhusu mada hii, gazeti la EßLINGER ZEITUNG limeimulika Marekani na kuandika:

„Itifaki ya Kyoto inayolenga kupunguza utoaji wa gesi zinazoongeza ujoto angani, haiungwi mkono na Marekani. Mkutano wa Montreal haukufanikiwa kuleta mabadiliko kwenye upande huu.

Zaidi ya hapo nchi zinazoendelea kiuchumi kwa kasi kama vile Uchina na India, ingefaa zihusishwe pia kwenye makubaliano ya Kyoto.“

Gazeti la WESTFÄLLISCHE RUNDSCHAU linampongeza Bill Clinton kwa kuandika:

„Aliyekuwa raisi wa Marekani alitoa hotuba ambayo bila shaka iliwangia akilini wawakilishi wa Marekani na hivyo kuepusha kuvurugika kwa mkutano.


Hata waziri mpya wa mazingira wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, anastahili pongezi kwa kuwatuliza wawakilishi wa Russia waliokwenda kwenye mkutano huo na madai mengi.

Gazeti hili linamalizia kwa kuandika:
Mkutano wa Montreal umekuwa wa mafanikio kwa kulinganisha na mvutano wa kisiasa ulioambatana na mkutano huu.