1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Udondozi wa magazeti ya Ujerumani, tarehe 02.03.2006

RM2 Machi 2006

Safu za maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo zimetoa uzito mkubwa zaidi kwenye mada mbili: Kwanza, wametathmini hotuba za wanasiasa wa vyama mbalimbali zilizotolewa hapo jana siku ya Jumatano, siku moja baada sherehe za Carnival. Hotuba hizi kwa kawaida huwa za kukosoana vikali lakini hapo jana, hali ilikuwa tofauti kwa vile vyama vikuu nchini ndiyo vinaunda serikali. Mada nyingine iliyopewa uzito mkubwa ni makubaliano ya waajiri na jumuiya za wafanyakazi wa umma yaliyofikiwa kwenye mkoa wa Hamburg.

https://p.dw.com/p/CHWo

Serikali ya mseto ya vyama vikuu nchini, chama cha Social democrats na vyama vya kihafidhina, CDU na CSU, imetimiza siku 100 madarakani kwenye kipindi cha kumalizika kwa sherehe za Karnival.

Kwa kawaida siku moja baada ya sherehe hizi, sikuu iitwayo kijadi, Politischer Aschermittwoch, huwa ni siku ya viongozi wa vyama mbalimbali kutoa hotuba za kukosoana vikali.

Hii ni siku ya kuhitimisha sikukuu ya Karnival na pia mwanzo wa mfungo wa siku 40 kwa Wakatoliki.

Lakini mwaka huu hali ilikuwa tofauti, kwani serikali kuu inaundwa na vyama vikuu vya kisiasa, kwa hiyo kazi ya kuikosoa serikali ilibaki kwa vyama vidogo tu vya upinzani.

Kuhusu mada hii, gazeti la SÜDDEUTSCHE ZEITUNG limeandika:

„Kwa vile vyama vikuu vya kisiasa ndiyo vinaunda serikali kuu, mara hii Jumatano ya mabishano ya kisiasa imepita kimnyakimnya.

Vyama vidogo vya upinzani, FDP na Chama cha Kijani bado vinatafuta njia ya kujizatiti zaidi, wakati vyama vikuu vya kisiasa vinaendelea kuoneana aibu.“

Gazeti hili linahitimisha maoni yake kwa kuandika: „Matokeo yake, vyama vya kisiasa havijihusishi kikamilifu na tatizo kubwa linaloizonga nchi hii hivi sasa, yaani upungufu wa ajira.“

Gazeti la Bielefeld, NEUE WESTFÄLISCHE, limemzungumzia kiongozi wa chama cha CSU, bwana Edmund Stoiber. Gazeti hili linadai kiongozi huyu amepoteza haiba yake ya zamani.

„Mtu aliyekimbia kuwajibika kwenye serikali kuu na kuamua kurudi kuongoza mkoa wake, hawezi kukikosoa chama cha SPD kama alivyokuwa anafanya hapo zamani.“

Kwa maoni ya gazeti la NEUE WESTFÄLISCHE, Bwana Edmund Stoiber amepunguza pia umuhimu wa chama chake na mkoa wa wake wa Bavaria.

Hata gazeti la SCHWARZWÄLDER BOTEN, limeandika, Jumatano ya mabishano makali ya kisiasa, politischer Aschermitwoch, mwaka huu ilikuwa tofauti. Gazeti hili limeendelea kwa kuandika:

„Kwanza siku hii siyo muhimu kwa mkoa wa Bavaria peke yake, kwa vile imeigwa hata na mikoa mingine. Zaidi ya hapo, siku hii imepoteza umaarufu wake mwaka huu kwa vile vyama vikuu vya kisiasa ndiyo vinaunda serikali kuu. Kwa mantiki hii haviwezi tena kushambuliana wazi bila ya kusita.“

Kwenye mzozo wa ‚muda wa kufanya kazi’ unaondelea kati ya jumuiya za watumishi wa umma na waajiri, makubaliano ya kwanza yamefikiwa kwa wafanyakazi 6000 wa mji wa Hamburg. Makubaliano haya yamechambuliwa kwa undani na magazeti ya Ujerumani hii leo.

Gazeti la DIE WELT limeyakosoa makubaliano hayo, kwa madai kwamba, yana mapungufu mengi.

“Jambo zuri ni makubaliano ya kuongeza muda wa kufanya kazi – yapata masaa 40 kwa wiki kwa baadhi ya wafanyakazi.
Jambo jingine la maana ni makubaliano ya kupunguza muda wa kufanya kazi kwa familia zilizo na watoto.”

Lakini gazeti hili maarufu hapa nchini linasema, makubaliano haya yanaonyesha jumuiya za wafanyakazi huwa haziangalii mbele. Kwa mfano linayakosoa makubaliano ya kuwaruhusu wazee kufanya kazi kwa muda mfupi kwa malipo yaleyale.

Gazeti hili linasema, mpango huu utaongeza gharama kwa watoa ajira.

Hivi ndivyo linavyoona hata gazeti la KÖLNER STADT ANZEIGER.

“Makubaliano ya kuwaepusha wazee kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi, yanaonekana kuwa ya kiutu na kiafya yanaweza kukubalika. Lakini kwa kufanya hivyo, gharama za nafasi za kazi za wazee zitakuwa kubwa kuliko kwa vijana. Ingekuwa bora zaidi kutofautisha muda wa kufanya kazi kufanya kazi, kwa kulingana na uzito wa kazi yenyewe.”