Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 09.11.2006
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Uchambuzi wa magazeti ya Ujerumani

Ni dhahiri kuwa mada kuu iliyoshughulikiwa na magazeti ya Ujerumani hii leo ni matokeo ya uchaguzi wa bunge nchini Marekani ambako chama cha Republikan cha rais George W.Bush kimeshindwa na upande wa upinzani wa Demokrat katika Baraza la wawakilishi.Hata kwenye Seneti,uwingi wa Warepublikan ni jambo la kale.

Gazeti la BERLINER KURIER linasema:

“Kinachochekesha ni kuwa safari ya mwisho,Bush aliingia Ikulu ya Washington kwa sababu ya siasa yake kali kuhusu Irak.Na sasa,vita vya Irak vilivyogubikwa na uwongo,ndio vimemtia matatani. Maovu aliyosambaza yanarejea kwake mwenyewe. Athari za vifo vingi vinavyotokea Irak zaonekana nchini Marekani.Ye yote yule anaetaka kumrithi Bush katika chama cha Republikan,anapaswa kutengana nae kwa haraka ikiwa anataka kuwa na nafasi ya kushinda.Hivi sasa,hiyo ni hatima ya kisiasa ya rais mjeuri,hata ikiwa bado yupo katika Ikulu ya Marekani.”Hayo ni maoni ya Berliner Kurier.

Tukiendelea na matokeo ya uchaguzi wa Bunge nchini Marekani,gazeti la OSTTHÜRINGER ZEITUNG linachambua hivi:

“Kwa muda wa miaka sita Bush ameweza kufanya alivyotaka.Aliungwa mkono na chama chake na mara nyingi aliweza pia kutegemea uwingi wa chama hicho bungeni.Sasa,ndio amepoteza kote.Pigo la kushindwa uchaguzi humaanisha kuwa Warepublikan wengi wataanza kumpa kisogo rais wao.”

Lakini kwa maoni ya gazeti la NORDKURIER kutoka Neubrandenburg,

“Bush hatokuwa Bush ikiwa atakabiliana na fedheha hiyo,bila ya kuonyesha ubabe.Hisia zake za kudhibiti mamlaka zimebakia pale pale,hata ikiwa bungeni atalazimika kuridhiana.Gazeti la Nordkurier likiendelea linasema,ye yote atakaetaraji kuona majeshi yakiondoshwa Irak basi atavunjika moyo.Hata hivyo lakini,serikali ya Bush haiwezi kujiepusha kufanya marekebisho fulani.”

Gazeti la RHEIN-NECKAR ZEITUNG kutoka Heidelberg pia linasema:

“Hata ikiwa kutafanywa mabadiliko katika siasa za Irak,basi mageuzi hayo yatatekelezwa pole pole. Sababu ni kuwa hata Wademokrat waliopata ushindi wa ghafula dhidi ya Bush na chama chake cha Repbulikan,hawana mkakati maalum kuhusu Irak. Wengi wao pia waliunga mkono vita vya Irak.Suala la Irak lilikuwa na umuhimu katika uchaguzi uliofanywa lakini hiyo si sababu pekee ya kujitenga na Bush. Asilia mia 75 ya wapiga kura wameamua kuachana na Bush kwa sababu hawataki tena kubeba mzigo wa kashfa mbali mbali.Rais Bush hivi karibuni,alijikuta amezungukwa na mikasa ya kashfa na ulajirushwa.Marekani hatimae imejikomboa kutoka kihoro cha Septemba 11 mwaka 2001,lamalizia Rhein-Neckar Zeitung.