Uchaguzi wa bunge Angola leo | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.09.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uchaguzi wa bunge Angola leo

Dosari zatokeza mjini Luanda

Kiongozi wa chama tawala MPLA na Rais wa Angola Jose Eduardo dos Santos.

Kiongozi wa chama tawala MPLA na Rais wa Angola Jose Eduardo dos Santos.

Uchaguzi wa bunge unafanyika leo nchini Angola, ikiwa ni baada ya kipindi cha miaka 16 na miaka 6 tangu kumalizika vita kati ya majeshi ya serikali inayoongozwa na chama cha MPLA na yale yaliokua ya waasi wa chama cha UNITA-vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 27. Tayari waangalizi wa umoja wa Ulaya wametoa taarifa wakikosoa walicho kishuhudia hadi sasa.

Uchaguzi huu ulioahirishwa mara kadhaa tangu ule wa kwanza 1992 uliozusha mabishano na kuripuka tena kwa vita kati ya majeshi ya serikali ya MPLA na yale ya UNITA, ulianza mapema leo asubuhi kukizuka matatizo katika baadhi ya vituo vya kupigia kura. Kubwa lilikua ni kuchelewa kuanza zoezi hilo.

Shauku kubwa zaidi imeonekana katika mji mkuu Luanda, lakini hata huko nako hadi saa 10 za asubuhi baadhi ya vituo vilikua havijafunguliwa na mamia ya wapiga kura wakisubiri .

Kiongozi wa ujumbe wa waangalizi kutoka Umoja wa Ulaya Luisa Morgantini alisema walichokiona mjini Luanda ni balaa.Sio tu wapiga kura walikua hawajaanza kupiga kura hadi muda wa masaa matatu tangu wakati pale vituo vilipopaswa kufunguliwa, lakini ilielekea maafisa hawakua hata wamejitayarisha. Bibi Morgantini alisema vifaa vilikua vitayarishwe jana na hali iliojitokeza ni vurugu tupu.

Kiroja cha mambo kilikua katika eneo moja la wakaazi wa tabaka la kipato cha wastani la Maianga , ambako orodha ya wapiga kura haikuonekana na maafisa walikua wakichukua namba zao za kujiandikisha na kuwaruhusu kupiga kura wakihoji watawaorodhesha baadae.

Pamoja na hayo mkuu huyo wa waangalizi wa Umoja wa ulaya alisema kwamba waangalizi wa umoja huo katika maeneo mengine hawakuripoti juu ya matatizo yoyote ya aina hiyo akiongeza kuwa inaelekea tatizo kubwa ni mjini Luanda.

Akizungumza na vyombo vya habari baada ya kupiga kura mjini Luanda Kiongozi wa UNITA Isaias Samakuva alikishutumu chama tawala MPLA kwa kile alichokiita kutoupa haki sawa upinzani si kifedha wala katika matumizi ya vyombo vya habari wakati wa kampeni . Hayo yalikua pia maoni ya mwanasheria wa Shirika la haki za binaadamu Human Rights Watch Reed Brody."Wakaazi wa Angola wanasubiri kupiga kura, lakini uwezo wa MPLAS kifedha ambazo ni fedha za dola unakipa nafasi kubwa chama hicho na kutoa wasi wasi kama kweli utakua uchaguzi huru na wa haki."

Licha ya hayo Kiongozi wa UNITA Bw Samakuva alisema leo ni siku ya matumaini , kwamba mambo yatabadilika kwa sababu waangola wameathirika mno, mmpaka kuishi katika amani."ikitamka kwa Kireno " Esperanca da Gloria."Pia Rais Jose Eduardo dos Santos alikua miongoni mawa waliopiga kura katika mji mkuu na alionyesha alama ya vidole viwili akiashiria ushindi, wakati akitoka kituoni.

Zaidi ya nusu ya waangola milioni 16 wamejiandikisha kupiga kura. Angola ina utajiri mkubwa wa almasi na mafuta , lakini ni sehemu ndogo tu ya mapatano ya fedha zinazotokana na utajiri huo , zinazotumiwa katika kukarabati miundo mbinu , au kuinua maisha ya watu wake. Kumekuweko na shutuma kali za ubadhirifu serikalini na kujitajirisha kwa maafisa wa serikali.

Katika bunge lililopita la viti 220 chama cha MPLA kiliku na 190 na vilivyobakia vikishikiliwa na UNITA. Katika uchaguzi wa leo pia kuna vyama vyengine vidogo vidogo 12. Lakini wadadisi wanaashiria MPLA kitabakia madarakani.


 • Tarehe 05.09.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FC67
 • Tarehe 05.09.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FC67
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com