1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Trump aahirisha hafla ya Florida kufuatia ongezeko COVID-19

24 Julai 2020

Rais Donald Trump wa Marekani amelazimika kuahirisha mkutano wa kumtangaza rasmi kuwa mgombea urais wa chama cha Republican uliokuwa ufanyike Florida, baada ya idadi ya walioambukizwa virusi vya korona kuongezeka.

https://p.dw.com/p/3fsZT
USA Präsident Trump
Picha: Reuters/L. Millis

Akitangaza uamuzi huo, Rais Trump amesema huu si wakati muafaka wa kuwakusanya watu kwenye mkutano mkubwa kama huo, kutokana na hali ilivyo sasa. Tangazo hili la Trump limekuja masaa kadhaa baada ya kuthibitishwa kwamba idadi ya waliokwishaambukizwa virusi vya korona nchini Marekani imepindukia milioni 4.

Nchini Mexico nako idadi ya watu waliosajiliwa kuambukizwa COVID-19 ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita imefikia 8,438, huku wengine 718 wakipoteza maisha. Kwa sasa taifa hilo la Amerika Kusini lina watu 370,712 walioambukizwa na imeshapoteza watu 41,908.

Hata hivyo, serikali inasema idadi kamili inaweza ikawa kubwa zaidi ya hiyo, kwani kiwango cha upimaji ni cha chini ikilinganishwa na Marekani. Uchumi wa Mexico unakisiwa kuwa utashuka kwa zaidi ya asilimia 10 mwaka huu kutokana na athari za korona.

Hapa Ulaya, Waziri Mkuu wa Bulgaria Boyko Borissov amelazimika kuwekwa karantini baada ya mkuu wa ofisi yake ya kisiasa kukutikana na maambukizo ya virusi vya korona hapo jana.

Borissov, mwenye umri wa miaka 61, ambaye vipimo vyake vya awali vilionesha kuwa hajaambukizwa, ataendelea kubakia kwenye karantini hadi matokeo ya vipimo vyengine jioni hii. Bulgaria imesajili wagonjwa wengine wapya 268 leo na kuifanya idadi ya waliokwishaambukizwa hadi sasa kufikia 9,853, wakiwemo 329 waliopoteza maisha.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa amevalia barakoa mnamo Julai 20, 2020 wakati w amkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya.
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwa amevalia barakoa mnamo Julai 20, 2020 wakati w amkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya.Picha: picture-alliance/AA/D. Aydemir

Kwa upande wake, Ujerumani imesajili watu wengine 815 walioambukizwa virusi vya korona ndani ya kipindi cha masaa 24 yaliyopita kwa mujibu wa taasisi yake ya uchunguzi wa maradhi, Robert Koch.

Sasa watu waliokwishaambukizwa virusi hivyo hapa Ujerumani imefikia 204,183. Taasisi hiyo pia imetangaza vifo vya watu wengine 10 kutokana na COVID-19 na kuifanya idadi ya waliokwishapoteza maisha kwa ugonjwa huo kufikia 9,111.

Hayo yakijiri, uchunguzi uliofanywa kufuatia mripuko wa maradhi hayo kwenye machinjio ya wanyama ya Tönnies magharibi mwa Ujerumani, ambayo yaliwakumba wafanyakazi zaidi ya 2,000 wa machinjio hayo, umegunduwa kwamba virusi hivyo vinaweza kusambaa kwa watu walio karibu na mtu aliyeathirika hata kwa umbali wa zaidi ya mita nane.

Matokeo hayo yamo kwenye ripoti ya Kituo cha Utafiti cha Helmholtz cha Hospitali ya Chuo Kikuu cha Hamburg-Eppendorf na Taasisi ya Vipimo vya Virusi vya Leibniz.

Mwanasayansi mkuu wa WHO, Dkt. Soumya Swaminathan
Mwanasayansi mkuu wa WHO, Dkt. Soumya SwaminathanPicha: picture-alliance/Keystone/AFP/F. Coffrini

Wakati huo huo, mwanasayansi mkuu wa WHO, Dkt. Soumya Swaminathan, anasema makisio ni kwamba angalau asimilia 50 mpaka 60 ya watu inahitajika kuwa imepata kinga ili pawe na kile kinachoitwa kinga ya kijamii.

Kinga hiyo aghlabu hupatikana kupitia chango na inatokea pale tu ambapo wengi wa watu hawawezi kuambukizwa maradhi.

Dokta Swaminathan amesema wakati mawimbi ya maambukizo yakiendelea kuyakumba mataifa, watu watajenga kinga za mwili na wao ndio watakaokuwa msingi wa kuwakinga wengine. Hata hivyo, tafiti nyengine zimeonesha kuwa ni hadi zaidi ya asilimia 70 ya watu wawe wameshajijengea kinga ndipo kinga ya kijamii inapokuwa imefikiwa.

Kwenye hatua za awali za janga hili, mataifa kama Uingereza na Sweden yalipendekeza kuchukuwa hatua hii ujenzi wa kinga ya kijamii kama mkakati wa kulikabili, lakini ukawarejea wenyewe.

Chanzo: https://www.dw.com/en/coronavirus-latest-no-herd-immunity-means-infection-risk-still-high-warns-who/a-54301885