1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SYDNEY : APEC kusaini mkataba wa mabadiliko ya hali ya hewa

8 Septemba 2007
https://p.dw.com/p/CBRu

Viongozi wa Asia na Pasifiki wanategemewa kusaini taarifa ya kihistoria juu ya mabadiliko ya hali ya hewa leo hii kwa kujiwekea malengo ya kupunguza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira mwanzoni mwa mkutano wa viongozi wa kila mwaka.

Mkutano huo wa kila mwaka wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa nchi za Asia na Pasifiki ambao unaaza leo hii unawakutanisha viongozi 21 wa nchi zenye nguvu za kiuchumi katika kanda hiyo wakiwemo Rais Georeg W. Bush wa Marekani, Vladimir Putin wa Russia na Hu Jintao wa China kwa mazungumzo juu ya masuala yatakayojumuisha pamoja na mambo mengine biashara,Myanmar na Korea Kaskazini.

Benedict Southworth kutoka shirika lisilo la kiserikali la World Development Movement analinganisha mazungumzo hayo ya APEC na yale ya shirika la biashara duniani WTO yaliokwama ambapo anasema Marekani,Canada na Australia zilizojitowa katika mkataba wa Kyoto hivi sasa zinajaribu kuzifanya nchi zinazoendelea kusaini makubaliano ambayo kwa kweli yatamaanisha kuongeza utowaji wa gesi zenye kuathiri mazingira.

Anasema kile hasa wanachokihitaji ni kwa kila mtu kukubali kwamba Umoja wa Mataifa ni mahala sahihi pa kufanyia mazungumzo na kwamba wanatakiwa kuzifanya Marekani,Canada na Australia kurudi kwenye meza ya mazungumzo.

Mwenyeji wa mkutano huo Waziri Mkuu wa Australia John Howard ameliweka juu suala la mabadiliko ya hewa kwenye agenda kwa kutaka kufikiwa muafaka wa makubaliano ya kuchukuwa nafasi ya Itifaki ya Kyoto baada ya kumalizika muda wake ambayo yataitwa Azimio la Sydney.