Spika wa Bundestag aitaka Israel isirudishe hukumu ya kifo
11 Februari 2026
Pendekezo hilo kwa sasa linajadiliwa na wabunge wa Knesset.
Klöckner ambaye yuko ziarani nchini Israel, katika mazungumzo yake na Spika wa Knesset Amir Ohana mjini Jerusalem amesema hukumu ya kifo hailingani na kulindwa kwa utu na kwamba taifa halistahili kulipiza kisasi.
"Naelewa ziara yangu Israel kama Rais wa Bundestag kwanza kama ishara ya mshikamano na usuhuba na taifa lenu la Israel. Pili ni kama ishara ya vita vy akupinga chuki dhidi ya Wayahudi na tatu ni dhamira ya mustakabali ambao watu katika eneo hili wanaweza kuishi salama na kwa heshima," alisema Klöckner.
Wabunge wa Israel wanajadili mswada wenye utata wa kuanzisha tena hukumu ya kifo kwa magaidi.
Mswada huo unaoungwa mkono na serikali ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu, ulipita hatua ya kwanza mwezi Novemba.
Ili kuwa sheria, mswada huo unastahili kupita hatua nyengine mbili zaidi katika bunge la Israel.