Israel yaweka malengo mawili makuu dhidi ya Hamas
28 Januari 2026
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu amesisitiza kwamba hakutakuwa na shughuli zozote za ujenzi ndani ya Gaza hadi malengo ya nchi hiyo yatakapotimizwa.
Kiongozi huyo ameonya kuwa yeyote anayetarajia kufanyika ujenzi ndani ya Gaza kabla ya hatua ya "kulipokonya silaha kundi la Hamas" ana matumaini yasiyo na msingi.
Ameongeza pia kuanzishwa kwa taifa la Palestina "hakujawahi kutokea na hilo kamwe halitatokea," akijipongeza kwa kile alichokitaja kama juhudi zake binafsi za kuzuia utekelezaji wa suluhisho la mataifa mawili kwa kipindi cha miaka mingi.
Kauli yake ameitoa katika wakati ambapo shinikizo la kimataifa - hasa kutoka mataifa ya Ulaya na mashirika ya kimataifa inaongezeka wakiitaka Israel kuitambua Palestina kama taifa huru.
Israel inasisitiza kuwa itaendelea kufanya kile inachokiita "udhibiti wa usalama kuanzia Mto Jordan hadi bahari", hatua inayojumuisha ukanda mzima wa Gaza pamoja na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.
Mpango wa kusitisha mapigano Gaza uliosimamiwa wa Marekani, na ulioanza kutekelezwa tangu Oktoba 10, uliweka masharti mawili muhimu, kwanza kurejeshwa kwa mateka wote walioko Gaza na Hamas kupokonywa silaha katika awamu inayofuata.
Hata hivyo, pamoja na Hamas kukabidhi mwili wa Ran Gvili—mateka wa mwisho —kundi hilo halijakubali kuweka chini silaha zake, likisisitiza kuwa kupokonywa silaha ni mstari mwekundu. Licha ya msimamo huo, kundi hilo limewahi kuashiria uwezekano wa kukabidhi silaha kwa mamlaka ya Palestina, pendekezo ambalo bado halijapatiwa majibu rasmi.
Ama kuhusu siasa za ndani ya Israel, Netanyahu amesema kwamba sasa sio wakati sahihi wa kufanyika uchaguzi, akitaja hatua hiyo kama "kosa" wakati serikali yake inapambana kupitisha bajeti ya taifa.
"Bila shaka nina wasiwasi. Na nadhani jambo la mwisho tunalohitaji hivi sasa ni uchaguzi. Tutakuwa na uchaguzi baadaye mwaka huu, lakini nadhani ni makosa kufanyika sasa na ninatumai kuwa watu wanaelewa hilo na kuchukua hatua kwa busara."
Bajeti ya serikali itasomwa kwa mara ya kwanza leo Jumatano katika bunge la Knesset, lakini nafasi ya Netanyahu kupata wingi wa kura inategemea pakubwa ushirikiano wa mshirika wa zamani ambaye msimamo wake bado haueleweki.
Sheria ya Israel inaeleza kuwa iwapo bajeti haitapitishwa kufikia Machi 31, basi uchaguzi wa mapema utaitishwa moja kwa moja. Kwa sasa, uchaguzi wa kawaida unatarajiwa kufanyika mnamo Novemba mwaka huu.