Siku 100 za Obama madarakani | Matukio ya Kisiasa | DW | 28.04.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Siku 100 za Obama madarakani

Rais mpya wa Marekani ataka kubadilisha mkondo wa siasa ndani ya nje ya nchi yake

Rais Barack Obama wa Marekani

Rais Barack Obama wa Marekani

Siku 100 tangu aingie madarakani,rais wa Marekani Barack Obama amejitenganisha moja kwa moja na mkondo wa siasa za mtangulizi wake.Na sekta ya kiuchumi ndiyo inayodhihirisha zaidi sura hii mpya ya ikulu ya Marekani.

Akijitokeza msuluhifu zaidi katika uwanja wa kidiplomasia kuliko mtangulizi wake,rais Barack Hussein Obama ametangaza kuondoshwa wanajeshi wa Marekani toka Irak,na kuweka kipa umbele cha harakati za kijeshi nchini Afghanistan.Anabidi lakini akabiliane na kuzidi kusonga mbele wataliban nchini Pakistan pamoja pia na kiu cha kinuklea cha Korea ya kaskazini na Iran.

Akiwa mtetezi mkakamavu wa sera za kiuchumi za chama chake cha Democratic,rais Obama anapigania mpango wa gharama kubwa,utakaolenga sekta za afya,elimu na nishati mbadala-sekta anazozitaja kua ni muhimu kwa mustakbal wa nchi yake.

"Ikiwa hatutapitisha hatua za kishujaa haraka,hali hii mbaya inaweza kuwa mbaya zaidi."

Kwa namna hiyo rais Barack Obama anaiongoza nchi yake katika njia nyengine kabisa ikilinganishwa na miaka minane ya siasa za kihafidhina,akijiwekea shabaha ya kuikwamua Marekani toka mgogoro wa kiuchumi ambao haujawahi kushuhudiwa tangu miongo kadhaa iliyopita.

"Kabla ya yote,nnataka kila mmarekani ajue kwamba,kila hatua tunayoipitisha ,lengo ni kufikia mustakbal wa Marekani ambapo ukuaji wa kiuchumi utakua imara,zitabuniwa nafasi za kazi na mishahara itaongezeka."Alisema hayo rais Obama katika hotuba yake ya hivi karibuni.

Kwa ufupi,mtaalam wa masuala ya kisiasa wa Chuo kikuu cha Emory cha Atlanta,Merle Black anasema Obama anaongoza utawala wa kiliberali ambao haujawahi kushuhudiwa,linapohusika suala la kile anachodhamiria kutoa njiani ,akijiwekea malengo makubwa kupita kiasi.

Kwa vyovyote vile itakavyokua wadadisi wanakubaliana Barack Obama anajivunia umaarufu na kupendwa na wamarekani.Utafiti wa maoni ya umma umeonyesha zaidi ya asili mia 60 ya wamarekani wana imani na rais wao.Picha zake zinaonyeshwa siku nzima katika vituo vya televisheni vya nchi hiyo.

Chochote kinachomhusu kinaonyesha kuwavutia,naiwe familia ya rais Obama ilipopatiwa kimbwa kidogo hivi karibuni,au bustani yao inayoshughulikiwa na mkewe Michelle au hata nguo anazovaa Michelle ambazo wataalam wa urembo wanazicchunguza juu chini chini juu.

"Upole wake unachangia kutuliza mambo nchini katika wakati ambapo Marekani inajikuta katika misuko suko mikubwa ya kiuchumi kuwahi kushuhudiwa tangu miaka ya 30" amesema hayo Howard Fineman katika ripoti yake kwa jarida la Newsweek.

Nje ya Marekani pia umashuhuri wake unafungamanishwa na hatua zake.Katika mkutano wa kilele wa nchi za Amerika,binafsi Barack Obama alifanya maskhara alipolinganisha diplomasia yake na "nadharia ya Obama."

Akipania kujitenganisha na Bush,Barack Obama amesisitiza,"hakuna nchi yoyote inayoweza kutatua tatizo lolote kubwa peke yake."Tamko hilo lilifuatiwa na ishara ya kuinyooshea mkono Cuba pamoja pia na kupeana mkono na rais wa Venezuela-bingwa wa siasa za mrengo wa shoto,Hugo Chavez.

Mwandishi :Hamidou Oummilkheir

Mhariri Abdul Rahman • Tarehe 28.04.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hfww
 • Tarehe 28.04.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Hfww
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com