Shida za kiuchumi zasababisha maandamano Ufaransa,wakati waengereza wajiandaa kufunga mkaja | Magazetini | DW | 21.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Shida za kiuchumi zasababisha maandamano Ufaransa,wakati waengereza wajiandaa kufunga mkaja

Katika wakati ambapo kuna majairani wanaopinga kufanya kazi wakiwa na zaidi ya miaka 62 na wengine wanatapa tapa baada ya serikali kutangaza hatua za kupunguza matumizi,nchini Ujerumani hali inatia moyo

Waandamanaji wametia moto mipira ya magari kupinga uamuzi wa rais Sarkozy

Waandamanaji wametia moto mipira ya magari kupinga uamuzi wa rais Sarkozy

Hatua za kufunga mkaja za serikali ya Uingereza,maandamano nchini Ufaransa na matumaini mema ya kiuchumi yanayochomoza nchini Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa zaidi na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanzie lakini Uingereza ambako serikali mpya ya muungano wa wahafidhina na mrengo wa kati imetangaza hatua kali za kupunguza matumizi.Gazeti la Stuttgarter Zeitung linaandika:

Suala kama ,kwa kutangaza hatua hizo ,serikali ya David Cameron inataka kufuata malengo ya kinadharia na kupiga mkasi kutoka chini mpaka juu,limeshajitokeza hadharani.Mjadala mkali ndio utakaofuatia.Suala jengine linalofuatia hapo ni kama mjadala huo utageuka maandamano.Kwa mazingira ya Uengereza si jambo la kawaida kuona mvutano wa kijamii ukimalizikia majiani.Lakini ikiwa waengereza wataanza kuona madhara ya hatua za kufunga mkaja,basi hapatapita muda na wakaazi wa kisiwani watateremka pia barabarani.

Maandamano na migomo si jambo geni nchini Ufaransa.Safari hii lakini serikali ya rais Nicolas Sarkozy inashikilia uamuzi wake wa kutaka kuzifanyia mageuzi sheria zinazoruhusu watu wastaafu.Gazeti la " Nordbayerischer Kurier" linaandika:

Miongoni mwa wanaoteremka majiani wanakutikana wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo vikuu.Kitisho cha kuzidi makali mvutano kati ya serikali na waandamanaji kimezagaa.Kwa Ufaransa kitovu cha mapinduzi yaliyoppelekea kukombolewa Bastille mnamo mwaka 1789,hilo si jambo geni.Zama hizo watu walikuwa wakifyekwa vichwa na katika zama hizi tulizo nazo,baadhi ya serikali mjini Paris zilibidi kuregeza kamba mbele ya waaandamanaji waliokuwa na ghadhabu.Rais Nicolas Sarkozy anaezidi kuchukiwa na wananchi ,kila atakalofanya atakosolewa.Lakini akistaafu jee?

Katika wakati ambapo Ufaransa watu wanateremka majiani,Uengereza wanahofia madhara ya hatua za kufunga mikaja,matumaini mema ya kiuchumi yamechomoza nchini Ujerumani.Gazeti la "Landeszeitung" linaandika:

Herbstprognose 2010 der Wirtschaftsinstitute

Wawakilishi wa taasisi ya uchunguzi wa kiuchumi nchini Ujerumani wakitangaza makadirio ya ukuaji wa kiuchumi kwa msimu wa mapukutiko wa mwaka huu wa 2010

Ni kiroja kikubwa hiki:Katika wakati ambapo wananchi wa Ufaransa wanapinga mpango wa kufanyiwa mageuzi sheria za kustaafu na nchini Uengereza kuna kitisho cha kutokea mfarakano kutokana na hatua kali za kufunga mkaja,nchini Ujerumani hali imeanza kupambazuko.Serikali kuu ya Ujerumani inakadiria ukuaji wa kiuchumi kupindukia asili mia tatu na hali hiyo itapelekea kubuniwa nafasi laki tatu zaidi za kazi.Haijawahi wakati wowote ule kutolewa makadirio imara kama safari hii.Hata lengo la kutokujwa tena na watu wasiokuwa na ajira si ndoto tena.Ikiwa fedha zaidi zitawekezwa katika sekta ya elimu na utafiti basi Ujerumani itazidi kuimarisha nafasi yake kama dola kuu la kiuchumi barani Ulaya.

Gazeti la "Braunschweiger Zeitung" linaandika:

Ukuaji wa kiuchumi nchini Ujerumani si jambo la sadfa.Ni matokeo miongoni mwa mengineyo ya makubaliano yaliyofikiwa miaka ya nyuma kati ya waajiri na waajiriwa.Uamuzi wa kutowafuikuza kazini waajiriwa na badala yake kuruhusu watu wafanye kazi kwa muda mfupi,umepelekea taa viwandani kupungua nuru tuu badala ya kuzimwa moja kwa moja.Fedha za mpango wa kuinua uchumi zinabidi zirejeshwe.Na hakuna wakati mwengine muwafak kuliko huu tulio nao.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse/dpa

Mpitiaji:Josephat Charo

 • Tarehe 21.10.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pjrx
 • Tarehe 21.10.2010
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pjrx