Seneta Barack Obama apiga hatua kubwa kwenye harakati za kuwania urais. | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Seneta Barack Obama apiga hatua kubwa kwenye harakati za kuwania urais.

Mgombea urais wa chama cha Democratic, Seneta Barack Obama, anaelekea kuutetemesha uwanja wa kisiasa nchini Marekani. Kinyume na ilivyotarajiwa na wengi, Seneta Barack Obama amefanikiwa kuchangisha karibu kiasi sawa cha fedha alizochangisha Bi Hillary Clinton, ambaye anapigiwa upatu huenda akateuliwa kuwania urais kwa chama cha Demokratic.

Seneta Barack Obama akihutubia katika mojawapo wa mikutano ya kampeni.

Seneta Barack Obama akihutubia katika mojawapo wa mikutano ya kampeni.

Kambi ya Seneta Obama imearifu kwamba miezi mitatu ya kwanza ya mwaka huu, seneta huyo wa Illinois alifanikiwa kuchangisha kiasi dola milioni ishirini na tano.

Mgombea huyo wa urais amebakisha kiasi dola milioni moja ili afikie kiwango cha fedha alizochangisha Bi Hillary Clinton.

Tangu hapo wengi wamekuwa wakiutilia shaka uzoefu wa Barack Obama aliye na umri wa miaka arobaini na mitano na ambaye amekuwa kwenye siasa za kitaifa kwa muda wa takriban miaka miwili.

Wadadisi wa masuala ya kisiasa wamekuwa wakimtanguliza Bibi Hillary Clinton mwenye umri wa miaka hamsini na tisa ambaye ameutawala ulingo wa siasa za kitaifa tangu enzi ya urais wa mumewe, Bill Clinton.

Kwa mujibu wa mchambuzi wa maswala ya kisiasa, Tim Russert wa shirika la habari la NBC, taarifa hiyo ya kambi ya Obama ni thibitisho kwamba seneta huyo ni tishio kwa wagombea wote wa nafasi ya kuwania urais kwa chama cha Democratic.

Mwenyekiti wa kitengo cha fedha za kampeni ya Seneta Obama, Bi Penny Pritzker amesema ufanisi huo uliopatikana kwa muda wa wiki chache, ni ishara kwamba Wamarekani wanahitaji mabadiliko ya kisiasa na pia wana imani tangu maeneo ya mashinani kwamba Obama yamkini akasaidia kutanzua matatizo yanayoikumba Marekani.

Taarifa hiyo ya fedha za kampeni ya Obama imetolewa siku mbili baada ya wagombea wengine wa Repubilican na Democratic kutangaza matokeo ya harakati zao za mwanzo za kutafuta michango ya kifedha.

Wagombea wengi wamevunja rekodi zilizopita za uchangishaji wa fedha kipindi sawa na hicho cha kampeni za urais.

Siku ya Jumatatu iliyopita, Bi Hillary Clinton alitangaza kuwa alifanikiwa kuchangisha dola milioni ishirini na sita na pia kuhawilisha dola milioni kumi zilizokuwa zimesalia wakati alipokuwa akiwania kuchaguliwa tena mwezi Novemba mwaka uliopita.

Mgombea mwengine wa Democratic anayeelekea kutoa vitisho vya haja ni Seneta John Edwards wa North Carolina ambaye alikuwa mgombea mwenza wa John Kerry katika uchaguzi uliopita wa urais.

Kambi ya John Edwards imetangaza kwamba imechangisha kiasi dola milioni kumi na nne.

Kwa upande wa Republican, mgombea ambaye hakutegemewa kutoa ngurumo za haja, Gavana wa zamani wa Massachusets, Mitt Romney, anaongoza orodha ya wagombea kwa kuchangisha kiasi dola milioni ishirini na tatu kufikia Jumatatu iliyopita.

 • Tarehe 05.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGq
 • Tarehe 05.04.2007
 • Mwandishi Omar Babu
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHGq

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com