Saudi Arabia ′kununua′ vifaru vya kijeshi kutoka Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.07.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Saudi Arabia 'kununua' vifaru vya kijeshi kutoka Ujerumani

Inasemekana Saudi Arabia inataka kununua vifaru vya kijeshi kutoka Ujerumani, jambo ambalo linapingwa vikali na upinzani nchini Ujerumani kwa maelezo kuwa linakwenda kinyume na muongozo wa biashara ya nje wa Ujerumani.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Serikali ya Ujerumani haijaikana habari hiyo, lakini imenyamaza kimya. Imenyamaza kujibu lile suali kama kweli imekubali kuiuzia Saudi Arabia vifaru vya kijeshi.

Inasemekana Wasaudi wanataka kununua vifaru 200 vya kisasa kabisa aina ya Leopard 2A7. Kutokana na habari ambazo bado hazijahakikishwa, tayari imeshanunuwa 44 kati ya hivyo kutoka kampuni ya Kijerumani ya Krauss-Maffei Wegmann, ambayo inatajwa kuwa itafanya biashara ya mabilioni ya fedha.

Serikali inatoa sababu ya kunyamaa kimya kuhusu jambo hilo kwa vile kunahitaji "mashauriano maalum" hapa Ujerumani kuhusu kusafirisha silaha hadi katika nchi zilioko katika hali ya utata. Inahitaji baraza la usalama la Ujerumani litoe kibali juu ya jambo hilo.

Baraza hilo ni kamati ya baraza la mawaziri ambayo mwenyekiti wake ni Kansela, na ndani yake wamo mawaziri kadhaa. Baraza hilo hukutana kwa siri, na ndio maana umma wa Ujerumani haukuarifiwa juu ya kutolewa kibali kwa biashara ya aina hiyo.

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Guido Westerwelle, amekataa kutoa maelezo yoyote kuhusu kikao cha baraza hilo, akisema kwamba vikao hivyo ni vya siri na "kwa hivyo siwezi kutoa jibu kuhusu tetesi zozote za jambo hilo, na sitotoa."

Kuna sheria kali kuhusu kusafirisha silaha hadi nchi ambazo Ujerumani hazina ushirika nazo. Ruhusa ya kufanya biashara haitolewi ikiwa biashara hiyo inaelekezwa katika eneo ambako haki za binadamu hazilindwi au ambako kumezagaa mivutano. Mwongozo wa lazima ni kwamba silaha zisipelekwe kwenye eneo la mizozo.

Hata hivyo, mara kadhaa kumetolewa maamuzi yasiofuata kawaida hiyo, na ambapo mwaka au miaka miwili baadae mtu anasoma katika ripoti za serekali ya Ujerumani kuhusu usafirishaji nje wa silaha.

Hata kama mkasa huu sio wazi bado, kama biashara hiyo kweli itafanyika, vyama vyote vitatu vya upinzani hapa Ujerumani vimepinga kwa ukali sana. Mkuu wa Chama cha Kijani, Claudia Roth, amesema biashara ya aina hiyo inakwenda kinyume na sheria

"Ni Wasaudi Arabia walioisaidia Bahrain kulikandamiza vuguvugu la kidimokrasia kwa kupeleka vifaru vya kijeshi katika nchi hiyo. Ni Saudi Arabia inayojiingiza katika biashara za ugaidi wa kimataifa na bado inaiunga mkono mifumo ya Wataliban. Kwangu mimi biashara hiyo ya Ujerumani kwa Saudi Arabia ni maafa moja kwa moja ya kuaminika siasa ya kigeni ya Ujerumani." Amesema Claudia Roth.

Mkuu wa Chama cha Kijani cha Ujerumani, Claudia Roth

Mkuu wa Chama cha Kijani cha Ujerumani, Claudia Roth

Pia chama cha Social Democratic kina wasiwasi juu ya uwezekano wa kusafirishwa vifaru vya kijeshi vya Ujerumani hadi Saudi Arabia. Katibu mkuu wa chama hicho, Andrea Nahles, amesema Saudi Arabia iko katikati ya kasiki la baruti, hivyo mtu hafai kupeleka huko vijiti vya kibiriti.

Naye Klaus Ernst, mkuu wa Chama cha Shoto, amesema Saudi Arabia ni kati ya nchi ambazo zinaendea kinyume vibaya sana haki za binadamu katika eneo hilo. Bwana Ernst aliilaumu fikra hiyo ya serikali ya Ujerumani na kusema vifaru vya kijeshi vinavyouwa vibaya kabisa anapewa mkanadamizaji mbaya kabisa.

Westerwelle amesema kwamba Ujerumani inatafuta ushirika na serikali kwenye ulimwengu wa Kiarabu, ambazo zinaweza tu kuyajenga maslahi ya siasa za kigeni ya Ujerumani. "Dola hizo, kwa hakika, pia zina fikra tafauti na sisi kuhusu masuala ya mahakama au jamii ya kiraia." Amesema Westerwelle.

Kama tamko hilo linaashiria kwamba waziri huyo wa mambo ya kigeni anaunga mkono biashara hiyo na Saudi Arabia au la, bado tetesi. Kwa vyovyote, upande wa upinzani utaliwasilisha suala hilo mbele ya bunge, na tena kushikilia upatiwe jibu.

Mwandishi: Nina Werkhäuser/ZR
Tafsiri: Othman Miraji
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com