Sarkozy aongoza kikao cha baraza la usalama juu ya masuala ya Afrika | Matukio ya Kisiasa | DW | 25.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Sarkozy aongoza kikao cha baraza la usalama juu ya masuala ya Afrika

Je, kweli dakika 90 zitatosha kwa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuzungumzia kwa kina masuala ya amani na usalama barani Afrika? Licha ya kwamba muda ni mfupi, Ufaransa ambayo ni mwenyekiti wa baraza hilo mwezi huu inajitahidi kuyapa kipaumbele masuala ya Afrika.

Sarkozy anataka sifa yake barani Afrika iboreke

Sarkozy anataka sifa yake barani Afrika iboreke

Suala kwenye mkutano huu utakapoanza baadaye leo jioni litakuwa kupitisha azimio juu ya kupelekwa jeshi la pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kwenda Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa lengo ya kuwalinda wananchi na athari zinazotokana na mzozo huko Darfur. Azimio hilo limetayarishwa na Ufaransa ambayo imependekeza maafisa wa polisi mia tatu wasimamie kambi za wakimbizi kutoka Darfur wakilindwa na kikosi ya askari 3000 wa Umoja wa Ulaya, hususan Wafaransa chini ya uongozi wa Uingereza. Masuala mengine yatakapozungumziwa na kikao hiki cha tatu cha aina hii juu ya Afrika ni kutumwa kwa haraka jeshi la Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa kwenda Darfur, vilevile hali ya usalama katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Sierra Leone na Liberia.

Wakati juhudi za Ufaransa zinasifiwa na mashirika mengi yasiyo ya kawaida, baadhi yao pia wana wasiwasi kuwa rais Sarkozy wa Ufaransa ana malengo mengine. Hata kabla ya kuingia madarakani alijipatia sifa mbaya kutokana na kuweka sheria kali za uhamiaji. Halafu kwenye ziara yake nchini Senegal alitoa hotuba ambapo alizungumzia bara la Afrika kuwa barna lilo nyuma sana.

Mtaalamu wa mambo ya kisiasa kutoka Senegal, Bw. Babacar Justin Ndiaye, anaona pia kuna nia nyingine katika sera za rais Sarkozy: “Kujenga upya sera za Ufaransa kuelekea Afrika kwa haraka akilenga kuhakikisha maslahi ya Ufaransa hata nje ya nchi ambazo tangu zamani zilishirikiana na Ufaransa. Hiyo ndiyo sababu Sarkozy alitayarisha mkutano wa kilele kuhusu suala la Darfur. Pia anataka kuwakaribia tena Waafrika ambao walikasirika baada ya ziara na hotuba zake za hivi karibuni. Na pia lengo lake ni kuhakikisha kuwa Ufaransa bado itakuwa na usemi barani Afrika.”

Hasa lakini rais Sarkozy anazingatia sera za ndani – hata ikiwa katika masuala ya Afrika. Mfano anataka nchi zinazozunguka bahari ya Kati zishirikiane katika kupiga vita ugaidi. Ndiyo sababu Patrice Bouveret ambaye anafanya kazi kwenye taasis ya amani na mizozo mjini Lyon haamini kuwa sera za Ufaransa kuelekea Afrika zitabadilika, kwani ili kuleta amani inabidi kuchukua hatua nyingine, yaani: “Kupunguza idadi ya majeshi ya Kifaransa yaliyoko barani Afrika na kuongeza misaada katika elimu na ya maendeleo. Nataka kusema kuwa inabidi kuwa na sera bora za maendeleo. Kwa sababu, ikiwa unataka kuleta amani ni kupitia msaada kwa nchi husika kujiendeleza.”

Alipoingia madarakani, Rais Sarkozy alisema anataka kumaliza sera za kisirisiri na misaada kwa marafiki kati ya nchi za Kiafrika na Ufaransa. Wakosoaji wake lakini wanasema kwa kutuma jeshi huko Tschad na Afrika ya Kati Sarkozy anaimarisha serikali za nchi hizo mbili ambazo zamani zilikuwa chini ya utawala wa Ufaransa na ambazo serikali zao zimeingia katika matatizo ya ndani.

 • Tarehe 25.09.2007
 • Mwandishi Ute Schaeffer / Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7k
 • Tarehe 25.09.2007
 • Mwandishi Ute Schaeffer / Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CH7k
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com