Rwanda yalalamika kukamatwa kwa afisa wake Ujerumani | Matukio ya Kisiasa | DW | 10.11.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Rwanda yalalamika kukamatwa kwa afisa wake Ujerumani

Amekamatwa kwa shutuma za kuiangusha ndege ya Habyarimana

Mabufuu ya wahanga wa mauaji ya halaiki ya 1994 nchini Rwanda

Mabufuu ya wahanga wa mauaji ya halaiki ya 1994 nchini Rwanda

Serikali ya Rwanda imelalamikia hatua ya kukamatwa kwa afisa wake wa serikali hapa Ujerumani.Afisa huyo Rose Kabuye ni mkuu wa itifaki na mshauri mkuu wa rais wa Rwanda Paul Kagame.Alikamatwa kwa kushukiwa kuhusika na kuidengua ndege iliokuwa imembeba raia wa Rwanda mwaka wa 1994.Kigali inadai kuwa afisa wake hana hatia.

Rose Kabuye,ni miongoni mwa watu tisa wanaotakiwa nchini Ufaransa kwa kuhusika na kifo cha rais wa zamani wa nchi yake ambacho kilisababisha mauaji ya halaiki ya mwaka 1994 yaliyodumu takriban siku 100.

Amekamatwa jana katika uwanja wa Frankfurt na polisi ya Ujerumani ikifuata hati iliotolewa Ufaransa.

Kukamatwa kwake kunafuatia, hatua ya mwaka wa 2006, ambapo jaji mmoja wa Kifaransa alipotoa hati ya kukamatwa kwa maafisa tisa ambao ni wa karibu sana na rais Paul Kagame,akiwemo Rose Kabuye.Maafisa hao inadaiwa kuwa walihusika na kuidengua ndege iliomuua rais wa Rwanda, wa wakati huo, Juvenile Habyarimana. Rose Kabuye alishiriki katika vita vilivyopelekea kuuondoa utawala wa Habyarimana na ana cheo cha Luteni Kanali.

Wakati hati hiyo ilipotolewa serikali ya Kigali ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Ufaransa.

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Rwanda, Rosemary Museminali, amewambia maripota kuwa, wametoa malalamiko yao kwa serikali ya Ujerumani kupitia ubalozi wake wa Kigali,akisisitiza kuwa Kabuye alikuwa na hati ya kusafiria ya kidiplomasia,na alikuwa ametumwa kwa shughuli rasmi za serikali na hivyo asingekamatwa na serikali ya Ujerumani.

Nayo wizara ya habari wa Rwanda,katika taarifa, imekuita kukamatwa huko-kama mchezo wa kisiasa uliopangwa kuficha ukweli na kuidhalilisha serikali.

Aidha taarifa imesema kuwa Kabuye alikuwa ameonywa, kabla ya kufunga safari kuja Ujerumani kuwa angeweza kukamatwa kutokana na hati hiyo.Hata hivyo yeye aliendelea na safari yake kwani hapo kabla alikuwa amefanya safari kadhaa hapa Ujerumani pamoja na mataifa mengine ya Ulaya bila ya shida yoyote.

Taarifa imeendelea kuwa Kabuye hana hatia na ndio maana alieendelea na safari yake hiyo licha ya onyo na ndio sababu amekubali kupelekwa Ufaransa kukabiliana na mashtaka.

Mwezi aprili mwaka huu, rais Kagame alifanya ziara ya siku nne hapa Ujerumani,na kwa mujibu wa vyombo vya habari Kabuye alikuwa katika ujumbe wake.Sheria za Ujerumani hazikubali kumkamata afisa yeyote ambae ameandamana na rais wakati wa ziara yake.

Tena katika sheria za Ufaransa hati ya kukamatwa rais haiwezi ikatolewa kumuhusu Kagame kwa sababu baado yuko ofisini.

Ndege ya Habyarimana ilishambuliwa na kombora. Na kifo chake kikaanzisha mauaji ya watutsi takriban laki nane.Wakati huo Kagame alikuwa kiongozi wa kundi la Rwanda Patriotic Front ambalo liliwalemea wanamgambo wa Kihutu ambao walikuwa wanaiunga mkono serikali ya Habyarimana na hivyo kukomesha mauaji ya halaiki.

Rwanda ni koloni la zamani la Ubeligiji hadi kujipatia uhuru wake mwaka wa 1962. Ufaransa imekuwa na uhusiano wa karibu na Rwanda tangu mwaka wa 1975 hadi 1994 ikiwa inaipa msaada wa fedha na wa kijeshi.

 • Tarehe 10.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FqfZ
 • Tarehe 10.11.2008
 • Mwandishi Kalyango Siraj
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/FqfZ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com