Ripoti ya jaji Goldstone yapokelewa kwa namna tofauti Israel na Gaza | Matukio ya Kisiasa | DW | 16.09.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Ripoti ya jaji Goldstone yapokelewa kwa namna tofauti Israel na Gaza

Israel yapanga kuizuwia ripoti hiyo isifike katika baraza la Usalama

default

Jaji Richard Goldstone

Tume ya uchunguzi ya Umoja wa mataifa inayoongozwa na jaji wa kutoka Afrika Kusini Richard Goldstone imechapisha ripoti ya kurasa 600 inayoilaumu Israel na Hamas kufanya uhalifu wa vita na uhalifu dhidi ya ubinaadam, jeshi la Israel lilipoihujumu Gaza kati ya mwezi Desemba mwaka jana na Januari mwaka huu. Israel inaipinga ripoti hiyo na kusema ni ya mapendeleo.

Jaji Richard Goldstone ambae binafsi ni yahudi anasema

"Mwishoni mwa uchunguzi wetu na kutokana na ushahidi tulioupata, tumegundua visa vingi vinavyokwenda kinyume moja kwa moja na sheria za kimataifa, tangu sheria za ubinaadam mpaka sheria za haki za binaadam, vimefanywa na Israel katika operesheni ya kijeshi huko Gaza. Tume imegundua uhalifu wa vita umefanyika na hata katika baadhi ya kesi pengine visa vya uhalifu dhidi ya ubinaadam vimefanywa na vikosi vya ulinzi vya Israel."

Israel haijakawia kujibu lawama hizo. Serikali ya Israel imesema katika taarifa yake haijashirikiana na tume ya Goldstone.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje amesema Israel inapanga kuanzisha juhudi kubwa za kidiplomasia kujikinga na madhara ya ripoti hiyo ya "kuchukiza na ya upotovu."

"Tutaendesha juhudi za kila aina za kidiplomasia na kisiasa kuzuwia na kukinga madhara ya kuchukiza na ya upotovu ya ripoti ya tume ya Goldstone", amesema hayo Ygal Palmor mbele ya maripota wa shirika la habari la Ufaransa, AFP.

BdT Israel zieht sich aus Gaza zurück

Wanajeshi wa Israel wanarejea nyuma baada ya vita vya Gaza

Wizara ya mambo ya nchi za nje ya Israel imeikosoa ripoti hiyo na kusema ni ya mapendeleo.

Kwa upande wake kiongozi wa Hamas katika Gaza, Ismael Hanniyeh ameisifu ripoti hiyo na kusema imetoa muelekeo bayana dhidi ya Israel kwa kufanya visa vya uhalifu wa vita dhidi ya raia wa kawaida.

Ismael Hanniyeh amesema tunanukuu. "Israel imetumia nusu ya silaha zake na kuwauwa umati wa watu katika siku 22 za vita. "Mwisho wa kumnukuu.

Hujuma za Israel ziligharimu maisha ya zaidi ya wapalastina 1400 - wengi wao wanasemekana walikuwa raia wa kawaida.

Mkuu wa tume hiyo ya uchunguzi ya Gaza, jaji wa Afrika Kusini Richard Goldstone amelitaka baraza la usalama la Umoja wa mataifa liilazimishe Israel ichunguze kisa cha kuhusika wanajeshi wake katika visa vya uhalifu.

Mwanasheria huyo wa kutoka Afrika Kusini anapendelea uchunguzi huo uwe huru na uambatane na sheria za kimataifa na paundwe kamisheni ya wataalam wa haki za binaadam kusimamia uchunguzi huo.

Pindi Israel ikipinga, jaji Richard Goldstone anataka wanachama wote 15 wa baraza la usalama wawasilishe kadhia ya Gaza mbele ya mahakama ya kimataifa mjini the Hague.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir

Mhariri:Othman Miraji

 • Tarehe 16.09.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JhnO
 • Tarehe 16.09.2009
 • Mwandishi Oumilkher Hamidou
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/JhnO

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com