REDET na Mchakato wa Shirikisho la Kisiasa EAC. | Masuala ya Jamii | DW | 10.09.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

REDET na Mchakato wa Shirikisho la Kisiasa EAC.

Wanasiasa na wasomi wangali wakidai Shirikisho muhimu.

Mojawapo ya Sehemu nzuri nchini Tanzania

Mojawapo ya Sehemu nzuri nchini Tanzania

Licha wananchi wengi katika nchi za Tanzania Kenya na Uganda kushauri isiwepo haraka katika kuanzishwa Shirikisho la Kisiasa katika EAC, viongozi wangali wakisisitiza kuwa shirikisho hilo ni muhimu sana kwa mstakabali wa eneo hili.

Lakini kinachotia moyo ni kuwa angalau wanasiasa wameng’amua umuhimu wa kutatua kero zilizo katika nchi wanachama kwanza ambazo inadhaniwa ndizo ziliwasukuma wananchi hao kutotaka haraka haraka hiyo.

Ndio maana katika mkutano uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita katika mji wa Kitalii wa Bagamoyo nchini Tanzania, naibu Waziri Mkuu wa Kwanza wa Uganda, Eliya Kategaya ambaye pia ni waziri wa Uganda anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki alitamka bila kumung’unya maneno, kuwa matatizo kama lile la Zanzibar lazima yatatuliwe kablya ya kufikia mchakato wa kuanzisha shirikisho hilo.

Bwana Kategaya alikuwa akifungua mkutano ambao umeandaliwa na Kitengo cha Chuo kikuu cha Dar es salaam kinachoshughulikia masuala ya kisiasa REDET ambao una azma ya kupitia na kuangalia namna bora ya kufikia shirikisho la kisiasa katika nchi tano wanachama wa Jumuia hii.

Bila shaka ni kero kama hii na nyingine zilizowasukuma marais sita waliokutana mwezi wa Agosti mwaka huu kuamua kwa pamoja kusogeza mbele uanzishwaji wa shirikisho la kisiasa.

Katika mkutano wao huo uliofanyikia katika Hoteli ya kitalii ya Ngurdoto iliyoko nje kidogo ya mji wa Arusha, marais hao walisisitiza kuwa kabla ya kufikia mwaka 2012 kwanza nchi hizo zianze kutumia sarafu moja na kuwa na soko la pamoja.

Lakini pia wakataja sababu nyingine kuwa maoni yaliyotolewa na wananchi wa nchi hizo, na haja ya kuzipatia nchi wanachama wapya katika umoja huo ambazo ni Rwanda na Burundi, nazo ziendeshe mchakato wa kukusanya maoni ya wananchi wake.

Mkutano huo licha ya kuwa kimantiki unaziwakilisha nchi tano ulihudhuriwa na marais sita, Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, Yoweri Museveni wa Uganda, Mwai Kibaki wa Kenya, Paul Kagame wa Rwanda, Makamu wa Rais wa Burundi, Gabriel Ntisezerana aliyemwakilisha rais Pierre Mkurunziza wa Burundi na Rais wa Zanzibar, Amani Karume.

Ukiangalia kwa makini wananchi wa kawaida katika nchi hizi wana maoni tofauti kuhusu kuelekea katika shirikisho hili.

Matokeo ya maoni yaliyokusanywa na Kamati ya Rais ya Kukusanya Maoni kuhusu Kuharakishwa kwa shirikisho iliyoongozwa na Profesa Samuel Wangwe asilimia 75.9 ya Watanzania waliohojiwa walipinga uamuzi wa kuharakishwa kwa uundwaji wa shirikisho hilo.

Lakini ukiangalia kwa mtizamo wa kikanda mambo ni tofauti kabisa. Mfano asilimia 47.1 ya wananchi wa Mkoa wa Kagera waliunga mkono uharakishwaji wa shirikisho hilo.

Sababu ni rahisi kabisa kuwa kwa kiasi kikubwa mkoa huu unapata mahitaji yake mengi na kunufaika kibiashara kutoka nchi jirani kwani ni mkoa ambao unaiunganisha Tanzania na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda na Kenya.

Lakini angalia mkoa kama vile Morogoro na Pemba wastani wa asilimia 87 walipinga uharakishwaji shirikisho hilo na wengi wa Wazanzibari wakataka kwanza kero za muungano zimalizwe kwanza.

Kile kinachodhihirika kwa upande mwingine ni kuwa karibu kila wananchi katika nchi wanachama wana wasiwasi wao wanaodhani wakiungana watapata hasara ya aina fulani ingawa kinachoonekana hapa ni kila mashaka yanayotolewa na upande husika yanaonekana kupuuzwa na upande wa pili kuwa mashaka hayo hayana msingi.

Mfano wakati fulani baadhi ya vyombo vya habari vya Uganda vilikariri kuwa katika utaratibu wa kukusanya maoni wanawake wa Kenya walisikika wakilalamika kuwa likianza shirikisho la kisiasa wanawake wa Uganda watawanyang’anya wanaume zao kwa kigezo kuwa waganda hasa kutoka kabila la wanyankole ni warembo.

Chombo hicho kilikariri kuwa katika mazungumzo ya uharakishwaji wa shirikisho hilo yaliyofanyika ikulu ya Nairobi kipindi fulani alipoambiwa juu ya wasiwasi huo rais wa Kenya Mwai Kibaki alicheka na kisha akajibu kwa mzaha akisema basi kama ni hivyo yafanyike mashindano ya wanawake wazuri katika Afrika Mashariki na watakaoshinda washinde.

Lakini wakati kuna mawazo kama hayo kwa Kenya upande wa Tanzania wananchi wana malalamiko kama hayo kuwa inapotokea nafasi za ajira hasa katika sekta binafsi, wakenya wanapenya kuliko watanzania. Na tena wazo la Kibaki linajirudia hapa kuwa inapotokea ajira na washindane na watakaoshinda washinde.

Mashaka mengine ni ya uwezo wa kiviwanda iliyo nao Kenya, na ule ukweli kuwa Tanzania ina ardhi kubwa ikilinganisha na idadi ya watu wake na ardhi iliyo nayo, mintarafu unapolinganisha jambo kama hilo kwa nchi za Kenya Uganda, Rwanda na Burundi.

Bwana Victor Kimesema afisa mwandamizi kutoka chama cha upinzani nchini Tanzania cha CHADEM alihudhuria mkutano huu wa Bagamoyo na haende mbali na mawazo kama haya.

“kuna maswali mengi ambayo federation ya haraka haraka haijaweza kuyajibu, na mengi ya hayo ni sensitive kwa mfano suala la uraia litakwendaje? pili ardhi ni ya nani? Watu wengi wanahofia hayo, kwa sababu distribution katika nchi hizi zinazoungana hailingani. Mmoja ana ardhi nyingi na watu wachache, nyingine zina watu wengi, na ardhi ndogo, matatizo yanaweza kutokea kutoka hapo.

Pili ukiangalia na issue kama ya sisi na zanzibar mwaka wa 43 tumeungana, bado mambo yako yanachekecha, je sasa ukiongeza na wengine ambao bado wako mbali na sisi, mambo yatakuwaje?

Tatu kuna kitu kinaitwa mobility of labour, hivi sasa tumekwishaona kabisa, kwamba Tanzania karibu senior positions nyingi, katika private sector, zinachukuliwa na wakenya. Ndani ya tanzania”.

Lakini nilipozungumza na Dk. Katumanga Msambae kutoka chuo kikuu cha Nairobi ambaye naye anahudhuria mkutano huu wa Bagamoyo, juu ya wasiwasi wa watanzania yeye anapuuza hasa kwa dhana kuwa haoni kama Kenya ina uchumi mkubwa na maendeleo ya kielimu kiasi cha kuweza kuziogofya nchi wanachama.

“ sidhani, sidhani! Hatua gani wakenya wamepiga?, viwanda vingi vinamilikiwa na akina nani?

Hoja ni kwamba ukienda kwenye misitu kama ile ya Congo, unakuta kama Mbilikimo. Wale ukiwapata watatu, wote wafupi sasa lakini hata kati yao, watakuwa wanachekana, mmoja anasema wewe mfupi, mi mrefu kidogo, lakini ukweli wa mambo ni nini? wote wafupi”.

Yeye anadhani kuna umuhimu mkubwa wa kuwepo shirikisho la kisiasa akitoa mfano wa kabila la Wamasai ambao wanapatikana Kenya na Uganda, kuwa ukiwauliza wamasai walio upande mbili hizo juu ya ikiwa wanataka shirikisho “ hawatajibu kuwa wanalitaka bali watasema wao tayari wamo kwenye shirikisho. Kwa sababu wao hawajui mipaka na hawaoni sababu ya mipaka hiyo”.

Lakini ukiachilia changamoto hizi zinazotokana na matatizo yaliyo ndani ya nchi hizi, kuna matizo ya nje. Mfano Changamoto za Umoja wa Forodha na sarafu moja hasa kutokana na ukweli kuwa hizi nchi wanachama wapo katika SADC na COMESA ambazo nazo zimo katika mchakato wa kuanzisha ushuru wa forodha na masuala mengine.

Mfano nchi wanachama wa SADC zimelenga kuwa ifikapo mwaka 2010, ziwe zimekamilisha mchakato wa kuanzishwa kwa ushuru wa pamoja vivyo hivyo na COMESA ambayo inatarajia kukamilisha hatua hii na mapema.

Sasa kwa mujibu wa taratibu zinazoongoza Umoja wa Forodha wa EAC sio vizuri nchi wanachama kushiriki kwenye jumuiya nyingine kutokana na kile kinachoelezwa kuwa ni kuepuka mgongano wa ki-maslahi. Na sheria za WTO zinalikazia mno macho suala hilo.

Sasa ile ndoto ya wakuu wa EAC ya kutaka kutimiza malengo hayo kabla ya kuanzishwa shirikisho la kisiasa zitatimia namna gani? Hilo bado ni swali linalosubiri majibu.

Lakini wanasiasa na viongozi wa EAC wanayajua yote hayo ila wao wamekazia kile wanachokiita “soko la zaidi ya watu milioni 100. hii ni nguvu kubwa ya uchumi”, kama alivyosema Bwana Eliya Kategaya na kuongeza.

“Muungano sio rahisi. Kuna matatizo kama kawaida. Hata ndoa, hata unapoanzisha ndoa, sio suala la maua tu. Kwa hiyo muhimu ni kuwa tunataka kufanya nini shabaha yetu ni nini.

Kawaida hata kama una nchi moja tu utapata matatizo lakini ni vizuri kama tukifanya”.

Naye Bwana Gideon Kainamula ambaye ni mbunge wa Rwanda anayeiwakilisha Rwana Patriotic Front katika Bunge la nchi hiyo anasema tayari nchi yake inapiga hatua za taratibu lakini za uhakika kuelekea katika jumuia hii.

“ kabla ya kuweka saini kwenye ratification hii, Wanyarwanda wote waliulizwa wakawa sensitized kabisa, kwamba wanaona marupurupu ya kujiunga na wenzao waganda watanzania na wakenya pamoja na warundi”. Anaendelea kufafanua kuwa japo nchi yake haijaanza zoezi la kuchukua maoni ya wananchi wake juu ya shirikisho la kisiasa lakini “ sisi tutaendelea kuzungumza nao kwa sababu tuko wapya, tataendelea kuwaambia kushirikiana …. nimuhimu sana”

Mwisho.

 • Tarehe 10.09.2007
 • Mwandishi Christopher Buke
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHjO
 • Tarehe 10.09.2007
 • Mwandishi Christopher Buke
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHjO

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com