1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ratiba ya kura ya maoni Sudan kusini yatangazwa

6 Oktoba 2010

Onyo latolewa: Matatizo yasiotarajiwa yanaweza kuchelewsha zoezi hilo.

https://p.dw.com/p/PWnN
Ramani ya Sudan (Eneo la rangi ya zambarau ni Sudan Kusini)

Wakaazi wa eneo lenye mafuta la kusini mwa Sudan waliahidiwa watapiga kura kuamua kama wanataka kubakia sehemu ya Sudan au kuwa huru, kutokana na mkataba wa amani ulioasainiwa 2005 kati ya chama cha SPLA na serikali ya Sudan na kumaliza vita vya miongo kadhaa kati ya kusini na kaskazini.

Maandalizi ya kura ya maoni ilinayopangwa kufanyika Januari 9 mwaka ujao tayari yako nyuma mno na maafisa wa kusini wameushutumu upande wa kaskazini kuwa unajaribu kuichelewesha kura ya maoni, ili kuendelea kudhibiti mafuta ya eneo hilo, jambo ambalo serikali mjini Khartoum inalikanusha.

Rais wa Sudan kusini Salva Kiir alisema Ijumaa iliopiata kwamba dalili zote sasa zinaonyesha wakaazi wa sehemu hiyo wanataka kuwa huru, na kuna kitisho cha kurejea tena katika matumizi ya nguvu kwa kiwango kikubwa, kama kura hiyo ya maoni itacheleweshwa au kuvurugwa.

Kwa mujibu wa ratiba iliotolewa, uandikishaji wapiga kura utaanza katikati ya mwezi ujao wa Novemba na orodha kamili ya wapiga kura , kuwa tayari ifikapo Desemba 31 -kukisalia siku nane kabala ya kura yenyewe Januari 9.

Mjumbe wa tume ya inayosimamia zoezi hilo Chan Reek Madut aliliambia Shiriaka la habari la Reuters kwamba kila mmoja anaizingatia tarehe hiyo ya kura ya maoni na kwamba zoezi la uandikishaji wapiga kuara litamalizika Desemba 4, huku kampeni zikiruhusiwa kuanza Desemba 7. Pamoja na hayo mjumbe huyo alisema bado hana hakikika jinsi zoezi la uandikishaji wapiga kura kutoka kusini wanaoishi kaskazini na nje ya Sudan litakavyofanyika., akikiri kwamba wakati ni mdogo na huenda kukazuka kasoro zinazoweza kuchelewesha kazi hiyo.

Kwa upande mwengine Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Hillary Clinton, ameungama kwamba imekuwa ni vigumu kushirikiana na serikali ya Sudan , ikiwa imebakia miezi mitatu kabla ya kura ya maoni ya wakaazi wa kusini mwa nchi hiyo. Clinton aliyasema hayo jana wakati alipokutana na wawakilishi wa kibalozi wa Marekani katika nchi za Kiafrika

Flash-Galerie Mächtige Politikerinnen Hillary Rodham Clinton
Waziri Hillary Clinton

Marekani inaendelea kuushinikiza utawala wa Rais Oamar Hassan al-Bashir wa Sudan utimize wajibu wake.Akihutubia mkutano wa Umoja wa mataifa kuhusu Sudan na kura ya maoni tarehe 24 mwezi uliopita, rais Barack Obama wa Marekani alisitiza kura hiyo lazima ifanyike kama ilivyopangwa.

Utawala wa Obama umetuma maafisa zaidi wa kibalozi nchini Sudan katika kile ambacho waziri Clinton amesema ni " kuweka shinikizo kabambe," kuhakikisha kura ya maoni inafanyika bila matatizo yoyote.

Nchi za magharibi kwa upande mwengine zimeonya kwamba ikiwa kura hiyo ya maoni juu ya mustakbali wa eneo la kusini mwa Sudan haitofanyika kama ilivyopangwa, huenda viongozi wa kusini wakajitangazia uhuru na hali hiyo inaweza kuzusha vita vipya vya wenyewe kwa wenyewe kati ya kusini na kaskazini.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman/Reuters/AFP/AP

Mhariri:Josephat Charo