1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Qatar ina matumaini vita vya Gaza vitasitishwa kabla ya Eid

Saumu Mwasimba
13 Machi 2024

Qatar ambayo inashiriki kwenye mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya kusitisha vita kati ya kundi la Hamas na Israel imesema ina matumaini ya kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita vya Gaza, kabla ya Eid al-Fitri.

https://p.dw.com/p/4dTfU
Gaza Khan Yunis
Wapalestina wakiwa wamekaa kando ya mali zao baada ya kutembelea makaazi yao yaliyoharibiwa na mashambulizi ya IsraelPicha: Mohammed Dahman/AP/picture alliance

Qatar ambayo inashiriki kwenye mazungumzo ya kutafuta makubaliano ya kusitisha vita kati ya kundi la Hamas na Israel imesema ina matumaini ya kufikiwa makubaliano ya kumaliza vita vya Gaza, kabla ya sherehe za kumalizika mwezi wa mfungo wa Ramadhan za Eid al-Fitri.

Sherehe za Eid zinatarajia kufanyika Aprili 10. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Qatar Majed al-Ansari amesema nchi hiyo inataka kuendeleza juhudi za kuzishinikiza pande zote mbili kufikia makubaliano.

Awali wasuluhishi wa mgogoro huo wa Gaza walitarajia makubaliano ya kumaliza vita yangefikiwa kabla ya Ramadhan lakini mazungumzo yamekwama huku mvutano mkubwa kati ya Israel na Hamas ikiwa ni suala la kipindi cha usitishaji mapigano. Juhudi za kusitisha mapigano Ukanda wa Gaza zaendelea

Kundi la Hamas linataka vita visitishwe kabisa na jeshi la Israel liondoke Ukanda wa Gaza wakati Israel ikipinga hatua hiyo.Qatar inajaribu kutafuta maelewano kuhusu mzozo huo pamoja na Marekani na Misri.