Papa anaweza kuwa na jukumu muhimu la kutatua migogoro
22 Septemba 2025
Baada ya mkutano wake wa faragha na Papa Leo, Steinmeier amesema kuna viongozi kadhaa wa dunia walio muhimu sana na walio na ushawishi kwa pande tofauti hasimu. Amesisitiza kuwa dunia haiwezi ikaenda salama bila usaidizi wa Papa pamoja na Vatican.
Papa Leo ambaye alitawazwa kuwa kiongozi wa waumini takriban bilioni 1.4 wa kikatoliki mapema mwaka huu, amekuwa akielezea utayari wake wa kuwapokea wawakilishi kutoka Urusi na Ukraine kwa majadiliano ya kufikiwa amani ya mataifa hayo mawili. Tayari ameshakutana na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.
Steinmeier, ambaye ni muumini wa kiprotestanti amesema amemuhimiza Leo kuendelea na juhudi zake. Rais huyo wa Ujerumani amesema dunia haipaswi kuwa na mashaka kwamba Papa anataka kuingia kikamilifu kuwa mpatanishi lakini akasema kuwa hadi sasa inaonekana kana kwamba Urusi haina nia ya kweli ya kuingia katika majadiliano.
Viongozi hao wawili Papa Leo na Steinmeier walizungumzia pia viwango vinavyopungua vya watu kusali makanisani akisema makanisa yanabakia kuwa sehemu kubwa ya mshikamano wa jamii zetu.
Steinmeier ametangaza kumualika Papa Leo kuitembelea Ujerumani hivi karibuni.Baada ya mkutano wake kiongozi huyo wa ujerumani alitembelea pia mashirika matatu ya Umoja wa Mataifa mjini Roma, shirika la Msaada wa Chakula, WFP, Shirika la Chakula Duniani, FAO na shirika la mfuko wa kimataifa wa kilimo na maendeleo. Katika ziara yake hiyo alikosoa hatua ya mataifa kadhaa kukata ufadhili wao kwa mashirika hayo ya misaada. Akisisitiza kuwa mashirika hayo yanahitaji uungwaji mkono wa hali ya juu.
.