Operesheni za kuweka amani katika Darfur zarefushwa muda wake | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.08.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Operesheni za kuweka amani katika Darfur zarefushwa muda wake

Jeshi la amani la Umoja wa Mataifa litabakia kwa muda zaidi huko Darfur

Wanajeshi wa Umoja wa Afrika wakipiga doria huko Darfur

Wanajeshi wa Umoja wa Afrika wakipiga doria huko Darfur


Yalikua malumbano makali kabla ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana kuweza kukubali kurefusha kuendeshwa operesheni za kuweka amani katika mkoa wa Darfur, nchini Sudan. Umoja wa Afrika, AU, ulijaribu kuuunganisha uamuzi huo na suala la kufanyiwa mashtaka Rais Hassan al-Bashir wa Sudan mbele ya mahakama ya kimataifa ya uhalifu. Kwamba jaribio hilo halijafanikiwa ni ishara nzuri.

Mara hii Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa halijayapigia magoti matakwa ya wale waliomo ndani ya baraza hilo kutaka kuilinda Sudan na rais wake. Suala la kurefushwa operesheni za Umoja wa Mataifa huko Darfur zilitengwa kabisa na lile takwa kwamba Baraza la Usalama lisimamishe uchunguzi unaofanywa na Mahakama ya uhalifu ya Umoja wa Mataifa dhidi ya Rais wa Sudan. Uamuzi huo ni mzuri.

Pia ni ishara nzuri kwa watu walioko katika vijiji vilioko katika mkoa wa Magharibi ya Sudan ulio na mizozo kwamba jamii ya kimataifa haijasita kuchukua hatua; haijazuilika, haitaki ibakie inakodolea macho tu huku maafa makubwa ya kiutu yakifanyika. Hata hivyo, wanajeshi wa kuweka amani wa Umoja wa Afrika na wale wa Umoja wa Mataifa wanaweza kuzuilika kufanya wajibu wao siku za mbele, kwani uwezo waliopewa ni dhaifu na vifao vyao vya kufanyia kazi ni ovyo.

Jeshi la amani la Umoja wa Mataifa na lile la Afrika, kwa jina UNAMID, linaweza kutoa mchango muhimu katika kuituliza hali ya mambo katika mzozo huo wa Darfur. Hivyo ndivyo alivosema siku chache zilizopita aliyekuwa mwakilishi maalum wa Umoja wa Afrika kwa ajili ya mzozo wa Darfur, Salim Ahmed Salim. Mwanadiplomasia huyo amelaumu kwamba sifa ya jamii ya kimataifa inaweza ikaharibika ikiwa wanajeshi hao wa kuweka amani watabakia hawapatiwi vifaa na silaha zifaazo. Mwanzoni mwa mwezi wa July, wanajeshi hao wa kuweka amani walishambuliwa, na hawajaweza kupata msaada wa ulinzi wa angani ili kujilinda dhidi ya silaha kali za waasi. Wanajeshi saba waliuliwa na wengine wengi walijeruhiwa vibaya. Wanajeshi wa kuweka amani huko Darfur hawawezi kujilinda wenyewe, hivyo vipi wataweza kuwalinda wananchi?

Sasa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limerefusha operesheni za jeshi hilo kwa mwaka mwingine, na wanachama wote wa Umoja wa Mataifa wameombwa kulisaidia sana jeshi hilo. Linahitaji fedha, ili kwamba liweze kuwa na mahitaji ya kimsingi ya kijeshi. Wakati huko Iraq zinafanya kazi helikopta 360, katika Darfur kumeahidiwa kupelekwa helikopta 18, lakini hata moja haiajapelekwa kufanya kazi

Jeshi la pamoja la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika Darfur sasa lina muda wa mwaka mmoja. Lakini hata hivi sasa jeshi hilo linaonekana kama mradi wa rahisi, usioweza kutekeleza wajibu wake. Wanamgambo wa rais wanaendelea kuendesha mashambulio yao dhidi ya waasi na raia, watu wanafukuzwa makwao na kuuliwa na pia kuchukuliwa kama mateka na waasi pamoja na wanamgambo. Mkoa wote unatiwa hofu. Mzozo wa Darfur unaendelezwa na pande zinazoshiriki, Rais wa Sudan al-Bashir, Rais wa Chad Deby, na waasi ambao wamenunuliwa katika biashara ya vita hivi vichafu vinavoendeshwa na pande mbili hizo.

Matokeo gani yatapatikana kwa operesheni za kuweka amani ikiwa katika eneo hilo hakuna mwanasiasa mwenye dhamana anayetaka amani? Ni tu mashauriano ya amani na wale wote wanaoshiriki katika mzozo huo- Sudan , Chad pamoja na makundi mbali mbali ya waasi, ndipo vita vitakoma katika Darfur. Hivyo anatakiwa mtu aliye na dhamana.

Kwa hivyo, ni uzuri kwamba Rais wa Sudan amenaswa na Mahakama ya kimataifa ya uhalifu. Ni kwa njia hiyo tu ndipo itakapokuwa wazi kwamba wahalifu dhidi ya uutu, wale waliokuwa na dhamana ya kufukuzwa watu kutoka majumba yao, watu kuteswa, kutendwa vitendo vya mabavu na kuuliwa, kwamba watu hao wanaadhibiwa. Umoja wa Nchi za Kiarabu, Arab League, na Umoja wa Afrika AU, haziukubali wazi wazi msimamo huo, kwani jumuiya hizo zinataka kuizuwia kazi ya Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu kupitia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Hivyo ilikuwa ni busara kwamba jambo hilo limeahirishwa na kutengwa na suala la kurefusha operesheni za jeshi la kuweka amani.

Uchunguzi utakaofanywa na Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu unaweza kuwa ni mbinyo wa kisiasa kwa al-Bashir, mbinyo ambao haujaweza kuwekwa na Umoja wa Mataifa, kwa vile China na Afrika Kusini, zinataka kumlinda rais wa Sudan. Na mwishowe, mbinyo huo wa kisiasa unaweza ukatumika kulifanya jeshi la kimataifa la huko Darfur kuungwa mkono zaidi ili liweze kufanya kazi vizuri zaidi. Lakini hayo sio hakika. Hadi hapo, watu wa Darfur wataendelea kusumbuliwa huku na kule na waasi pamoja na wanamgambo, na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa na wale wa Afrika watabidi waangalie tu.
 • Tarehe 01.08.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EoYe
 • Tarehe 01.08.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EoYe
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com