Operesheni ya kijeshi yaendelea kusini mwa Afghanistan
18 Februari 2010Matangazo
Operesheni ya kijeshi inayofanywa na vikosi vya Marekani na
Afghanistan dhidi ya Wataliban, inaendelea kwa siku ya sita kusini
ya Afghanistan chini ya uongozi wa majeshi ya Marekani. Lakini
maafisa wa kijeshi wanasema kuwa operesheni hiyo ya pamoja
inakwama kwa sababu ya mabomu yaliyotegwa chini ya ardhi na pia
Wataliban kutumia raia kama ngao.
Operesheni hiyo dhidi ya ngome ya Wataliban katika eneo la Marjah
inatazamwa kwa makini kama mtihani mkuu wa kwanza wa mkakati
wa Rais wa Marekani Barack Obama. Lengo ni kumaliza vita vya
miaka minane nchini Afghanistan na kuwatimua wanamgambo wenye
siasa kali na kuirejesha serikali katika eneo hilo.
Mapema juma hili jemadari wa vikosi vya Afghanistan alisema,
takriban eneo zima la Marjah na Nad Ali tayari limedhibitiwa. Lakini
maafisa rkutoka maeneo ya mapigano wanasema wapiganaji wa
Taliban wanajificha nyuma ya raia wa kawaida na wanatega mabomu
barabarani na katika majengo. Kwa mujibu wa Jemadari Mohaidin
Ghori anaeongoza kiasi ya wanajeshi 4,400 wa Afghanistan katika
operesheni hiyo ya pamoja, Wataliban wamewazuia raia kama
mateka. Amesema wanawake na watoto wanatumiwa kama
ngao.Lakini msemaji wa Taliban amekanusha kutumia binadamu
kama ngao.
Operesheni hiyo ikiendelea kati kati ya eneo linalolima bangi katika
Wilaya ya Helmand, maelfu ya watu wamekimbilia mji wa Lashkar
Gah na mikoa mingine ya jirani na eneo la Nimroz ambako Shirika la
Umoja wa Mataifa WFP linaloshughulikia mipango ya chakula
duniani, limegawa chakula kwa mamia ya familia zilizokuwa na njaa.
Kiasi ya watu 80,000 wanaishi katika eneo hilo. Lakini kwa mujibu
wa Amnesty International linalotetea haki za binadamu duniani, kama
raia 10,000 wamelikimbia eneo hilo.Shirika hilo limeonya kuwa
maelfu wengine wamenasa katika maeneo ya mapigano.
Wakati huo huo,hii leo nchi jirani Pakistan imeelezea wasiwasi
kuhusu uwezekano wa wakimbizi wa Kiafghanistan na wanamgambo
kuvuka mpaka kama ilivyotokea mwaka 2001 kufuatia uvamizi wa
Afghanistan na hivyo kusababisha harakati za wanamgambo katika
eneo la mpakani. Waziri Mkuu wa Pakistan Yousuf Raza Gilani
aligusia suala hilo alipokutana na Richard Holbrooke alie mjumbe
maalum wa Marekani katika Afghanistan na Pakistan. Amesema ni
matumaini yake kuwa majeshi ya Marekani na vikosi vya kimataifa
ISAF vitazingatia wasiwasi wa Pakistan kuhusu wakimbizi na
wanamgambo kutoka kusini mwa Afghanistan.
Mwandishi: Martin,P/AFPE/RTRE
Mhariri: Hamidou,Oummilkheir
Matangazo