1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni yapi malengo ya Rais Putin kwa kuandaa uchaguzi?

Bakari Ubena Cathrin Schaer / Kate Hairsine
15 Machi 2024

Ingawa Vladimir Putin ana uhakika wa kushinda uchaguzi wa wa rais wa mwaka 2024, analenga kuuaminisha ulimwengu kuwa nchi yake ni ya kidemokrasia.

https://p.dw.com/p/4dhdq
Urusi | Rais Vladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir Putin akilihutubia taifa mbele ya wajumbe wa Baraza la Bunge la ShirikishoPicha: Evgenia Novozhenina/REUTERS

Wakosoaji wamekuwa wakisema mara kwa mara kuwa Urusi ni taifa la kidikteta lakini hata hivyo, kati ya Machi 15 na 17, nchi hiyo inafanya uchaguzi wa rais. Vladmir Putin, ambaye amekuwa akiiongoza nchi hiyo kwa miaka 25 anatarajiwa kujishindia muhula wa tano madarakani na hivyo kusalia kwenye Ikulu ya Kremlin hadi angalau mwaka 2030.

Lakini watu wengi wanajiuliza ni kwanini rais Putin anaandaa uchaguzi ambao matokeo yake yanafahamika?

Ingawa watu wanaofuatilia kwa karibu siasa za Urusi wanasema kuwa Putin yuko tayari kujipatia ushindi wa kishindo, uchaguzi huu wa rais nchini Urusi una malengo mawili muhimu ya kushughulikia changamoto za ndani na nje zinazoukabili utawala wa Putin.

Soma pia: Warusi wapiga kura katika uchaguzi wa rais utakaodumu hadi Jumapili

Hayo ni kwa mujibu wa Konstantin Kalachev, mchambuzi wa masuala ya siasa na mshauri wa zamani wa Kremlin ambaye amesema kuwa ndani ya nchi, uchaguzi huu unatazamiwa kuthibitisha uhalali wa mamlaka ya rais Putin na kuonyesha kwamba watu wa Urusi wameshikamana kumuunga mkono kiongozi wao.  Aidha, Konstantin Kalachev amesema:

" Ni muhimu Kremlin kuonyesha kwamba Putin anatekeleza sera ya kigeni kulingana na matakwa ya watu wa Urusi, na anataka pia kuudhihirishia ulimwengu kuwa Warusi wameshikamana na wanamuunga mkono. Na hilo ni kwa dhamira ya kupambana na fikra anazoziona kuwa za udanganyifu za mataifa ya Magharibi za kwamba anakabiliwa na upinzani kutoka kwa raia wake."

Mikakati ya Kremlin ya kufanikisha zoezi hilo 

Urusi| Kituo cha kupigia kura katika uchaguzi wa rais
Msimamizi wa uchaguzi akipiga kura ya mapema katika kituo cha kupigia kura cha Kamchatka nchini UrusiPicha: Yelena Vereshchaka/TASS/dpa/picture alliance

Katika nchi ambayo karibu kila mtu anadhani kuwa matokeo yanafahamika hata kabla ya uchaguzi kufanyika,  inaweza kuwa vigumu kuwashawishi watu wengi zaidi kujielekeza kupiga kura. Lakini kama jarida huru la habari liitwalo Meduza la nchini Latvia lilivyoandika mapema mwezi, mamlaka za Urusi zimechukua hatua mbalimbali kuhakikisha kuwa uchaguzi wa urais unatoa picha ya kuwa wa huru na wa haki.

Soma pia:Raia wa Urusi wapiga kura ya rais 

Jarida hilo pia limesema, serikali mjini Moscow inalenga kupata angalau asilimia 80 ya idadi jumla ya wapiga kura. Ili kufanikisha hilo, utawala umepanga kuwahamasiha wapiga kura watiifu kwa serikali ambao ni wafanyakazi wa sekta ya umma, wafanyakazi wa mashirika ya serikali na makampuni makubwa, wakereketwa wa chama tawala pamoja na jamaa na marafiki zao.

Taarifa ya jarida hilo imefahamisha kwamba wanachama wa chama cha Putin cha "United Russia", wamehimizwa kuandamana na angalau watu 10 kwenye vituo vya kupigia kura. Maafisa wa serikali na wale wa chama tawala wanaweza kuona ni nani hasa aliyejitokeza kupiga kura kutokana na mfumo wa kielektroniki au nambari za kidijitali zinazowatambulisha  wapiga kura.

Katika hotuba yake ya kuelezea hali ya nchi aliyoitoa mbele ya Bunge la Shirikisho la Urusi mwishoni mwa mwezi Februari, Putin pia alisisitiza kuendeleza kile anachokiita "operesheni ya kijeshi nchini Ukraine."

Wafahamu wagombea urais nchini Urusi

Urusi | Mwanasiasa wa upinzani  Boris Nadezhdin
Mwanasiasa wa kiliberali Boris Nadezhdin, ambaye ni mtu pekee mwenye upinzani wa kweli, amezuiwa na Mahakama za Urusi kuwania urais Picha: Alexander Zemlianichenko/AP/picture alliance

Mwanasiasa wa kiliberali Boris Nadezhdin, ambaye ni mtu pekee mwenye upinzani wa kweli, amezuiwa kuwania urais na mahakama za Urusi, ikiwa ni pamoja na Mahakama ya Juu, baada ya kukata rufaa.

Wagombea wengine ni pamoja na Nikolai Kharitonov, 75, ambaye anawakilisha chama cha Kikomunisti nchini Urusi. Kwa kawaida mgombea wa chama hiki huwa wa pili baada ya Putin. Kharitonov amekosoa baadhi ya sera za ndani za Putin lakini anaunga mkono uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine.

Soma pia: Uchaguzi nchini Urusi unafanyika ikiwa katika vita na Ukraine

Mgombea mwingine ni Vladislav Davankov mwenye umri wa miaka 40, mwanasiasa huyo ni mmoja wa wagombea wenye umri mdogo zaidi na amekuwa akijinadi kama mliberali linapokuja suala la kuzuia uhuru wa watu nchini Urusi. Hata hivyo, Davankov amesema hatodiriki kuwakosoa wapinzani wake wa kisiasa.

Kulingana na shirika la habari la Reuters, Kharitonov na Davankov kila mmoja anaweza kupata kati ya asilimia 4 hadi 5 ya jumla ya kura.

Licha ya yote hayo, bado kunaweza kuwa na aina fulani ya kura za kudhihirisha upinzani kwa  utawala wa Putin  ingawa vigogo karibu wote wa upinzani wameikimbia Urusi lakini wamewataka wafuasi wao kuchukua hatua wakati wa uchaguzi. Kwa mfano, mjane wa kiongozi wa upinzani aliyefariki hivi majuzi Alexei Navalny, ametoa wito kwa wafuasi wake kujitokeza kwa wingi katika vituo vya kupigia kura na kuwataka kuandika jina la Navalny kwenye karatasi za kupigia kura.