Mzozo wa bei za mafuta duniani wamuumiza kila mtu. | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.06.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mzozo wa bei za mafuta duniani wamuumiza kila mtu.

Kila kukicha bei za mafuta ya petroli yaliosafishwa na yasiosafishwa zinazidi kupanda kote duniani. Nini cha kufanya?

Mkutano wa kilele wa Jeddah, Saudi Arabia, baina ya nchi zinazotoa na zinazotumia mafuta kwa wingi pamoja na makampuni makubwa ya mafuta.

Mkutano wa kilele wa Jeddah, Saudi Arabia, baina ya nchi zinazotoa na zinazotumia mafuta kwa wingi pamoja na makampuni makubwa ya mafuta.

Jee watu waelekeze zaidi juhudi zao katika nishati mbadala, kama ile inayotokana na nguvu za jua? Au suluhisho liko katika kuchimbua mafuta zaidi, au kwa serekali kupunguza kodi zinazotoza kwa mafuta hayo?

Hayo ni mambo yaliowashughulisha wakuu wa kutoka nchi 36 zinazotoa na zinazotumia sana mafuta duniani pale walipokutana na wawakilish wa makampuni makubwa 22 ya mafuta mwishoni mwa wiki iliopita katika mji wa Jeddah, Saudi Arabia. Watu hao walikubaliana na jambo moja, nalo ni kwamba uwekezaji uengezwe ili kuzidisha utoaji wa mafuta na kuweko uwazi katika bei za mafuta. Zaidi ya hayo, Saudi Arabia, nchi inayotoa mafuta kwa wingi sana, ilitangaza iko tayari kuengeza kutoa mafuta. Nayo Ujerumani, nchi inayotegemea mafuta ya kutoka nje, iliwakilishwa katika mkusanyiko huo na waziri wa uchumi, Michael Glos. Aliporejea nyumbani alionekana ameridhika na matokeo, yakiwemo mapatano kwamba kutaendelezwa mazungumzo baina ya nchi muhimu zinazotoa na zile zinazotumia mafuta.

Waziri wa mafuta wa Saudi Arabia, Ali al-Naimi, mwishoni mwa mkutano huo alisema kila nchi ifanye inachoweza ili kupunguza makali ya hali ilivyo sasa, japokuwa hajataja hatua gani zichukuliwe. Ila tu Mfalme Abdullah wa nchi yake alipoufungua mkutano huo alitoa ishara ya kuzituliza na kuzitoa wasiwasi nchi zinazotumia mafuta, akitaja kwamba nchi yake kutoka July Mosi mwaka huu itazidisha utoaji wa mafuta yake. Pia nchi yake imetenga kitita maalum cha fedha kuzisaodia nchi maskini ambazo zimeumia sana kutokana na kupanda bei za mafuta:

"Tangu kuundwa Jumuiya nchi zinazosafirisha ngambo mafuta, OPEC, msingi wa siasa ya Saudi Arabia ni kufikia bei ambayo haitawaumiza watoaji wala wateja wa mafuta. Kwetu sisi neema ya dunia ni kwa maslahi ya taifa letu. Siasa hiyo imekaririwa kulaumiwa. Tumezidisha kutoa mafuta mnamo miezi michache iliopita kutoka mapipa milioni tisa kwa siku na kufikia mapipa milioni 9.75; na sisi tuko tayari kutekeleza ombi lolote la ziyada."

Lakini waziri wa mafuta wa ufalme huo wa Saudi Arabia, Ali al-Naim, alisema pindi wateja wataomba basi nchi yake iko tayari kuchimba mafuta zaidi:

"Pale Saudi Arabia inapozidisha au inapopunguza kutoa mafuta, haifanyi hivyo hivi hivi tu, lakini kutokana na mahitaji ya wateja wake. Bila ya shaka, tunatimiza maombi ya wateja wetu. Kwa upande mwengine, hata hivyo, tunatumai nchi zinazotumia mafuta zitaambatana na kanuni fulani, kwa mfano, zitawekeza katika kujenga viwanda vya kusafishia mafuta na zitaruhusu kuchimbwa mafuta katika bahari na ardhi zao. Katika jambo hilo tunataka kuweko ushirikiano, na leo, kwa kweli, tumefikia makubalaino katika jambo hilo. Natumai makubaliano haya yatabakia. Pande zote mbili, watoaji na watumiaji wa mafuta, lazima washirikiane ili kuleta utulivu katika masoko, jambo hilo haliwezi kufanywa na upande mmoja tu."

Kwa nchi zinazotumia sana mafuta, hasa za Ulaya na zile za Amerika ya Kaskazini, ushirikiano huo ni muhimu ama sivyo kuna hatari ustawi wa maisha katika nchi hizo utapungua kutokana na miripuko ya bei za bidhaa ínayosababishwa na kupanda juu sana bei ya mafuta. Kuna baadhi ya wanauchumi, kama wa huko Uengereza, wanaozungumzia kwamba wafanya kazi itawabidi mwaka ujao wakubalie nyongeza za mishahara zilizo chini ya ughali wa maisha. Maisha, bila ya shaka, yatakuwa magumu.

Waziri mkuu wa Uengereza, Gordon Brown, aliyekuweko pia katika mkusanyiko wa Jeddah, alisema yaweza kwamba dunia hivi sasa inajionea mshtuko mwengine wa kupanda bei za mafuta, na huenda mshtuko huu ni mkubwa sana, kwani unaathiri hali za maisha ya watu. Lengo lake, alisema, ni kupunguza kutegemea mafuta, na kwamba nchi zinazotoa mafuta zitegemea mazao mengine, licha ya mafuta na anataka kuweko wizani ulio bora zaidi katika masoko ya mafuta. Huko Jeddah, alisema hivi:

"Napendekeza kwamba Uengereza na nchi nyingine zinazotumia mafuta zifungue masoko yao kwa uwekezaji mpya kutoka nchi zinazotoa mafuta, na pia kupitia akiba za kiserekali za uwekezaji, ili fedha hizo zitumiwe kwa ajili ya ina zote za kutafutia nishati, kama nishati hizo ni za mbadala au za kinyukliya. Kwa njia hiyo, nchi zinazotoa mafuta zitaweza kutengeneza mustakbali wao bila ya kutegemea mafuta. Kinyume na hayo, nchi zinazotoa mafuta ziwekeze kwa nguvu katika shughuli za kuchimba mafuta. Kwa njia hiyo tunaubadilisha mzozo wa zamani wa kimaslahi baina ya watoaji na watumiaji wa mafuta kuwa jamii kubwa ya kimaslahi baina ya nchi zinazotoa na zinazotumia mafuta."

Kwa mujibu wa waziri mkuu wa Uengereza, Gordon Brown, utaratibu huo utazipatia nchi hizo zinazotoa mafuta utulivu ambao unakosekana katika masoko ya mafuta. Alisema nchi hizo zina fedha nyingi ambazo zinabidi ziwekezwe katika kutafuta nishati ya mbadala.

Kwa kiasi gani nchi za Ghuba la Uarabu zitatilia maanani fikra hiyo ya Gordon Brown ni jambo lisilokuwa wazi bado. Pia sio wazi kama kweli nchi nyingine za Ghuba, kama vile alivosema Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia, zinataka kuweko na bei za mafuta zinazoingia akilini. Wanadiplomasia wa nchi za Magharibi walivunjika moyo, kwani , licha ya Saudi Arabia, hamna nchi niyngine inayotoa mafuta iliotoa ahadi madhubuti kwamba itaongeza kima cha utoaji wa mafuta yake, angalau kulituliza soko.

Kupanda sasa kwa bei kunatokana pia na wasiwasi ulioko kwamba Israel huenda ikashambulia vituo vya kinyuliya vya Iran, jambo ambalo litajibiwa vikali na watawala wa Tehran. Mzozo baina ya nchi hizo mbili utapelekea kufunguwa ujia wa maji wa Hormuz ulioko baina ya Iran na Bara Arabu na ambako yanapitia asilimia 40 ya mafuta yanayouzwa ngambo. Pia mashambulio ya watu wenye silaha katika eneo la kusini mwa Nigeria dhidi ya visima vya mafuta yamesababisha makampuni ya mafuta, kama vile Chevron kutoka Marekani na Shell ya Uholanzi na Uengereza, kusimamisha shughuli zao huko. Nigeria ni nchi inayotoa mafuta ya petroli kwa wingi kabisa barani Afrika, lakini miaka miwili iliopita imekuwa ikitoa robo ya kima ilichowekewa.

Bei ya mafuta ya petroli mwezi huu imekaribia dola 140 za Kimarekani kwa pipa moja, hivyo kuchochea malalamiko ya hasira katika nchi nyingi na kuweko hofu kwamba uchumi wa dunia utakuwa mashakani. kuangalia athari za kupanda bei za mafuta huko Afrika Mashariki, nilimuuliza kwa njia ya simu Soud Bargash, mmiliki wa kituo cha Petroli huko Mwembe Chai, Dar es Salaam, Tanzania:

Lakini Mfalme Abdullah wa Saudi Arabia alionya juu ya kusikiliza tu tetesi, na badala yake watu watafute sababu halisi za kupanda bei za mafuta:

"Kuna sababu nyingi ya kupanda haraka bei ya mafuta. Kwa sehemu kunatokana na ulanguzi katika masoko, kwa maslahi ya kibinafsi, mahitaji yanayozidi ya nchi zinazoinukia pamoja na kupanda kodi za mafuta katika baadhi ya nchi zinazotumia sana mafuta."

Suala kama ombi la wateja la kupatiwa mafuta zaidi litatimizwa na nchi zinazotoa, ni jambo litakaloamuliwa na nchi za jmuiya ya OPEC mwezi Septemba mwaka huu. Venezuela, Algeria na Iran zimeshatangaza kwamba zinapinga kuengezwa viwango vya utoaji kwa kila nchi mwanachama. Hata hivyo, neno la mwisho inayo nchi yenye mafuta mengi kabisa, nayo ni Saudi Arabia.

 • Tarehe 23.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EPUc
 • Tarehe 23.06.2008
 • Mwandishi Othman, Miraji
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/EPUc
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com