Mkutano wa wafadhili kuinua uchumi wa Palastina mjini Paris | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.12.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mkutano wa wafadhili kuinua uchumi wa Palastina mjini Paris

Wapalastina wanahitahji dala zaidi ya bilioni tano kukidhi mahitaji ya kiuchumi kabla ya kuundwa dola yao

default

Rais wa Palastina Mahmoud Abbas na waziri wa nje wa Israel Tzipi Livni

Wajumbe kutoka nchi na mashirika zaidi ya 90 wanakutana hii leo mjini Paris kwaajili ya kuwasaidia kifedha wapalastina waweze kutekeleza matakwa yao ya kuunda dola yao na kwa namna hiyo kuyapa nguvu matumaini japo dhaifu ya amani yaliyochomoza kufuatia mkutano wa kimataifa wa Annapolis-Marekani,mwishoni mwa mwezi uliopita.

Mawaziri kutoka mataifa 70 pamoja na mashirika kama 20 hivi au taasisi za kifedha za kimataifa,wanahudhuria mkutano huo wa Paris uliopewa jina “mkutano wa wafadhili kwaajili ya dola la Palasatina”.Lengo ni kukusanya dala bilioni tano na nusu zilizopendekezwa na utawala wa ndani wa Palastina ili kuwalipa wafanyakazi na kugharimia miradi ya kiuchumi ya taifa la siku za mbele la palastina kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice,waziri mwenzake wa Urusi,Serguei Lavrov na mwenzao wa Israel,Tzipi Livni wamemzunguka mkutanoni rais wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas ambae jana usiku alikaribishwa na rais Nicolas Sarkozy katika kasri la Elysée.

Akiufungua mkutano huo rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameahidi kuwapatia wapalastina msaada wa dala milioni 300 kusaidia kuundwa dola la Palastina.Rais Nicolas Sarkozy ameshauri pia “muda ukiwadia,kitumwe kikosi cha kimataifa kusaidia shughuli za vikosi vya usalama vya Palastina.”Usalama ndio ufunguo wa mamlaka” amesisitiza rais Sarkozy aliyeelezea matumaini ya kuona dola huru,la kidemokrasi na la kudumu la Palastina litakaloishi kwa amani pamoja na Israel likiundwa kabla ya kumalizika mwaka 2008.

Kwa upande wake kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas,baada ya kuishukuru Ufaransa na mataifa yanayoshiriki katika mkutano huu wa wafadhili,ametoa mwito misaada itolewe haraka ili kuepukana na kile alichokiita “Balaa”Rais mahmoud Abbas ametoa mwito pia wa kusitishwa harakati zote za ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika ardhi za wapalastina

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani bibi Condoleezza Rice aliyewasili tangu jana usiku mjini Paris,amenukuliwa akisema Marekani itawapatia wapalastina msaada wa zaidi ya dala milioni 550 mwakani.Ujerumani imeahidi pia kuchangia dala milioni 300.Kwa upande wa Umoja wa ulaya,kamishna anaeshughulikia uhusiano wa nchi za nje bibi Benita Ferrero-Waldner ameliambia shirika la habari la AFP kwamba halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya itaangaza msaada wad ala milioni 650 kwa mwaka 2008.

Mjumbe maalum wa tume ya pande nne inayosimamia utaratibu mpya wa amani ya mashariki ya kati,waziri mkuu wa zamani wa Ungereza Tony Blair amesema anaamini mahitaji ya wapalastina yatatekelezwa.

Mbali na mkutano huu wa wafadhili,mkutano mwengine pia,ule wa wawakilishi wa pande nne zinazosimamia utaratibu mpya wa amani ya mashariki ya kati,utafanyika pia hii leo mjini Paris.

 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CcfQ
 • Tarehe 17.12.2007
 • Mwandishi Oummilkheir
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CcfQ

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com