Mkutano wa kimataifa kuhusu uhalifu wafanyika Ujerumani | Masuala ya Jamii | DW | 20.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Mkutano wa kimataifa kuhusu uhalifu wafanyika Ujerumani

Matumizi ya nguvu, picha za ngono kwa watoto na ugaidi wa kimataifa ni miongoni mwa mada zinazojadiliwa katika mkutano wa siku mbili ulioanza jana (19 Oktoba 2010) mjini Wiesbaden hapa Ujerumani.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maiziere

Mkutano huu unaohudhuriwa na kiasi washiriki 500 kutoka kote ulimwenguni, umeitishwa na Idara ya Kupambana na Uhalifu ya Shirikisho la Ujerumani, BKA, kuangalia chanzo, maendeleo na mikakati ya kupambana na uhalifu huo.

Katika hotuba yake ya makaribisho hapo jana (19 Oktoba 2010), Rais wa BKA Jörg Ziercke alisema kwamba, takwimu za uhalifu wa matumizi ya nguvu zinatisha, lakini pakiwa na mashirikiano, jambo hili linaweza kutatuliwa kwa haraka.

"Si bahati mbaya kwamba masuala kama vile mashambulizi ya kigaidi, uhalifu wa matumizi ya nguvu unaosababishwa na kuruka kwa akili au misimamo mikali yameibuka. Kwa hakika kila kosa ambalo linafanyika kwa kiwango kikubwa kama hiki, basi lina sababu zake na ni muhimu kukutana kama hivi tukajaribu kuangalia namna ambavyo tunaweza kupunguza matatizo haya." Alisema Bwana Ziercke.

Rais wa BKA, Jörg Ziercke (kulia)

Rais wa BKA, Jörg Ziercke (kulia)

Katika hotuba yake ya ufunguzi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, Thomas de Maizière, alieleza matarajio ya Ujerumani kuuona ulimwengu wote uko salama. Hata hivyo, Waziri huyo alionesha kukasirishwa na tabia inayozuka sasa hapa Ujerumani ya matumizi ya nguvu dhidi ya polisi. Kumekuwa na visa ambapo makundi ya mrengo wa kushoto huwashambulia maafisa wa Polisi, jambo ambalo linaondosha imani ya watu kwa jeshi hilo, wakidhani kwamba linashindwa hata kujilinda lenyewe.

Waziri de Maizière alisema kwamba katika mwaka 2009 peke yake, palikuwa na visa zaidi ya 1500 kama hivyo, ambapo katika kisa kimoja, kundi la kiasi watu 15 lilikivamia kwa mawe kituo cha polisi cha Mtakatifu Pauli. Katika hali hii, akautaka mkutano huu, ujadili sio tu matumizi ya nguvu baina ya raia wenyewe kwa wenyewe, bali pia baina ya raia dhidi ya vyombo vya dola, ambavyo kimsingi vinapaswa kuwalinda.

Nukta nyengine muhimu ya mkutano huu ni suala la picha za ngono kwa watoto, ambalo linachangiwa sana na mawasiliano kwa njia ya mtandao. Mkutano utajadili njia za kuzuia uhalifu huu, ukiwemo uwezekano wa kuzuia matumizi ya mitandao yenye picha hizo kwa watoto. Hatua hiyo, bila ya shaka, itayahusisha masuala mengine kadhaa katika huduma ya mitandao, likiwemo lile la mabadiliko ya sheria zinazomlinda mtumiaji na mtowaji wa huduma hizi.

Kwa mujibu wa Waziri de Maizière, halitakuwa jambo la ajabu kuwa na sheria ambayo inagusa uhuru binafsi wa mtu, ikiwa tu kufanya hivyo kunanusuru maisha ya watoto ambao ni nguzo muhimu ya taifa. Kumekuwapo na mifano mingi hapa Ulaya, ambapo watoto wameingia katika mitego ya wahalifu, na wengine hata kupoteza maisha, kutokana na kufuata habari au mambo wanayoyaona kupitia mitandao.

Mkutano huu pia unaangazia suala la ugaidi wa kimataifa. Ujerumani inaangaliwa kama nchi ambayo magaidi wa wangependa kuishambulia wakati wowote, ingawa hadi sasa hakujakuwa na kitisho chochote cha moja kwa moja. Hivi karibuni, wizara ya Mambo ya Ndani ilipuuzia onyo la mashambulizi ya kigaidi lililotolewa na Marekani kwa raia wake wanaoitembelea nchi hii, lakini wizara hiyo ikaweka wazi kwamba ugaidi unaweza kutokea popote pale duniani, ikiwemo Ujerumani.

Mkutano huu wa siku mbili unafanyika katika majira haya ya Mapukutiko na unatarajiwa kuwa na mjadala mkali: masuala ya uhalifu wa kutumia nguvu, picha za ngono kwa watoto na ugaidi wa kimataifa, yote ni matatizo ambayo yanatakiwa kudhibitiwa na kutatuliwa na jeshi la polisi.

Lakini kama anavyosema de Maizière, polisi ni sehemu ndogo tu ya jamii kubwa na changamano.

"Naliweka hili kwenye mjadala, ikiwa kweli tunataka kufanikiwa kwenye mambo haya, basi duara dogo la maafisa wa polisi halitoshi. Ni lazima sio tu tuwawezeshe polisi hawa kwa vifaa na mafunzo, bali pia kwa jamii nzima kushiriki. Kwa mfano kama katika suala la picha za ngono kwa watoto, wajibu ni wa kila mtu."

Mwandishi: Mohammed Khelef/ZPR

Mhariri: Charo, Josephat

 • Tarehe 20.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pigp
 • Tarehe 20.10.2010
 • Mwandishi Admin.WagnerD
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Pigp
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com