Mkutano mkuu wa SPD wafunguliwa Berlin | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.12.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mkutano mkuu wa SPD wafunguliwa Berlin

Katika mkutano wao mkuu mjini Berlin , wawakilishi wa chama cha Social Democrat -,SPD, mbali na kuwaidhinisha viongozi wawili wapya, watafafanua vipi serikali kuu ya muungano itaweza kuendelezwa.

SPD kinaelekea wapi? Chama hicho kikongwe zaidi cha kisiasa nchini Ujerumani kinayumba yumba.Tangu mwaka 1998, pale wana Social Democrat walipojipatia zaidi ya asili mia 40 katika uchaguzi wa bunge, hali imebadilika. Hivi sasa chama hicho kinaondoka na kati ya asili mia 13 na 14 tu. Wafuasi wengi wa SPD wanaitwika serikali kuu ya muungano, jukumu la kuporomoka chama chao.Tangu mwaka 2005  hadi sasa SPD wanashirikiana kwa mara ya tatu na CDU/CSU serikalini. Imekuwa shidaa kugundua tofauti inayovitenganisha vyama hivyo huku SPD wakipoteza haiba yao, analalamika Saskia Esken, ambae pamoja na Norbert Walter-Borjans wameteuliwa kukiongoza kwa pamoja chama hicho.

Mwenyekiti mteule wa SPD Norbert Walter-Borjans akionyesha kidole gumba kabla ya mkutano mkuu kuanza

Mwenyekiti mteule wa SPD Norbert Walter-Borjans akionyesha kidole gumba kabla ya mkutano mkuu kuanza

Mabishano kati ya wanaounga mkono na wale wanaopinga serikali kuu ya muungano

Katika kinyang'anyiro cha kuania uongozi wa SPD, bibi huyo mwenye umri wa miaka 58, mbunge ambae hadi wakati huu hakuwa akijulikana na mwenzake , waziri wa zamani wa fedha katika jimbo la North Rhine Westphalia, mwenye umri wa miaka 67 hawakuficha msimamo wao dhidi ya serikali kuu ya muungano. Esken mara nyingi amekuwa akidai chama chake kitoke katika serikali ya muungano. Na pengine hiyo ndio sababu wanasiasa hao wanaoelemea mrengo wa kushoto wamechaguliwa mashinani wakiongoze chama cha SPD. Lakini tangu walipochaguliwa, wameregeza kamba. Badala yake wanazungumzia umuhimu wa kuzungumza na washirika wao serikalini kuhusu mabadiliko ya tabianchi na namna ya kuzidisha kiwango cha mishahara ya chini.

Wafuasi wa mrengo wa kushoto ndani ya chama cha Social Democrat wanataka mkondo mpya ufuatwe ili kurejesha imani ya wapiga kura.

Mkutano mkuu wa chama cha SPD unatishia kugeuka uwanja wa kupimana nguvu kati ya wanaotaka serikali kuu ya muungano iendelezwe na wale, ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wa tawi la vijana wa SPD, Kevin Kühnert, wanaotia kishindo  SPD ijitoe katika serikali hiyo ya muungano.

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com